Ndugu Wananchi,
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kwa
kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta zinazohusika na Usafi na Afya
Mazingira inaungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha Siku ya Unawaji Mikono
(Global Hand Washing Day). Siku hii huadhimishwa tarehe 15 Oktoba ya kila mwaka
kwa lengo la kuhamasisha jamii kuongeza uelewa na ufahamu zaidi wa umuhimu wa
unawaji mikono kwa maji tiririka na sabuni kama njia madhubuti na rahisi katika
kudhibiti magonjwa yanayoweza kuenezwa na mikono iliyochafuliwa na vimelea
mbalimbali vya magonjwa.
Nchi yetu imekuwa ikiadhimisha siku hii tangu mwaka
2011 ambapo shughuli mbalimbali zenye kulenga kuhamasisha jamii zimekuwa zikifanyika.
Ndugu Wananchi,
Tunapokumbushia kila mwaka juu ya umuhimu wa unawaji wa mikono katika
siku hii, ni kwa ajili ya kutia chachu katika jamii yetu juu ya manufaa
yapatikanayo kutokana na kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni.
Umuhimu huu
unakwenda sanjari na ukweli kwamba kutozingatia kanuni za tabia binafsi za
usafi hupelekea kuenea kwa magonjwa. Ni dhahiri kuwa mikono michafu huchangia
kwa kiasi kikubwa kuenea kwa magonjwa kama vile kuhara, kuhara damu, magonjwa
ya macho na ngozi pamoja na maambukizi ya mfumo wa hewa kama vile mafua
na homa ya mapafu (pneumonia) ambayo kwa kiwango kikubwa, yanaweza kuepukika
ikiwa tabia ya unawaji wa mikono ikizingatiwa ipasavyo.
Ndugu Wananchi,
Tafiti mbalimbali za hivi karibuni zinaonesha kuwa vyanzo vikuu viwili
vya vifo vya watoto katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania ni magonjwa ya
kuhara na maambukizi ya mfumo wa upumuaji. Kitendo rahisi cha kunawa mikono kwa
sabuni kinaweza kuondoa takribani nusu ya hatari ya uambukizwaji wa magonjwa ya
kuhara na takribani theluthi ya maambukizi ya mfumo wa upumuaji. Hali hii
inabainisha kunawa mikono kuwa ni chaguo bora zaidi na rahisi katika kuzuia
maambukizi ya magonjwa.
Ndugu Wananchi,
Kunawa mikono na kuzingatia kanuni nyingine za usafi ikiwemo matumizi ya
vyoo bora na maji safi na salama ya kunywa kwa ujumla wake vimebainika kuwa
afua muhimu katika jamii yetu hasa kwenye makuzi ya watoto.
Takwimu zinaonesha
kuwa asilimia 30% ya udumavu wa mwili kwa watoto katika nchi yetu unasababishwa
na kutokuzingatia kanuni za usafi. Hali hii inaweka changamoto zinazogusa
nyanja za uchumi, maendeleo ya nchi na ustawi wa jamii kwa ujumla.
Jamii
inapokuwa na afya njema kunakuwa na manufaa ya kuongeza tija ya uzalishaji
mali. Licha ya kuwa zoezi hili linaweza kuonekana dogo lakini kwa upande wa
afya ni kubwa hasa katika kuzuia maambukizi ya magonjwa kwenye vituo vyetu vya
afya.
Takwimu zinaonyesha kuwa kunawa mikono kwa maji na sabuni kunaweza
kupunguza magonjwa yanayoweza kutokea kwenye vituo vya afya (Hospital Acquired
Infections) kwa asilimia 50%.
Ndugu Wananchi
Wahenga walisema Samaki
mkunje angali mbichi, methali hii inatukumbusha jukumu tulilonalo la kuwafundisha watoto na
vijana wetu umuhimu wa usafi binafsi hususani unawaji wa mikono kwa sabuni.
Tafiti za kisayansi zinathibitisha kuwepo kwa uhusiano wa ongezeko la
mahudhurio ya wanafunzi shuleni na uboreshaji wa miundobmbinu ya maji na usafi
wa mazingira katika shule husika.
Takwimu zinaonyesha kuwa ni asilimia ndogo tu
ya shule za msingi ndizo zina vifaa vya kunawia mikono. Hii ina maana kuwa
tunahitaji kuboresha hali ya usafi wa mazingira katika shule ili matokeo
makubwa sasa yaweze kufikiwa katika sekta ya Elimu.
Hivyo, ninapenda kutoa wito
kwa jamii kushirikiana na serikali kuhakikisha kuwa kila shule nchini inakuwa
na huduma ya vyoo bora na pia sehemu maalum za kunawa mikono ili kuwakinga
wanafunzi dhidi ya maradhi yanayoenezwa kwa njia ya uchafu.
