Mwakilishi wa kampuni ya Yapi Merkezi ya nchini Uturuki ,inayojenga mradi
wa reli ya Standard Gauge kutoka Dar es Salaam- Morogoro,Mhandisi Mert Oz
,(aliyesimama katikatika )akimuonyesha maelezo yaliyomo kwenye karatasi,mkuu wa
mkoa wa Pwani ,Mhandisi Evarist Ndikilo(wa kwanza kushoto) wakati alipokwenda
kutembelea mradi huo huko Soga wilaya ya Kibaha.
Picha na Mwamvua Mwinyi
......................
Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
MKUU wa Mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo amewasimamisha kazi watumishi
wawili wa kampuni ya ujenzi ya Yapi Merkezi ya nchini Uturuki inayojenga reli
ya Standard Gauge kutoka Dar es Salaam- Morogoro kwa tuhuma za rushwa ya ajira.
Aidha ameagiza watumishi hao wasimamishwe kupisha uchunguzi huku akitoa
siku saba kwa vyombo vya dola kufuatilia suala hilo.
Mkuu huyo wa mkoa ,aliyasema hayo wakati alipotembelea ujenzi wa mradi
huo kwenye kijiji cha Soga wilayani Kibaha .
Mhandisi Ndikilo,alieleza kuwa endapo ikibainika wamehusika na vitendo
hivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Aliwataja watumishi hao ambao walikuwa wakilalamikiwa na wananchi
waliokuwa wakienda kuomba kazi kuwa walikuwa wakiomba rushwa ni pamoja na
Nelson ambae ametambulika kwa jina moja ofisa mwajiri (HR) kwenye kampuni hiyo
.
Mwingine ni Torong’ong’o ambaye ni dereva wa moja ya viongozi wa kampuni
hiyo ambao hawakuhudhuria hata kwenye mkutano huo.
Awali mhandisi Ndikilo alipokelewa kwa mabango na watu waliokuwa nje ya
kampuni hiyo wakilalamika kunyimwa ajira upande wa madereva na waendeshaji wa
mitambo wakidai kuwa ajira zinatolewa kwa njia ya rushwa.
“Tunanyimwa ajira hasa tunaotoka maeneo ya Kibaha na mkoa wa Pwani kwa
ujumla na wanaoajiriwa ni watu wa nje ya mkoa”walisema.
Mhandisi Ndikilo,alielezea kwamba alikuwa pia akipelekewa malalamiko
ofisini kwake ambapo baadhi ya madereva waliandika majina yao na kuambatanisha
vyeti vyao na uzoefu wao wa kazi lakini hawakupata ajira.
“Malalamiko yamekuwa ni mengi sana na wanaolalamika wanasema wamenyimwa
ajira wengi ni wa hapa Kibaha na mkoa wa Pwani ambao walipaswa kunufaika na
mradi huu kwani kila eneo lenye mradi lazima wahusika wa eneo wapewe kipaumbele
“
“Inadaiwa walioajiriwa hata 100 hawafiki katia ya 390 ya walioajiriwa,”
alisema Ndikilo.
“Tumeambiwa kuna baadhi wanaajiriwa kusikojulikana wakija hapa
wanaingizwa moja kwa moja na kati ya wafanyakazi 390 wengi wanatoka nje ya mkoa
huku wa hapa wakiambulia kula vumbi tu wakishinda hapa nje bila ya mafanikio,”
alisema mhandisi Ndikilo.
Akizungumzia suala hilo Diwani wa Kata ya Soga Ramadhan Chezeni alisema
taarifa kuwa wapo watu wameajiriwa kwa kufuata sifa si la kweli.
Alieleza kuna vijana wengi wanasifa zinazostahili lakini wanasumbuliwa
bila ya kupata ajira.
Kwa upande wake Meneja mradi huo uliochini ya Reli Assets
Holding Company (RAHCO) ,mhandisi Maizo Mgedzi alisema suala la rushwa
halifahamu .
Alisema anachojua wanaoajiriwa wote ni wenye sifa na vigezo ,na wanatoka
nchini bila ya kujali eneo analotoka.
Mgedzi alisema kuwa watahakikisha wanalifuatilia suala hilo ili kupisha
uchunguzi lengo likiwa ni kuhakikisha hakuna malalamiko kwa wananchi
wanaozunguka eneo la mradi huo.
Naye mwakilishi wa kampuni ya Yapi Merkezi Mhandisi Mert Oz
alisema,endapo watabaini wapo walioingizwa kwenye ajira kinyume cha
utaratibu,hawatasita kuwaondoa.
Oz alisema , wanafuata taratibu za ajira na wanategemea kuletewa
wafanyakazi kwa utaratibu wa nchi na kufuata sheria za ajira.
MKUU
wa Mkoa wa Pwani ,Mhandisi Evarist Ndikilo akipokelewa kwa mabango na
baadhi ya watu ,wakati alipokwenda mradi wa reli ya Standard Gauge kutoka
Dar es Salaam- Morogoro inayojengwa na kampuni ya ujenzi ya Yapi Merkezi
ya nchini Uturuki ,huko Soga wilayani Kibaha.
No comments:
Post a Comment