Tuesday, October 31, 2017

MADIWANI KISARAWE WAMFUKUZA KAZI MGANGA MFAWIDHI WA ZAHANATI

BAADHI ya madiwani wa wilaya ya Kisarawe Mkoani Pwani ,wakionekana kusikiliza jambo  wakati wa baraza la madiwani lililofanyika mjini hapo .
Picha na Mwamvua Mwinyi

......................................
 
Na Mwamvua Mwinyi, Kisarawe
BARAZA la madiwani la halmashauri ya wilaya ya Kisarawe mkoa wa Pwani, imeazimia kumfukuza kazi mganga mfawidhi wa zahanati ya Mtakayo wilayani humo Dkt. Emmanuel Benedict.

Benedict amefukuzwa katika nafasi hiyo kutokana na kutowajibika ipasavyo,utoro na kufunga zahanati kwa siku tisa hali iliyokwamisha utoaji huduma ndani ya siku hizo .

Mwenyekiti wa halmashauri ya Kisarawe Hamisi Dikupatile akizungumza baada ya kumalizika kwa baraza la madiwani alieleza wamechukua hatua hiyo kufuatia mtumishi huyo kufanya uzembe.

Alisema maamuzi hayo yamefanyika kwa mujibu wa kanuni za utumishi ya mwaka 2003 jedwali A ,kifungu namba 42 ambapo kuna mapendekezo ya adhabu ikiwemo kushushwa cheo,kupunguziwa mshahara au kufukuzwa kazi .

Dikupatile alibainisha kwamba ,Benedict hajaitendea haki jamii ambayo ilikuwa ikihitaji huduma za afya ,hali iliyosababisha mgogoro kati ya wananchi na eneo analotolea huduma.

Alifafanua ,kutokana na hayo ndipo wakaadhimia kumfukuza kazi ili kurudisha nidhamu kazini .

“Kama Rais Dkt. John Magufuli anavyotaka kuona uwajibikaji kazini na kuhudumia wananchi na kama mtumishi awezi anatakiwa kupisha nafasi yake ama kuwajibishwa nasi tumemua kumuachisha kazi mara moja kwa kitendo chake cha kutokaa katika eneo la kazi”alieleza Dikupatile.

Hata hivyo alielezea kwasasa wanawachukulia hatua mbalimbali watumishi wenye makosa ya kiutumishi ambao wapo waliowapunguzia mishahara .

Alisema hatua wanazozichukua zinarejesha heshima kazini na kuleta tija kwa wananchi .

Dikupatile alisema baraza hilo pia limeadhimia kuwa kabla ya mwaka wa fedha 2018/2019 wakazi wa Kibong’wa wanaodai fidia yao inayofikia mil.246 ,wawe wamelipwa fidia hiyo .


No comments:

Post a Comment