Tuesday, November 29, 2016

HALMASHAURI ZAONGOZA KWA RUSHWA ZIKIFUATIWA NA POLISI.

mlowolapicha
 Halmashauri nyingi hapa nchini zinaongoza kwa kupokea rushwa kubwa kubwa huku jeshi la polisi likiongoza kwa kupokea rushwa ndogo ndogo suala ambalo limepelekea mapambano dhidi ya rushwa kuwa magumu.

Hayo yameelezwa jana na Mkurugenzi wa Takukuru Valentino Mlowola wakati wa mkutano wa mkuu mwaka wa siku 2 wa Shirikisho la mamlaka za kuzuia na kupambana na rushwa nchi za Afrika Mashariki(EAAACA) unaofanyika jijini Arusha ambapo unawashiriki kutoka mataifa 8 barani Afrika.

Mlowola alisema kuwa Hadi sasa katika kipindi cha mwaka mmoja wa wameweza kuokoa zaidi ya billion 45 za miradi mbalimbali zilizokuwa ziangukie mikononi mwa watu wachache ambapo aliitaka jamii kutoa ushirikiano dhidi ya mapambano ya kuzuia rushwa.

Alisema kuwa miradi mingi inayopitia katika halmashauri nyingi hapa nchini imekuwa ikigubikwa na rushwa na kuifanya miradi hiyo kujengwa chini ya viwango hali inayopelekea matumizi mabaya ya fedha za umma.

Aidha katika jeshi la Polisi alitanabaisha kuwa kumekuwa na ongezeko la kuomba na kupokea rushwa ndogo kutoka kwa jamii hali inayosababisha wananchi kukosa imani na kupelekea malalamiko kwa jeshi hilo.

“Waandishi wa habari iwapo mtaona mradi wowote hauendi kwa viwango vilivyokusudiwa mtoe taarifa kwani hivi sasa tuna maofisa wetu katika kila wilaya ambao wataweza kufanya uchunguzi na kubaini mianya ya rushwa”alisema Mlowola.

Kwa upande wake waziri wa nchi ofisi ya Raisi Utumishi na Utawala Bora  Angela Kairuki alisema kuwa serikali imeanzisha mahakama ya mafisadi ambapo kesi kadhaa zimeanza kusikilizwa hali itakayopelekeakupunguza kuomba na kupokea rushwa hapa nchini.

Alisema kuwa kesi nyingi zimepelekwa katika mahakama hiyo na siku si nyingi mafanikio ya vita dhidi ya ubadhirifu wa mali za umma utapungua kama sio kwisha kabisa

Waziri huyo alitoa wito kwa taasisi mbalimbali za serikali kushirikiana na sekta binafsi katika kuhakikisha mapambano dhidi ya rushwa katika nchi za ukanda wa afrika mashariki zinakoma.

No comments:

Post a Comment