Sunday, November 20, 2016

WALIOUNDA GROUP FACEBOOK KUTAFUTA MASHAMBA WATAPELIWA ZAIDI YA MILIONI 300 BAGAMOYO.

Watu  400 ambao walikutana kwenye ukurasa wa Facebook mwaka 2014 kwa lengo  la kutafuta  mashamba, wametapeliwa zaidi ya shilingi milioni 300 katika kijiji cha Kidomole kata ya Fukayosi wilayani  Bagamoyo baada ya  kuuziwa  eneo linalomilikiwa na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) lililopo wilayani Bagamoyo  ambalo hujulikana kama Ranchi ya Ruvu.

Utapeli huo umebainika baada ya mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga kuunda tume ya kuchunguza migogoro mbalimbali iliyojitokeza  katika kijiji cha Kidomole hali iliyopelekea  serikali ya kijiji  kusimamishwa  ili kupisha uchunguzi.

Awali serikali ya kijiji imekuwa ikituhumiwa kwa matumizi mabaya  ya madaraka kwa kusimamia mauzo katika hifadhi za  serikali pamoja na ubadhilifu wa fedha na kusababisha kuzorota kwa shughuli mbalimbali za maendeleo katika kijiji hicho.

Akielezea hali hiyo mbele ya mkuu wa wilayaya Bagamoyo, kiongozi wa wanunuzi hao wapatao mia nne, Jackline Mushi alisema mnamo mwaka 2014 mwezi wa sita walitengeneza kikundi kupitia ukurasa wa Facebook kwa  lengo la kutafuta mashamba ambapo walifikia idadi ya watu mia nne.

Alisema mara baada ya  kusikia Bagamoyo kuna maeneo yanauzwa kijiji cha Kidomole  walifika kijijjini hapo ambapo walipewa namba zinazoonyesha kuwa eneo hilo limepimwa na kwamba wauzaji ndio wamiliki halali.

Aliongeza kuwa baada ya kupata  namba zinazoonyesha shamba hilo  limepimwa walifika ofisi za Ardhi Bagamoyo ili kujiridhisha  ambapo ofisi ya Ardhi Bagamoyo ilisema eneo hilo lipo katika mpango wa matumizi bora ya Ardhi, na limetengwa kwaajili ya  makazi na  kilimo.

Jackline, aliendelea kueleza kuwa  mara baada ya kutoka ofisiya Ardhi walirudi kijijini ambapo walionyeshwa kitabu cha mpango wa matumizi bora ya Ardhi ambacho kinafanana na kile  walichoonyeshwa ofisi ya  Ardhi.

Alisema mara baada ya kujiridhisha waliomba kuelekezwa taratibu za manunuzi ili waweze kufanya malipo ambapo katika kikundi cha watu miane kila mmoja  alinunua kulingana na uwezo wake ambapo Jackline alinunua heka 50, wengine ni heka 30 kila mmoja na zaidi ya watu miambili walinunua heka mojamoja.

Mara baada ya kuuziwa maeneo hayo ambapo kila  heka  waliuziwa  shilingi  laki tatu, 300,000 na kufanikiwa kuuziwa  heka  elfu moja  na  hamsini  1,050 sawa na shilingi milioni mia tatu na kumi na tani, 315,000,000/=  walitakiwa kulipa asilimia kumi ya kijiji  ili wajadiliwe kwenye mkutano mkuu wa kijiji na kupitishwa.

Katika mauzo hayo ambayo yameidhinishwa na mwenyekiti wa kitongoji cha Kinyemvuu Mrisho Saidi, wauzaji walikuwa 27 ambao wao waliodai kuwa ni wamiliki wa eneo hilo ambao waliongozwa na Salum Kagunia na Selemani Mkwamba.

Hata hivyo Jacqueline amekiri kuwa, mara baada ya kununua eneo hillo mwezi wa  sita 2014  ilipofika mwezi wa 11 mwaka 2014 alifika aliyekuwa  mkuu wa mkoa wa  Pwani wakati huo Hajat Mwantumu Mahiza, na kuwaambia kuwa eneo hilo ni mali NARCO na kwamba  wao wametapeliwa.  

Taarifa ya uchunguzi kutoka ofisi ya mkaguzi Halmashauri ya Bagamoyo, iliyosomwa mbele ya mkuu wa wilaya imewataja  aliyekuwa mwenyikti wa kitongoji cha Usigwa Elizabeth Nazari na aliyekuwa mtendaji wa  kijiji cha Kidomole Seifu Mohamedi mayala kuhusika katika kujipatia fedha za asilimia 10 ambazoni miloni thelasini na  moja na  laki tano,  31,500,000 kinyume cha  utaratibu baada ya kubainika  asilimia kumi ya mauzo ya  shamba  hayakuingizwa  kwenye akaunti yakijiji kama walivyodai  hali inayoashiria kuwa kulikuwa na njama za kuwatapeli wanunuzi hao.

Kufuatia Taarifa ya wakaguzi kutoka Halmashauri ya Bagamoyo, mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga aliamuru waliohusika na mauzo hayo ya eneo la NARCO  wakamatwe na kwamba  wale wote walionunua waende mahakamani kudai haki zao.

Aidha, mkuu wa wilaya ya  Bagamoyo amewataka wanachi wanaotaka kununua Ardhi katika wilaya ya Bagamoyo kufuata  taratibu  za  kisheria  ikiwa ni  pamoja na kufika ofisi za Ardhi kwaajili ya kupata ushauri wa kitaalamu kabla ya kufanya  manunuzi.

Wanaoshikiliwa na  polisi ni Selemani Mkwamba  na Salum Kagunia  ambao ni viongozi wawauzaji Mrisho Saidi mwenyekiti wa kitongoji cha Kinyemvuu, huku Elizabeth Nazari akiendelea kutafutwa ili kutoa maelezo ya namna walivyopokea milioni  31,500,000  kama asilimia kumi ya mauzo.

No comments:

Post a Comment