Mhasibu wa Shule ya Sekondari ya Mtakatifu Joseph, Elizabeth Asenga
(40) amehukumiwa kulipa faini ya Sh 5 milioni ama kutumikia kifungo cha mwaka
mmoja jela baada ya kukutwa na hatia katika shitaka la kutuma ujumbe
wa kumkashifu Rais John Magufuli kupitia mtandao wa WhatsApp.
Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Huruma Shaidi, ametoa hukumu
hiyo leo Jumanne baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na mashahidi saba wa
upande wa mashtaka na utetezi uliotolewa na mshtakiwa mwenyewe na kumhukumu
mshtakiwa huyo kulipa faini ya Sh 5 milioni ama kutumikia kifungo cha mwaka
mmoja jela.
Hata hivyo, mshtakiwa huyo alifanikiwa kulipa kiasi hicho cha fedha na
kukwepa adhabu ya kifungo.
Kesi hiyo namba 317 ya 2016 mshtakiwa huyo alidaiwa kuwa Agosti 6, 2016,
aliwasilisha ujumbe wenye mazingira ya kumkashifu Rais Magufuli kwa njia ya
WhatsApp kwenye kundi la kijamii liitwalo STJ Staff Social Group.
Mshtakiwa huyo aliandika ujumbe usemao: ‘Godmorning humu. hakuna Rais
kilaza kama huyu wetu duniani, angalia anavyompa Lissu umashuhuri, fala lile,
picha yake ukiiweka ofisini ni nuksi tupu. Ukiamka asubuhi, ukikutana na picha
yake ya kwanza siku inakuwa mkosi mwanzo mwisho.”
Baada ya kusomewa shitaka hilo alikana na alikuwa nje kwa dhamana
kwa kuwa na wadhamini wawili ambao kila mmoja wao alisaini hati ya
dhamana ya maneno ya Sh 2 milioni.
CHANZO: FULL SHANGWE BLOG.
No comments:
Post a Comment