Thursday, October 19, 2017

BANDARI YA BAGAMOYO KUANZA KARIBUNI.


Waziri wa Mafuta na Gesi kutoka Serikali ya Oman Dkt. Mohamed Bin Hamad Al–Rumhy (katikati) akiwa katika eneo ambalo linatarajiwa kujengwa Bandari ya Bagamoyo, wa pili kulia ni Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji wa Tanzania,  Mhandisi Stellah Manyanya  wakati wa ziara ya Waziri huyo katika maeneo ya uwekezaji kiuchumi (EPZA), wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Alhaji Majjid Hemed, Mkuu wa Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo.
 Mkuu wa Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo akimueleza Waziri wa Mafuta na Gesi kutoka Serikali ya Oman Dkt. Mohamed Bin Hamad Al–Rumhy kwamba jiwe la msingi limekaa miaka miwili toka kuwekwa kwake bila kuanza ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo. katika eneo la Mbegani Bagamoyo.
...................................

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo, amesema Bandari ya Bagamoyo ipo katika hatua za mwisho kuanza ujenzi.

Mhandisi Evarist Ndikilo aliyasema hayo leo Tarehe 19 Oktoba 2017 alipokuwa katika msafara wa waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman Dkt. Mohamed Hamad Al Rumhy ambe alikuwa na ziara ya kutembelea wilaya ya Bagamoyo kwa lengo la kuangalia maeneo ya uwekezaji pamoja na eneo litakalojengwa Bandari.

Alise kufuatia mazungumzo kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman wamekubaliana mambo ya msingi yatakayowezesha kuanza kwa ujenzi wa Bandari ya kisasa Bagamoyo.
Aliongeza kwa kusema kuwa pamoja na ujenzi wa Bandari kutakuwa na ujenzi wa viwanda makazi ya watu huduma mbalimbali za kijamii zitakazokuwa kwenye michoro ya kisasa ya kimataifa.

Mkuu huyo wa Mkoa wa Pwani alisema licha ya kuongea na Mh. Rais Magufuli, Waziri huyo wa Mafuta na Gesi wa Oman leo ameithibishia serikali ya Mkoa wa Pwani kuwa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo upo na utaanza hivi karibuni kwakuwa taratibu zote za awali zimeshakamilika.

Alisema serikali ya Mkoa wa Pwani na Serikali ya wilaya ya Bagamoyo kwa kushirikiana na wananchi wa vijiji vinavyozunguuka mradi huo wa Bandari watahakikisha Mradi huo unatekelezeka bila ya kikwazo chochote.

Mhandisi Ndikilo alisema wananchi wote wanaozunguka vijiji vya mradi wako tayari kuupokea Mradi huo na kwamba wanachosubiri ni utekelezaji tu.
Akizungumzia swala la fidia Mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Ndikilo alisema katika utekelezaji wa Mradi wa Bandari ya Bagamoyo hakuna mwananchiatakaedhulumiwa haki yake na kwamba kila anaestahiki kulipwa atalipwa ili kupisha mradi kwa salama na amani lakini pia yule ambae hana haki ya kulipwa serikali itahakikisha haitolewi fidia kwa mtu ambae hana eneo.

Kwa upande wake waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman alisema amefurahishwa na mapokezi aliyopata toka serikali ya Tanzania na kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli amesema serikali ya Tanzania iko tayari kwa kuanza kazi ya ujenzi wa Bandari kwa kushirikiana na wahisani wake ambao ni serikali ya Oman na China.

Alisema ameona jiwe la msingi limewekwa miaka miwili iliyopita lakini pia mkataba wa makubaliano umefanyika toka mwaka 2012 na kwamba sasa kilichobaki ni kuanza kazi tu.

Akizungumzia mahusiano ya kibiashara na fursa zilizopo nchini oman Waziri Dkt. Mohamed alisema Tanzania inayo nafasi kubwa ya kuzalisha bidhaa mbalimbali na kuziuza katika masoko ya Oman.

Alisema Ardhi ya tanzania ni nzuri na vinastawi vitu mbalimbali ambavyo oman vinahitajika kama vile unga wa muhogo na matunda aina mbalimbali
Nae Naibu waziri wa Viwanda Stela Manyanya amesema serikali ya Tanzania haina kikwazo chochote juu ya kupokea wawekeza na washirika wa maendeleo na kwamba mtu yeyote atakaejitokeza kuvuruga mipango ya serikali hatavumiliwa.

Balozi wa Tanzania nchini Oman Abdallaah kilima amesema watanzania wanapaswa kutumia fursa ya kibiashara iliyopo Oman ili kujipatia kipato kwa kuzalisha na kusafirisha mazao ya biashara.

Mkuu wa Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo akimuonyesha Waziri wa Mafuta na Gesi kutoka Serikali ya Oman Dkt. Mohamed Bin Hamad Al–Rumhysehemu ya Bahari ya hindi katika eneo linalotarajiwa kujengwa Bandari wilayani Bagamoyo .
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamoyo, Fatuma Latu akisalimiana na Naibu Waziri wa Utalii wa Oman Bi. Maitha Saif Majid Al- Mahrouqi, mara walipowasili katika eneo la Mbegani Bagamoyo.

Balozi wa Tanzania nchini Oman, Abdallah Kilima, akizungumza na waandishi wa Habari katika makumbusho ya Kaole Bagamoyo, mara baada ya Msafara wa ujumbe kutoka Oman kuwasili katika eneo hilo la kihistoria, wa kwanza kulia ni mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Alhaj, majid Mwanga, wapili ni Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman, Dkt. Mohamed Hamad Al Rumhy na wa kwanza kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo.

No comments:

Post a Comment