Ndugu Wananchi,
Kauli mbiu ya Siku ya Kunawa Mikono kwa mwaka huu ni “Mikono Safi kwa
Manufaa ya sasa na ya Baadaye!” ambayo kwa kiingereza ni“Our Hands, Our Future!”, Kauli mbiu hii imejikita katika kusisitiza jamii yetu kwa ujumla wake
kujenga tabia ya kunawa mikono nyakati zote muhimu hali inayoweza kuokoa maisha
na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi .
Unawaji wa mikono ninaufananisha
na chanjo ambayo mtu anajichanja mwenyewe.
Hii inatokana na ukweli usiopingika
wa manufaa katika kuzuia magonjwa ambayo nimekwisha yataja hapo mwanzo.
Vilevile, kauli mbiu hii inatupa fundisho zaidi za kulinda afya zetu na vivyo
hivyo kutuwezesha kuimarisha afya yetu, familia na jamii kwa sasa na baadaye
ili kujiweka tayari kwenye uzalishaji viwandani, mashambani na maofisini.
Ndugu Wananchi,
Afya bora kupitia usafi wa mikono ni moja ya misingi ya kuitambua
jamii kuwa ni wastaarabu. Hatuwezi kuwa na afya bora kama hatujawekeza kwenye
masuala muhimu ya kulinda afya zetu.
Hali ya unawaji mikono katika Bara letu la
Afrika si wa kuridhisha kwani imebainika kuwa nchi nyingi zina wastani wa chini
ya asilimia 50%. Kwa upande wa nchi yetu ni asilimia 12% tu ya kaya zina vifaa
vya kunawia mikono vinavyofanya kazi. Takwimu hizi zinadhihirisha kuwa kati ya
watu 100 ni kumi 12 hunawa mikono.
Mtakubaliana nami kuwa kupitia utamaduni
tuliojijengea wa kusalimiana kwa kushikana mikono unaweza ukapima namna ambavyo
tunaweza kuambukizana magonjwa kwa njia hii. Wito wangu kwenu wananchi ni kila
mmoja wetu azingatie tabia ya kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni kwa
manufaa yetu sote.
Ndugu Wananchi,
Neno ustaarabu lina maana pana hasa katika kipimo cha maandeleo kwani
ustaarabu unajumuisha usafi katika nyanja zote. Kwa muktadha huu, ni matumaini
yangu unapoitwa mstaarabu katika jamii yetu tambua kwamba wewe ni miongoni mwa
watu wasafi wanaozingatia kanuni zote za afya.
Ni matumaini yangu sote kwa
pamoja tutabadilika katika kuhakikisha kaya zetu zinakuwa na vifaa vya kunawia
mikono nyakati zote muhimu ambazo ni KABLA YA KULA, KABLA YA KUANDAA CHAKULA,
BAADA YA KUTOKA CHOONI, BAADA YA KUMSAFISHA MTOTO ALIYEJISAIDIA NA KABLA YA
KUMLISHA MTOTO.
Mwisho
Kutokana na hali hii niliyoieleza, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto na wadau imejipanga kutumia njia mbalimbali ambazo
zitasaidia kupunguza tatizo la uchafu katika mazingira yetu ikiwemo unawaji wa
mikono.
Ili kukabiliana na tatizo la uchafu wa Mazingira nchini, Serikali kwa
kushirikiana na wadau wa maendeleo inatekeleza Kampeni ya Taifa ya Usafi wa
Mazingira.
Kupitia Kampeni hii tunatarajia kuongeza idadi ya kaya zitakazo kuwa
na vifaa vya kunawia mikono angalau kwa zaidi ya asilimia 50% toka asilimia 12%
ilivyo sasa hadi asilimia 50% ifikapo 2021.
Kupitia kauli mbiu ya NIPO TAYARI
ya Kampeni hii ninamtaka kila mmoja wetu awe tayari kubadilika na kuzingatia
usafi kwa ujumla wake.
Aidha, nitoe rai kwa wadau mbalimbali na jamii kwa
ujumla kushiriki kikamilifu katika kutekeleza Kampeni ya Taifa ya Usafi wa
Mazingira, kwani ni kwa manufaa yetu wenyewe na vizazi vijavyo.
Itakuwa faraja kubwa kwangu na Serikali kwa ujumla endapo kila
Mji/Kata/Mtaa/Kijiji na Kitongoji kitashirikisha wananchi wake katika shughuli
za usafi wa mazingira ikiwa ni pamoja na kuhamasisha uwekaji wa vifaa vya
kunawia mikono. Hali kadhalika, Viongozi na Wataalam Afya Mazingira waendelee
kuwa mstari wa mbele kuhimiza suala hili kwenye jamii.
Nimatumaini yangu kwamba
tutakapoadhimisha Siku ya Matumizi ya Choo Duniani na Wiki ya Usafi tarehe 19
Novemba, 2017 elimu na hamasa kuhusu kunawa mikono kwa maji na sabuni kutakuwa
kumezoeleka.
Ahsanteni kwa kunisikiliza
No comments:
Post a Comment