Wednesday, November 9, 2016

HOSPITALI YA TUMBI YAANZA KUZALISHA DRIP YENYEWE NA KUONDOA ADHA YA KUNUNUA SEHEMU NYINGINE.

tum
KAIMU mganga mkuu wa hospitali ya rufaa ya Tumbi ,mkoani Pwani, Dkt. Bryceson Kiwelu,akionyesha chupa ya drip ambazo wanazalisha katika kitengo cha hospitali  hiyo ambapo kwasasa wanaondokana na adha ya kununua drip nje ya hospital kwa asilimia 98 sasa.(Picha zote na Mwamvua Mwinyi)
 tubi

Na Mwamvua Mwinyi-Kibaha

HOSPITALI ya rufaa ya Tumbi mkoani Pwani,imeanza kuzalisha drip zake kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa hali inayosababisha kuondokana na adha ya kununua drip nje ya hospitali hiyo kwa asilimia 98.

Aidha hospitali hiyo bado inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa kipimo cha CT Scan na kupelekea wagonjwa wanaotakiwa kufanyiwa kipimo hicho kwenda hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Akizungumza kuhusiana na mafanikio na changamoto zinazozikabili hospitali hiyo ,kaimu mganga mkuu wa hospitali ya rufaa ya Tumbi,Bryceson Kiwelu,alisema kwasasa Tumbi ina kitengo cha kuzalisha drip yenyewe.

Alieleza kwamba drip hizo wanatengeneza katika ujazo wa mill’s 250 hadi 500 lakini wanatarajia kuzalisha katika ubora wa chupa za vioo ili waweze kuuza katika hospitali na vituo vya afya vingine kwa lengo la kujipatia kipato.

“Kuna wauguzi zaidi ya watatu ambao wana vyeti vinavyoruhusiwa kutengeneza drip hizo,ndio wataalamu kwenye kitengo hiki lakini lengo letu ni kupeleka wengine wawili masomoni ili wasomee utaalamu huu”alifafanua Dkt. Kiwelu.

Mafanikio mengine ni pamoja na hospitali kupata mtambo wa hewa ya oxygen,uliogharimu sh.mil.184 ambao unasaidia kuhudumia wagonjwa 75 kwa wakati mmoja ikiwemo wa ajali za barabarani.

Dk.Kiwelu alisema ipo changamoto ya kipimo cha CT Scan, endapo kingekuwepo kingesaidia kwa kiasi kikubwa hasa wahanga wa ajali za barabarani kwani Tumbi huhudumia wagonjwa hao kwa asilimia 8 ambao wengi wao huumia vichwa.

Nae mkurugenzi wa shirika la elimu Kibaha, Dk. Cyprian Mpemba alisema mafanikio hayo, yametokana na ubunifu wao kwa kuandika maandiko kwa wafadhili na ushirikiano.

Alisema pia wameweka mtambo mpya wa kisasa wa kufulia nguo za wagonjwa uliogharimu mil .119.

“Mtambo huo wa kufulia nguo unasaidia hospitali nyingine ikiwemo Bagamoyo na vituo vya afya kupeleka mashuka kufuliwa”alisema dk. Mpemba.

Dk.Mpemba alifafanua kwamba pia kumejengwa na maabara katika shule ya sekondari ya wasichana ambapo imeshakamilika kwa asilimia 75.

Alieleza licha ya hayo yote bado wanakabiliwa na ufinyu wa bajeti.

Dk.Mpemba alisema bajeti iliyoidhinishwa 2016/2017 katika 
mishahara,matumizi na miradi ya maendeleo ni zaidi ya sh.bil 19.324 ambapo mapato halisi ya Julai/Septemba 2016 ni sh.bil 3.210 pekee sawa na asilimia 16.6.


No comments:

Post a Comment