Rais
mstaafu wa awamu ya nne ,Dk.Jakaya Kikwete, akionekana pichani ,wakati
akizungumza na viongozi mbalimbali wilayani Kibaha na Mkoa wa
Pwani,walimu,wanafunzi na wazazi wa wanafunzi wa shule ya sekondari Kibaha,huko
shirika la elimu Kibaha.(picha na Mwamvua Mwinyi)
...............................
Na Mwamvua Mwinyi-Kibaha
RAIS mstaafu wa awamu ya nne ,Dk.Jakaya Kikwete ,amesema uwepo wa walimu
maalum wa kufundisha somo la michezo katika shule mbalimbali itasaidia
kuibua vipaji kwa wanafunzi na kujenga afya zao .
Ameeleza vipo vipaji vingi vya michezo tofauti tofauti vilivyojificha
mashuleni ambapo endapo vitaibuliwa vitawezesha kupata wana michezo bora
watakaotumika kuliletea sifa Taifa .
Dk Kikwete aliyasema hayo shirika la Elimu Kibaha ,wakati akizungumza na
wazazi ,wanafunzi ,walimu na viongozi mbalimbali ,katika shule ya sekondari
Kibaha.
Alieleza ,shule ya sekondari Kibaha ndipo alipogundua na kuibua kipaji
chake cha kucheza mpira wa kikapu .
“Nilikuwa nikitumainiwa na walimu wangu wa michezo ,ndio waligundua
kipaji changu kipo kwenye mpira huo,nilikuwa nikitumainiwa na walimu wangu “
“Kama kuna mechi nje ya shule,sekondari ya Pugu ,Azania ilikuwa lazima
niende ,nikiugua mwalimu wangu anasema haikubaliki ilikuwa lazima niende na
tushinde .” alisema Dk.Kikwete .
Dk Kikwete alifafanua pia alikuwa bingwa wa riadha shuleni licha ya yeye
kupenda mchezo wa mpira wa miguu .
“Nilikuwa nikipenda sana mpira wa miguu lakini kumbe kipaji changu
kilikuwa kwenye basketball “; Hapa nachotaka kusema ni kwamba somo la michezo
katika shule zetu litasaidia kuibua vipaji kwa watoto wetu” alisema .
Alielezea kwamba ,shule ya sekondari Kibaha ilikuwa ikiwika na kuongoza
kwa michezo nchini .
Dk.Kikwete alisema ,shule hiyo ilikuwa ikitumika viwanja vyake vya
michezo mbalimbali ,na kuwa na walimu maalum wa somo la michezo .
Alifurahi kusikia bado viwanja hivyo vinaendelea kutumika na kuwepo na
walimu wa somo hilo lakini aliusihi uongozi wa shirika kusimamia suala la
michezo shuleni humo .
Hata hivyo ,rais huyo mstaafu hajafurahishwa kusikia kuna upungufu wa vifaa
vya michezo shule ya sekondari Kibaha jambo ambalo aliahidi kuangalia namna ya
kusaidia vifaa hivyo ili kurejesha sifa iliyokuwepo awali shuleni hapo .
Dk.Kikwete alisema ,mamlaka husika pia imesikia ,na itatatua changamoto
hiyo .
Awali mwalimu mkuu wa shule ya sekondari Kibaha ,Chrisdom Ambilikile
,alisema shule inakabiliwa na upungufu wa vifaa vya kimichezo ikiwemo mipira ya
michezo mbalimbali na sare .
No comments:
Post a Comment