WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameliegiza Baraza la Madiwani la Halmashauri
ya Wilaya ya Kibaha lifanye maamuzi ya kupima ardhi haraka na kutenga maeneo
kwa ajili makazi na viwanda ili kujiandaa na uwekezaji mkubwa.
Ametoa agizo hilo jana mchana (Jumamosi, Novemba 19, 2016) wakati
akizungumza na wananchi na viongozi mbalimbali wa Serikali na wa Mkoa wa Pwani
mara baada ya kukagua kiwanda cha kutengeneza magari ya zimamoto na matrekta
cha Equator SUMA JKT Limited kilichopo Ruvu JKT, wilayani Kibaha mkoani Pwani.
“Jiji la Dar es Salaam limejaa,
na Kibaha mjini pia hawana ardhi ya kutosha kwa kimbilio pekee hivi sasa ni
Kibaha Vijijini. Baraza la Madiwani fanyeni maamuzi, pimeni ardhi na mtenge
maeneo ya makazi, viwanda na taasisi za elimu ili mkipata wawekezaji iwe rahisi
kuwapa maeneo,” amesema.
Waziri Mkuu amesema ujenzi wa kiwanda hicho utakuwa mkombozi kwa taasisi
nyingi na halmashauri nyingi nchini kwani zilikuwa zinashindwa kumudu bei ya
kununua magari ya zimamoto. “Baadhi ya Halmashauri nyingi zilikuwa zinanunua
gari moja kwa sh. milioni 500 na hiki ni kiasi kikubwa mno… kwa hiyo kiwanda
hiki kitakuwa mkombozi kwa taasisi nyingi na halmashauri zetu,” amesema.
Amesema maeneo mengi nchini yanahitaji magari ya zimamoto lakini yalikuwa
yanashndwa kumudu bei za magari hayo.
Aliyataja maeneo hayo kuwa ni viwanja vya
ndege, bandari, taasisi zilizo chini ya TAMISEMI kama vile shule za sekondari
za bweni, Majiji, miji mikuu, Manispaa na Halmashauri za Wilaya.
Amesema ameguswa kukuta kiwanda hicho pia kina uwezo wa kutengeneza
matreka na zana za kilimo (farm implements) kwani asilimia kubwa ya Watanzania
ni wakulima na wanategemea jembe la mkono. “Kupitia kiwanda hiki, matrekta
mengi yataunganishwa na nina imani bei itakuwa ya chini ili wananchi waweze kumudu.”
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Equator SUMA JKT Ltd, Eng. Robert Mangazini
alimweleza Waziri Mkuu kwamba asilimia 80 ya ujenzi wa kiwanda hicho
imekamilika na kwamba hivi sasa wako kwenhye hatua ya kufunga mitambo. Hata
hivyo, alisema wanaisubiri iwasili kutoka India.
Alisema kiwanda hicho kikikamilika kitaweza kuunganisha matrekta 3,000
kwa mwaka na magari ya zimamoto 100 na kubainisha kuwa faida za kuunganisha
magari hayo hapa nchini ni kuwa na uwezo wa kuzalisha vipuri ndani ya nchi.
“Tukiweza kuzalisha vipuri hapa nchini kwa asilimia 60, umiliki wa magari
haya na matrekta utakuwa ni wa Tanzania na siyo wa kampuni za nje tena. Pia
tutakuwa tumefaulu kuhamisha teknolojia kwa vijana wetu,” alisema.
Alisema hadi sasa vijana 60 wamekwishapatiwa mafunzo ona wako tayari
kuanza kazi mara uzalishaji utakapoanza Machi, 2017.
Kuhusu teknolojia ya utengenezaji wa magari ya zimamoto, Eng. Mangazini
alisema kiwanda hicho ni cha pili kujengwa barani Afrika cha kwanza kikiwa huko
Bassa, Afrika Kusini.
Mapema, akisoma risala mbele ya Waziri Mkuu, mwakilishi wa Equator SUMA
JKT Ltd. Kapteni Farijala Mkojera alisema kiwanda hicho kinamilikiwa kwa pamoja
na kampuni ya Equator Automech Ltd ambao wana hisa asimilia 70 na SUMA JKT
inamiliki asilimia 30 ya hisa za kiwanda hicho.
Akizungumzia ujenzi wa kiwanda hicho, alisema hadi sasa wamekwishatumia
sh. bilioni 1.5 na kwamba hadi ujenzi utakapokamilika, wanatajia kuwa wametumia
sh. bilioni mbili. “Ujenzi ukikamilika, tunatarajia kuajiri wafanyakazi 200
katika fani mbalimbali,” alisema.
Alisema wakianza uzalishaji, mbali ya magari ya zimamoto na matrekta,
wataweza pia kuunganisha mabasi na zana za kilimo kama vile combine harvesters.
“Tutakuwa tumefanikiwa kuhamisha teknolojia kutoka Russia (magari za zimamoto)
na India na Poland (matrekta). Tuna uhakika wa soko hapa nchini katika Jumuiaya
za EAC na SADC,” alisema.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, NOVEMBA 19, 2016.
No comments:
Post a Comment