Saturday, October 14, 2017

MWIGULU NCHEMBA ATAKA SHERIA YA UHAMIAJI IREKEBISHWE KUWABANA WAHAMIAJI HARAMU.


 Waziri wa mambo ya ndani ya nchi, Mwigulu Nchemba akizungumza na waandishi wa Habari leo Tarehe 14 Oktoba 2017, katika Gereza la Kigongoni Bagamoyo.
.........................................
Waziri wa mambo ya ndani ya nchi, Mwigulu Nchemba amesema iko haja ya kufanya marekebisho ya sheria ili kuwabana wanaoingia nchini bila ya kufuata taratibu za Tanzania.

Waziri Mwigulu Nchemba alitoa kauli hiyo wilayani Bagamoyo leo Tarehe 14 Oktoba 2017 alipofanya ziara kutembelea Gereza la Kigongoni lililopo wilayani Bagamoyo.

Kauli hiyo ya waziri wa mambo ya ndani ya nchi imekuja kufuatia taarifa iliyotolewa na Mkuu wa magereza Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, SACP Boyd Mwambingu ambae alisema mkoa Pwani wafungwa ambao ni raia wa Ethiopia waliofungwa katika Magereza ya Mkoa huo ni 334, Mahabusu 12 na wanaosubiri kusafirishwa ni 91 ambao jumla ya raia kutoka Etheopia ni 437 wa Malawi ni 1 Msomali ni 1 wa DRC ni 1 wa Burundi 2 na kenya ni 2 ambapo jumla ya wafungwa wote raia wa kigeni waliopo ndani magereza ya mkoa wa pwani ni 339 na kufanya asilimia 40 ya wafungwa wote waliopo Mkoa wa Pwani ni raia wa kigeni.

Nae Mkuu wa Gereza la Kigongoni Mrakibu wa Magereza, SP. Muyengi Bulilo alisema gereza la kigongoni lina raia wa Etheopia 91 ambao wamemaliza kifungo chao na wanasubiri kusafirishwa.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Pwani, Plasd J. Mazengo  alisema sheria inataka wafungwa ambao ni raia wa kigeni walioingia nchini bila ya kufuata utaratibu wanapomaliza kifungo wanapaswa kurudishwa kwa fedha za serikali.

Kufuatia hali hiyo Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi Mwigulu Nchemba alisema haiwezekani wahamiaji haramu wasafirishwe kwa gharama za serikali ambazo ni kodi za wananchi hali yakuwa tayari wameshatia hasara ya kula chakula cha serikali pindi walipotumikia kifungo.

Aidha, alisema iko haja ya kupitiwa upya kwa sheria hizo ili kuona namna ya kutoa adhabu kubwa zaidi kwa wahamiaji haramu na sio kufungwa mwezi mmoja na kisha wanarudia makosa hayo.

Aliongeza kwa kusema kuwa mwezi mmoja hautoshi kwa mtu kujutia kosa lake na badala yake atavumilia baada ya mwezi akitolewa na kurudishwa kwenye nchi yake atarudia tena kwakuwa kifungo cha mwezi mmoja hakijamuathiri.

Wakati huohuo waziri Mwigulu alisema wale wote watakaobainika kuwasafirisha wahamiaji haramu sheria kali zitachukuliwa dhidi yao ikiwa ni pamoja na kutaifisha magari yao. 
  Waziri wa mambo ya ndani ya nchi, Mwigulu Nchemba akisikiliza ripoti ya kutoka kwa mkuu wa Gereza la Kigongoni,Mrakibu wa Magereza, SP. Muyengi Bulilo

Waziri wa mambo ya ndani ya nchi, Mwigulu Nchemba akizungumza na maafisa wa magereza, Uhamiaji na Polisi katika Gereza la Kigongoni Bagamoyo, leo Tarehe 14 Oktoba 2017, alipotembelea Gereza hilo ili kujua changamoto zinazowakabili.

Waziri wa mambo ya ndani ya nchi, Mwigulu Nchemba akizungumza na maafisa wa magereza, Uhamiaji na Polisi katika Gereza la Kigongoni Bagamoyo, leo Tarehe 14 Oktoba 2017, alipotembelea Gereza hilo ili kujua changamoto zinazowakabili.

No comments:

Post a Comment