Tuesday, October 17, 2017

UJUMBE KUTOKA OMAN MATUMAINI BANDARI YA BAGAMOYO.


Meli ya iliyobeba ujumbe kutoka Oman ijulikanayo kwa jina la Fulk Al Salamah ikiwasili katika bandari ya Dar es Salaam ikiwa na ujumbe wa watu takribani 350 kutoka Oman.
.....................................
MAKALA MAALUM YA BAGAMOYO.

Ujio wa ujumbe huo kutoka Oman Hapa nchini ni matumaini mapya kwa wananchi wa Bagamoyo na watanzania kwa ujumla kwani Oman ni wahisani washirika wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo.

Akizungumza na waandishi wa Habari mara baada ya kupokea ujumbe huo kutoka Oman, Waziri wa viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage alisema ujio wa ujumbe huo ni fursa nyingine kwa Tanzania kuimarisha mahusiano baina ya Oman na Tanzania.

Alisema ujumbe huo utafanya mazungumzo na serikali ya Tanzania katika nyanja mbalimbali za uwekezaji ikiwa ni pamoja na ujenzi wa viwanda pamoja na Bandari ya Bagamoyo.

Jiwe la msingi la ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo limewekwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya nne Mh. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete Tarehe 16 Oktoba 2015 muda mfupi kabla ya kuondoka madarakani.

Katika hutuba yake aliyoitoa Mbegani Bagamoyo, Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete alisema ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo utajengwa kwa ushirikiano kati ya nchi tatu Oman, China na wenyeji Tanzania na unatarajiwa kugharimu dola Bilioni kumi.

Bagamoyo ndio sehemu iliyotengwa kwaajili ya uwekezaji wa kimataifa ambapo limetengwa eneo maalum la kiuchumi, Special Economic Zone, (SEZ) na eneo Maalum la Viwanda Bagamoyo ambalo lipo chini ya The Export Processing Zone Authority  (EPZA).

Katika ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo Mamlaka ya Bandari nchini, Tanzania Ports Authority (TPA) ilishafanya uchambuzi yakinifu toka mwaka 2010 na kuandaa sehemu ya kujenga lango kubwa la kuwezesha meli kuingia ambalo lango hilo linatarajiwa kuwa na ukubwa wa Cubic Metre 25,000,000.

Katika kuhakikisha kuwa ujenzi  wa Bandari ya Bagamoyo unakamilika kama ilivyokusudiwa na kuandaa miundombinu wezeshi itakayokabiliana na ukubwa wa mji wa Bagamoyo na kuweza kusafirisha mizigo itakayofikia katika Bandari ya Bagamoyo.

Serikali imepanga kuipanua Barabara ya Tegeta-Bagamoyo kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita 43.2 na upana wa kupita gari mbili kila upande.

Barabara nyingine inayatarajiwa kujengwa katika kiwango cha lami ni ile inayotoka daraja la Makofia-Mlandizi yenye urefu wa kilomita 36.7 na Barabara ya Mbegani -Bagamoyo Mjini yenye urefu wa kilomita 7.2 nayo itajengwa kwa kiwango cha lami.

Sambamba na ujenzi wa Barabara za lami Reli pia ni muhimu katika kusafirisha mizigo itokayo Bandarini ambapo serikali imepanga kujenga Reli itakayotoka Mpiji hadi Bagamoyo yenye urefu wa kilimita 60.

Ujenzi wa Viwanda na maendeleo mengine yanahitaji umeme, katika kuhakikisha umeme TANESCO chini ya Wizara ya Nishati inatarajia kupeleka umeme mkubwa chini ya mradi wa North East -3 ambao utaweza kutoa jumla ya 220 KV ikiwa ni pamoja na kuongeza nguvu umeme wa wa eneo la Zinga kufikia mpaka 132 KV.

Aidha, TANESCO wanatarajia kuweka Power plant eneo la Zinga yenye uwezo wa kuzalisha takriban Megawatt 200.

Lakini pia TANESCO ili kuhakikisha umeme huu unakuwa wa uhakika wanatarijia kujenga Bomba la gesi kutoka Tegeta hadi Bagamoyo eneo la Viwanda.

Kuhusu maji ya uhakika DAWASCO wanatarajia kusambaza maji kutoka vyanzo vyake ikiwa ni pamoja na kujenga Bwawa la maji katika mto Ruvu litakalokuwa na uwezo wa kuhifadhi maji jumla ya ujazo wa lita milioni 190.

Upande wa mawasiliano TTCL wanatarajia kuunganisha eneo la viwanda Bagamoyo kwenye mkongo wa taifa kwa upande wa kutoka Chalinze - Bagamoyo ikiwa ni pamoja kuweka mawasiliano yenye kasi ya 4G kwaajili ya matumizi ya ofisi na majengo katika eneo hilo la viwanda Bagamoyo.

Mikakati hii na mingine mingi itakayoivusha bagamoyo kutoka hapa ilipo na kufika mbali kiuchumi, kimaendeleo na Teknolojia imeshajadiliwa na wadau wa sekta mbalimbali wa ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha malengo haya yanafikiwa.

Katika kikao ambacho kilikaliwa Tarehe 22 Juni 2016 Ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere kilichojumuisha Makatibu wakuu, Wakuu wa Taasisi na Wakala mbalimbali za Serikali zinazoshiriki katika kutekeleza mradi wa eneo la viwanda Bagamoyo kilijadili kwa kina mikakati ya kufika malengo haya ya kuimarisha miundombinu wezeshi kwa mji wa Viwanda na uwekezaji Bagamoyo.

Ni matumaini yetu kuwa mipango hii madhubuti iliyopangwa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itatekelezwa na kuifanya Bagamoyo na Tanzania kwa ujumla ipige hatua katika sekta ya uwekezaji na Viwanda hasa kwa kuanza na kukamilika kwa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo.

imeandaliwa na Mwandishi
Athumani Shomari Mkwama
0715483123
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage akiteta jambo na Balozi wa Oman hapa nchini Mhe. Ali A. Al Mahruqi walipokutana katika hafla ya mapokezi ya meli iliyobeba ujumbe kutoka kwa mfalme wa Oman uliowasili katika bandari ya Dar es Salaam leo. Katikati ni Mfanyabiashara wa Tanzania Seif A. Seif.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Dkt. Hussen Mwinyi akimpokea Waziri wa Mafuta na Gesi toka Oman Dkt. Mohamed Hamed  Al- Rumhi ambaye ndiye kiongozi wa ujumbe kutoka kwa mfalme wa Oman uliowasili na meli ya mfalme ya Fulk Al Salamah katika bandari ya Dar es Salaam jana Tarehe 16 Oktoba 2017.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Dkt. Hussen Mwinyi akisalimiana na Balozi wa Oman hapa nchini  Mhe. Ali A. Al Mahruqi walipokutana katika hafla ya mapokezi ya meli iliyobeba ujumbe kutoka kwa mfalme wa Oman uliowasili katika Bandari ya Dar es Salaam jana Tarehe 16 Oktoba 2017.

No comments:

Post a Comment