Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto inapenda kutoa taarifa kwa umma, kuhusu kuwepo ugonjwa wa tauni katika
nchi ya Madagascar kuanzia Agosti, 2017.
Taarifa kutoka Shirika la Afya Duniani
(WHO) imeeleza kuwa nchini Madagascar mikoa minane (8) imeripoti kupata
wagonjwa ikiwa ni pamoja na Antananarivo ambao ni Mji mkuu wa Madagascar, Sava,
Tamatave/Atsinanana na Majunga /Boeny. Kati ya Agosti 23 hadi Septemba 28 mwaka
huu, wagonjwa 104 wameripotiwa na kati yao ishirini (20) wamepoteza maisha (CFR
19.2%).
Wagonjwa wengi walioripotiwa wameonyesha kuwa na
uhusiano kwa njia moja au nyingine na mgonjwa wa kwanza, jambo linalothibitisha
kuwa yapo maambukizi ya ugonjwa wa tauni kati ya binadamu na binadamu. Hivyo,
kwa mujibu wa WHO, upo uwezekano wa kadri (moderate risk) wa ugonjwa huo
kusambaa katika nchi jirani na Madagscar.
Tahadhari hii inatolewa kwa kuzingatia kwamba nchi
ya Madagascar haiko mbali sana na Tanzania, na inawezekana kukawa na
muingiliano kati ya wananchi wa Tanzania na wale wa Madgascar. Inasisitizwa
kwamba kwa sasa hapa nchini Tanzania hakuna mgonjwa yeyote aliyeripotiwa.
UGONJWA WA TAUNI
Ugonjwa huu unasababishwa na bakteria anayejulikana
kitaalam kama “Yersinia pestis”, ambaye hupatikana katika baadhi ya
wanyama wadogo kama vile panya, paka na mbwa na viroboto. Ziko njia kuu tatu
ambazo mtu anaweza kupata maambukizi:
1.
Kung’atwa na
viroboto vyenye maambukizi ya bakteria hao kutoka kwa wanyama kama mbwa na paka
ambao huweza kubeba viroboto hawa.
2.
Kugusana bila
kuwa na vikinga mwili na majimaji yenye vimelea vya bakteria kutoka kwa mtu/mnyama
aliyeathirika kwa njia ya kugusa sehemu zenye vimelea zilizochafuliwa na
mgonjwa/mnyama na kasha mtu huyo kujigusa mdomomi au puani.
3.
Kugusana na
majimaji yanayotoka kwa mgonjwa kwa njia ya kukohoa au kupiga chafya bila ya
mgonjwa huyo kufunika pua au mdomo.
Ugonjwa wa tauni hujitokeza kwa aina kuu tatu:
1.
Kuathiri
mitoki (Bubonic plague):
Mgonjwa hupata homa, kusikia baridi, mwili kukosa
nguvu na mitoki kuvimba katika makwapa na mapaja.
Mgonjwa asipotibiwa ugonjwa
husambaa sehemu nyingine za mwili. Aina hii hutokea baada ya mtu kuumwa
na viroboto au kuhudumia mnyama aliyeathirika.
1.
Maambukizi
katika damu (Septicemic plague)
Mgonjwa hupata homa, kusikia baridi, mwili kukosa
nguvu kabisa, maumivu ya tumbo, ngozi kuvia damu pamoja na viungo vingine. Aina
hii hupatikana kwa kuumwa na viroboto au kuhudumia mnyama aliyeathirika.
1.
Tauni
inayoathiri mfumo wa hewa (Pneumonic plague):
Mgonjwa hupata homa, kichwa kuuma, mwili kuishiwa
nguvu na kupata kichomi (nimonia) kikali na kupumua kwa shida.
Pia hukohoa na
kupata maumivu ya kifua. Hii huambukizwa kwa kuvuta hewa au majimaji ya mfumo
wa hewa kutoka kwa mgonjwa, au endapo aina mbili za hapo juu hazikutibiwa
kikamilifu na vimelea vikashambulia mapafu. Aina hii ni hatari sana na ni aina
pekee inayoweza kuambukizwa toka kwa binadamu aliyeambukizwa kwenda kwa
mwingine. Aina hii ndiyo imethibitishwa kuwepo huko Madagascar kwa wakati huu.
Kwa bahati nzuri ugonjwa wa Tauni unatibika hivyo ni
muhimu kuwahi katika vituo vya kutolea huduma ya afya mara mtu anapoona dalili.
HATUA ZINAZOCHUKULIWA NA WIZARA KATIKA KUZUIA
UGONJWA HUU USIINGIE NCHINI.
Hatua zifuatazo zimechukuliwa baada ya kupata
taarifa ya tahadhari ya ugonjwa huu kutoka WHO hapo Septemba 29, 2017;
- Kuandaa barua za tahadhari za ugonjwa huu kwa Makatibu Tawala wa mikoa yote ya Tanzania Bara kwa ajili ya kuwataarifu na kuwataka kuchukua tahadhari.
- Kuimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa katika viwanja vya ndege, mipakani pamoja na bandari ili kubaini wagonjwa waingiao nchini wakiwa na dalili za ugonjwa huo.
- Kupitia kwa Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Wizara inatoa maelekezo ya kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji na utambuzi wa magonjwa (Surveillance) katika vituo vya kutolea huduma nchini kote.
- Wizara itatoa elimu kwa jamii kuhusu ugonjwa huu.
Ili kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huu jamii inaaswa
kuzingatia yafuatayo:
1.
Kuwahi katika
vituo vya kutolea huduma za afya mara wanapoona dalili.
2.
Kuimarisha
usafi wa mazingira.
3.
Kudhibiti
viroboto kwa dawa.
4.
Kudhibiti
panya katika makazi yetu.
5.
Mazao
yahifadhiwe vizuri kuepuka kuwavutia panya kuja katika makazi yetu.
6.
Wanyama
waogeshwe kama inavyoelekezwa na wataalam wa mifugo ili kuepuka viroboto
ambavyo hubeba vimelea vya tauni.
7.
Kuacha
utaratibu wa Binadamu kukaa nyumba moja na wanyama.
Hitimsho
Serikali inasisitiza kuwa mpaka sasa ugonjwa wa
tauni haujaingia hapa nchini. Kwa kuwa magonjwa hayaangalii mipaka, tunahitaji
kuchukua tahadharii madhubuti ili kuzuia ugonjwa huu usiingie hapa nchini.
Hivyo wananchi wanahimizwa kuzingatia kanuni za afya za kuzuia ugonjwa huu, pia
wanatakiwa kuripoti haraka kwenye vituo vya kutolea huduma za afya mara waonapo
dalili zozote za ugonjwa huu.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini – Afya
03 Oktoba, 2017
No comments:
Post a Comment