Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Alhaj, Majid Mwanga
amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chalinze kufuatilia wanafunzi wote
waliopata mimba na kushindwa kuendelea na masomo ili kuwachukulia hatua za
kisheria wazazi, pamoja na wanaume ambao wamewatia mimba.
Akizungumza katika mahafali ya 10 ya wanafunzi
waislamu wanaosoma katika katika shule ya Sekondari Chalinze, Mkuu huyo wa
wilaya alisema zipo badhi ya kesi zinaendelea mahakamani na kwamba lengo ni
kuhakikisha kila aliyehusika kwa namna moja au nyingine kukatisha masomo ya
mwanafunzi anachukuliwa hatua stahiki za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine
wenye tabia kama hizo.
Aidha, alisema katika wilaya ya Bagamoyo Tarafa
ya Chalinze ndio inayoongoza kwa kwanafunzi kukatisha masomo kwasababu ya
kupata mimba hivyo amemuagiza Afisa Tarafa wa Tarafa ya Chalinze kupata takwimu
ya wanafunzi waliokatisha masomo yao katika Tarafa hiyo.
Akizungumzia maadili katika jamii mkuu huyo wa
wilaya ya bagamoyo aliwataka mabinti wa kiislamu kuvaa mavazi ya stara katika
maisha yao ya kila siku ili kuepuka vishawishi kwa wanaume hali itakayopelekea
kukatisha masomo yao na kupata magonjwa ya zinaa ikiwemo UKIMWI.
Alisema jamii inapaswa kutambua kuwa UKIMWI bado
upo na kwamba njia kubwa inayopelekea kupata maambukizi ya VVU ni kufanya zinaa
hivyo aliwataka vijana kuepuka starehe ambazo zitakatisha ndoto zao na ndoto za
wazazi wao.
Kwa upande wake Mjumbe wa Baraza la ulamaa
BAKWATA wilaya ya Bagamoyo, sheikh Simba Aboubakari aliwataka vijana
wanaomaliza elimu ya sekondari waonyeshe tofauti kati yao na wale ambao
hawakufika ngazi hiyo ya elimu.
Alisema Elimu bora ni ile inayompelekea mtu kuwa
na tabia njema, madili mema yanayotafsiriwa kwa vitendo katika jamii
inayomzunguuka.
No comments:
Post a Comment