Saturday, October 28, 2017

WAWILI WAFARIKI KWA MAJI PWANI.

IMG-20171027-WA0061
Hali ya maeneo yakiwa yamejaa maji kutokana na mvua kubwa iliyonyesha Mkoani Pwani na kuleta madhara makubwa ya vifo viwili na magari na wananchi kushindwa kupita katika baadhi ya barabara ,mito na madaraja.(picha na Mwamvua Mwinyi)
…………………………………………………………………..
Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
Miili ya watu wawili imeopolewa baada ya kuzama maji katika mvua kubwa iliyonyesha Oct 26/27 mwaka huu, Mkoani Pwani .

Kaimu kamanda wa polisi mkoani Pwani ,Blasilus Chatanda ,akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na matukio hayo alisema ,Oct 27majira ya saa 2.30 asubuhi huko Mheza kata ya Pangani wilayani Kibaha, Saimon Ramadhani umri kati ya miaka 25-30 alifariki dunia baada ya kusombwa na maji.

Alisema Saimon alikuwa akijaribu kuvuka kwenye mto Mpiji uliokuwa umejaa maji kufuatia mvua hiyo .

Katika tukio jingine ,Chatanda alielezea ,majira ya saa 5 asubuhi ,mwili wa mtu aliyetambulika kwa majina ya Issa Ally (mgambo),umeokotwa huko mto Kiluvya .

Marehemu anadaiwa kuzama maji wakati akijaribu kumuokoa mtoto aliyetaka kusombwa na maji na hakuweza kuonekana hadi maji yalipopungua na kukutwa amekufa umbali wa km nne toka eneo alilozama maji .

Chatanda alisema,miili ya marehemu wote imehifadhiwa katika hospitali ya rufaa ya Tumbi na itakabidhiwa kwa ndugu baada ya kufanyiwa uchunguzi wa daktari .

“Watu tuwe na tahadhari katika wakati huu wa mvua ,tusiamini maeneo yenye maji mengi ” alisema Chatanda .

Jeshi la Polisi Mkoani Pwani ,limetoa rai kwa wananchi kuchukua tahadhari wakati wa kuvuka mito na maeneo yenye maji mengi ,katika kipindi hiki cha mvua ili kuepusha madhara yasiyo ya lazima .

No comments:

Post a Comment