Katibu
Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Dkt.Adelhelm Meru akiongea wakati
wa hafla ya uwekaji jiwe la msingi katika kiwanda cha kutengeneza vifungashio
cha Global Packaging Limited kilichopo Wilayani Kibaha Mkoani Pwani ambapo
alimpongeza muwekezaji wa kiwanda hicho na kutoa rai kwa wakuu wa wilaya na
mikoa nchini kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya wawekezaji ikiwemo kutenga
maeneo maalum kwa ajili ya viwanda kama ilivyo katika mkoa wa Pwani.
..........................................................
Wakuu wa Mikoa na Wilaya nchini wametakiwa kuweka kuweka mazingira
wezeshi kwa wawekezaji nchini ikiwemo kutenga maeneo maalum kwa ajili ya ujenzi
wa viwanda nchini.
Akizungumza wakati wa uwekaji jiwe la msingi katika kiwanda cha
kutengeneza vifungashio kilichopo wilayani Kibaha mkoani Pwani Katibu Mkuu
Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Dkt. Adelhelm Meru amesema kuwa tukiwa
tunaelekea katika nchi ya viwanda serikali inajukumu la kutoa ushirikiano wa
kutosha kwa wawekezaji nchini.
Dkt. Adelhelm amesema kuwa viongozi hao hawana budi kuiga mfano wa Mkuu
wa Mkoa wa Pwani na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha kwa ushirikiano wanaoutoa kwa
wawekezaji ikiwemo kutenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa viwanda katika mkoa
huo.
“Dhumuni la serikali kwa sasa ni kuhakikisha tunaifikia nchi ya uchumi wa
kati kupitia viwanda,na hili tutalitekeleza pia kwa kushirikiana na sekta
binafsi na ni jukumu la viongozi ikiwemo wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa
nchini kote kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wawekezaji ikiwemo kutenga maeneo
kwa ajili ya ujenzi wa viwanda”. Alisema Dkt. Adelhelm
Dkt. Adelhelm aliongeza kuwa mpaka ifikapo mwaka 2020 Serikali imepanga
kuhakikisha sekta ya viwanda nchini inachangia asilimia 15 kwenye pato la taifa
kutoka asilimia 7.3 iliyopo hivi sasa.
Pia Dkt. Adelhelm alisema kuwa Serikali imepanga kuongeza idadi ya ajira
za viwandani na ajira zitokanazo na sekta ya viwanda hadi kufikia asilimia 40
ifikapo mwaka 2020.
Naye Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Taifa(NDC) Bw. Mlingi
Mkucha amesema kuwa shirika hilo litaendelea kutoa ushirikiano kwa wawekezaji
wote wenye nia ya kuwekeza katika viwanda ikiwemo kupitia maandiko ya miradi
yao na kuwasimamia ili kuhakikisha kwa pamoja wanatimiza lengo la serikali ya
awamu ya tano ya kufikia uchumi wa kati kupitia viwanda.
Bw. Mkucha aliongeza kuwa katika wilaya ya Kibaha kuna hekari 330
zilizotengwa kwa ajili ya viwanda vya aina mbalimbali ikiwamo viwanda vya
kuunganisha magari, vuwanda vya madawa na viwanda vya nguo hivyo kama kuna
muwekezaji mwenye nia ya kuwekeza katika sekta hizo aende katika ofisi za
Shirika hilo ili kuweza kujadili namna ya kutekeleza suala hilo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Bi. Asumpta Mshana alisema kuwa ujenzi wa
kiwanda hicho katika mkoa wa pwani ni mwendelezo wa jitihada za kumuunga mkono
Rais Magufuli ya kufikia uchumi wa kati kupitia viwanda.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mwendeshaji wa Kiwanda cha kutengeneza
vifungashio cha Global Packaging Bw. Joseph Wasonga alishukuru jitihada za
serikali na taasisi zake kwa ushirikiano wanaoupata tangu wakiwa na wazo la
kuanzisha kiwanda hicho hadi kufikia hatua hiyo ya uzinduzi.
Bw. Wasonga aliongeza kuwa dhumuni la kiwanda hicho ni kuzalisha
vifungashio milioni 16 hadi milioni 20 kwa mwaka na kuongeza zaidi idadi ya
ajira kwa wakazi wa maeneo yanayozunguka kiwanda hicho na maeneo ya jirani.
Kiwanda cha hicho kinamilikiwa kwa ubia kati ya Shirika la Maendeleo la
Taifa(NDC) na kampuni ya Wande Printing and Packaging inayomilikiwa na mzawa.
Mkuu
wa Wilaya ya Kibaha Bi. Asumpta Mshana akiongea wakati wa hafla ya uwekaji jiwe
la msingi katika kiwanda cha kutengeneza vifungashio cha Global Packaging
Limited kilichopo Wilayani Kibaha Mkoani Pwani na kumshukuru muwekezaji wa
kiwanda hicho kwa kuamua kuwekeza katika mkoa wa pwani kwani itaisaidia kuongeza
mapato katika mkoa na kuongeza ajira kwa wakazi.
Katibu
Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Dkt.Adelhelm Meru (katikati
mwenye miwani), Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) Mlingi
Mkucha (mwenye tai nyekundu), Mkurugenzi Muendeshaji wa Kiwanda cha vifungashio
Bw. Joseph Wasonga (wanne kutoka kulia) na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Bi. Asumpta
Mshana wakiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Kiwanda hicho na
wafanyakazi wa NDC.
No comments:
Post a Comment