Thursday, October 19, 2017

OMAN YAAHIDI MAKUBWA KWA TANZANIA.



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman Dkt. Mohamed Hamad Al Rumhy alipokutana na kufanya naye mazungumzo Ikulu jijini Dar es salaam jana Oktoba 18, 2017
....................

Mfalme wa Oman Mtukufu Sayyid Qaboos bin Said Al Said amemhakikishia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kuwa nchi hiyo ipo tayari kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuongeza uwekezaji katika viwanda, uzalishaji wa nishati, kuongeza thamani ya madini, kuendeleza sekta ya gesi na mafuta na kuendeleza ukanda wa uwekezaji wa Bagamoyo ili kukuza uchumi kwa kasi zaidi.

Ujumbe huu wa Mfalme wa Oman umewasilishwa kwa Mhe. Rais Magufuli na Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman Mhe. Dkt. Mohammed Hamad Al Rumhy aliyeongozana na Waziri wa Uwekezaji wa Oman Mhe. Salem Ben Nasser Al Ismaily na Naibu Waziri wa Utalii Mhe. Maitha Saif Majid, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Dkt. Rumhy ambaye ameongoza watu zaidi 300 waliokuja nchini kwa meli ya Mfalme wa Oman amesema ziara hii imelenga kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Oman hususani katika masuala ya uchumi, ambapo Oman inabadilishana uzoefu na Tanzania kuhusu biashara ya mafuta na gesi, itajenga kiwanda kikubwa cha kuzalisha mbolea katika ukanda wa uwekezaji wa Bagamoyo, itajenga viwanda vya mazao na kununua mazao ya wakulima na itawekeza katika uchakataji wa madini ili kuongeza thamani.

“Mhe. Rais tunataka kushirikiana nanyi kuendeleza ukanda wa uwekezaji wa Bagamoyo, tunataka Bagamoyo isiwe eneo la bandari tu, bali pia liwe ni eneo ambalo tutajenga viwanda mbalimbali, tuzalishe mbolea na tununue mazao ya wakulima na kuyasafirisha, sisi tupo tayari na kesho tunakwenda kuangalia eneo hilo ili kazi zianze mara moja” amesema Dkt. Rumhy.

Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mfalme wa Oman Mtukufu Sayyid Qaboos bin Said Al Said kwa kutuma ujumbe huo na amemhakikishia kuwa Tanzania ipo tayari kuendeleza na kukuza zaidi uhusiano wake na Oman.

Mhe. Rais Magufuli amemtaka Dkt. Rumhy kufikisha ujumbe wake kwa Mfalme na wawekezaji wa Oman kuwa atafurahi kuona uwekezaji huo unaanza mara moja na kwamba Serikali itatoa ushirikiano wowote utakaohitajika kwa manufaa ya pande zote mbili.

“Mhe. Dkt. Mohamed naomba ukamwambie Mfalme kuwa namshukuru kwa ujumbe huu na namkaribisha sana Tanzania, nimefurahi kuona mpo tayari kushirikiana nasi kujenga viwanda, kuzalisha mazao na kuendeleza ukanda wa uwekezaji wa Bagamoyo, sisi tupo tayari hata leo, njooni tushirikiane kwa sababu nyinyi ni ndugu zetu na tutafanya uwekezaji kwa faida yetu sote” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli ametaka Oman iongeze ushirikiano na Tanzania katika masuala ya utalii na usafiri wa anga, kuwekeza katika usindikaji wa nyama na uvuvi na ushirikiano katika kubadilishana wataalamu wa nyanja mbalimbali wakiwemo walimu wa lugha ya Kiswahili na Kiarabu.

Amemshukuru Mfalme wa Oman kwa msaada kujenga visima vya maji 100 hapa nchini na amemuomba kuungana na Serikali katika safari yake ya kuhamia Dodoma kwa kujenga miundombinu itakayoweka kumbukumbu ya ushirikiano wa kidugu na kihistoria kati ya nchi hizi mbili.

Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard Matogoro Kalemani na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Suzan Alphonce Kolimba.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
18 Oktoba, 2017
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimsiliza Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman Dkt. Mohamed Hamad Al Rumhy akiongea na wanahabari baada ya kukutana na kufanya naye mazungumzo Ikulu jijini Dar es salaam jana Oktoba 18, 2017

No comments:

Post a Comment