Saturday, October 21, 2017

BAGAMOYO YATUMIKA KUSAFIRISHIA WAHAMIAJI HARAMU.



Kamanda wa Polisi Mkoani Pwani (ACP)Jonathan Shanna akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu kukamatwa kwa watanzania wawili waliokuwa wakisafirisha wahamiaji haramu 21 .(picha na Mwamvua Mwinyi)
............................................


Na Mwamvua Mwinyi-Bagamoyo

JESHI la polisi mkoani Pwani ,linawashikilia wahamiaji haramu 21 ,raia wa Ethiopia kwa kosa la kuingia nchini bila kibali ikiwa ni kinyume na sheria .

Aidha limewakamata watanzania wawili waliokuwa wakiwasaidia kuingia nchini wahamiaji hao ambapo pia inausaka mtandao unaojihusisha na biashara hiyo.

Akielezea kuhusiana tukio hilo ,kamanda wa polisi Mkoani Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Jonathan Shanna alisema ,octoba 20 usiku  , eneo la Ruvu darajani wilaya ya kipolisi Mlandizi askari wakiwa doria waliwakamata Yabata Shaban (30) mkazi wa Bagamoyo na Mohammed Ayub (20) mkazi wa Bunju wakiwasafirisha wahamiaji hao.

Alisema watuhumiwa walikuwa wakiwasafirisha raia hao kwa kutumia usafiri wa gari aina ya Noah yenye namba za usajili T.209 DEW .
“Walikuwa wakitokea Ethiopia kwenda Afrika ya Kusini ,” Waliingia nchini kwa usafiri wa majahazi wilayani Bagamoyo .

Kamanda Shanna alielezea ,Bagamoyo ndio lango kuu lina bandari bubu kama 17 ,ambazo baadhi ya watanzania wanazitumia vibaya kupitisha magendo na kufanya biashara ya kusafirisha wahamiaji haramu .

Alibainisha kwamba ,watataifisha mali zote za watu wanaojihusisha na biashara ya usafirishaji wa wahamiaji haramu.

Kamanda Shanna aliwatahadhalisha ,wale wanaotoa vyombo vyao vya majini na nchi kavu kusafirisha wahamiaji wanaoingia nchini pasipo kufuata  sheria za nchi kwani navyo vitataifishwa .

Alisema Jeshi la polisi mkoani humo, linaendelea na mahojiano na watuhumiwa wote ili kubaini mtandao wao na wale wanaowasaidia kuingia nchini .

Kamanda huyo ,alisema kuwa wahamiaji hao watafikishwa idara ya uhamiaji kwa hatua nyingine za kisheria ikiwemo kufikishwa mahakamani .

Ni siku chache zimepita waziri wa mambo ya ndani Mwigulu Nchemba alipotembelea magereza ya Kigongoni -Bagamoyo,mkoani hapo na kukutana na wimbi la wahamiaji haramu gerezani ambao wengi wao wanasubiria kumaliza kifungo chao na kupelekwa makwao kwa gharama za serikali .

Kutokana na hilo alisema hakuna sababu ya serikali kuendelea kutumia mamilioni ya fedha za walipa kodi kuwahudumia wahamiaji haramu wanaoingia kiholela bila kufuata taratibu .

Nchemba alieleza, badala yake wajihudumie ama wahudumiwe na nchi zao ili kuliondolea mzigo Taifa.


No comments:

Post a Comment