Saturday, October 14, 2017

RAIS MAGUFULI AGOMA KUUFUTA MWENGE WA UHURU



RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Magufuli ambaye leo Oktoba 14, 2017 alikuwa Mgeni Rasmi kwenye Maadhimisho ya Kumbukumbu ya kifo cha Rais wa kwanza wa Tanzania Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Kilele cha Mbio za Mwenge amesema amejisikia faraja kuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo ikiwa ni mara yake ya kwanza kushiriki maadhimisho hayo tangu awe Rais.

Aidha, Magufuli amemuelezea Hayati Mwl. Nyerere kama kiongozi shupavu aliyepigania maslahi ya wanyonge na kupambana na wakoloni katika kufanikisha kupatikana kwa Uhuru wa Tanganyika, Zanzibar na nchi nyingine za Afrika.

Amesema Nyerere alianza harakati za siasa mwaka 1953 baada ya kuchaguliwa kuwa Rais wa Chama cha TAA ambacho baadaye kilizaa TANU huku akiwa Mwalimu wa Shule ya Sekondari ambayo kwa sasa inaitwa Pugu Sekondari ambapo baadaye aliacha kazi hiyo ya kufundisha na kujikita kwenye siasa za ukombozi.

Rais Magufuli pia alisema iwapo Mwl. Nyerere angekuwa kiongozi mwenye tamaa au mbinafs, basi angechukua fukwe zote za Msasani, jijini Dar es Salaam na kuzifanya ziwe mali yake, lakini hakufanya hivyo kwa sababu ya uzalendo mkubwa aliokuwa nao.

Rais amesisitiza kuwa kamwe hatokukubali mbio za Mwenge wa Uhuru zifutwe katika kipindi chake cha uongozi, kwani mwenge huo una manufaa makubwa kwa Taifa ikiwemo kuzindua miradi mbalimbali za maendelo pamoja na kuwa nembo muhimu kwa Taifa letu.

Amesema wanaotaka mwenge huo ufutwe huenda hawajui historia ya nchi hii na kwamba kama wanaweza kukubali fimbo na kombe la dunia vikaletwa nchini na wakavipokea basi mbio za mwenge ni muhimu zaidi kuliko wanavyodhani.

Akizungumzia hali ya uchumi wa nchi, rais amekanusha wanaodai kuwa uchumi umeshuka huku akieleza kuwa uchumi wa Tanzania unazidi kupanda hukui mfumuko wa bei ukishuka na matokeo yake yanaonekana kwenye bidhaa pamoja na kushuka bei zake. Pia ameeleza kuongezeka kwa viwanda na wawekezaji wa kibiashara hapa nchini.

No comments:

Post a Comment