- Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage akizungumza na wahitimu 1,811 wa Chuo cha Elimu ya Biashara
(CBE) waliotunukiwa stahili zao katika Fani mbalimbali kwa mwaka 2016 wakati wa Mahafali ya 51 ya chuo jijini Dar es salaam...........................
amewataka wahitimu 1,811 wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE)
waliotunukiwa stahili zao katika Fani mbalimbali kwa mwaka 2016
kuchangamkia fursa za ajira zilizopo nchini kwa kuanzisha makampuni na viwanda vidogo vidogo vitakavyowawezesha kujiajiri na kuajiri wengine.
Akizungumza katika mahafali ya 51 ya chuo hicho jijini Dar es salaam
Mhe.Mwijage amesema kuwa makampuni na viwanda vidogo vidogo
watakavyoanzisha vitatumika kuzalisha bidhaa mbalimbali zenye ubora ambazo zitauzwa kote duniani hivyo kukuza uchumi wa nchi na kuwapatia ajira ya uhakika.
Amesema Serikali ya Tanzania inapenda kuwaona Wawekezaji wengi wa Kitanzania wakiingia na kuwekeza kwenye rasilimali mbalimbali
zilizopo nchini Tanzania badala ya kuwaachia wageni kwa kuwa inao
wasomi waliobobea kwenye fani ya biashara pamoja na ujasiriamali.
” Taifa letu limebarikiwa kuwa na fursa nyingi za kujiletea maendeleo,
Serikali ingependa kuona wawekezaji wengi wa Kitanzania wakiwekeza kwenye rasilimali zilizopo kwa mfano tunayo gesi, madini, kilimo na na rasilimali nyinginezo nyingi” Amesisitiza Mhe.Mwijage.
Amefafanua kuwa Serikali itaendelaea kuwekeza kwenye Elimu ya Biashara kuwawezesha wananchi wengi zaidi kujiajiri na kuajiriwa katika sekta binafsi hasa Biashara.
Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea na mikakati ya kudumisha
ushirikiano na nchi za jirani kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki
(EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kwa lengo la kuondoa kuondoa vikwazo mbalimbali vya kiuchumi, kijamii na kibiashara katika nchi zilizo katika ukanda huo ili kuwawezesha watanzania kuendelea kunufaika.
” Nawaomba sana muondoe hofu mzitumie fursa zilizoko nje ya Tanzania, msifungwe na mipaka , fuateni taratibu zilizopo ili mjinufaishe na kulinufaisha Taifa letu” Amebainisha Mhe.Mwijage.
Katika hatua nyingine amekipongeza chuo hicho na wake kwa kuendelea kupanua wigo wa utoaji wa elimu katika fani mbalimbali kwa kuongeza matawi ya chuo hicho kwenye mikoa ya Dodoma, Mwanza na Mbeya na kukiwezesha kuwa na kufikisha idadi ya wanachuo wapatao 11,000.
Aidha, amesema kuwa ili kukabiliana na ongezeko la idadi ya wanachuo wanaodahiliwa kila mwaka na changamoto ya uhaba wa majengo na kumbi za mihadhara amewataka viongozi na watendaji wa Wizara yake washirikiane na Bodi ya CBE na Menejimenti ya chuo hicho kuangalia uwezekano wa kujenga majengo makubwa na marefu katika eneo la chuo hicho ili kukidhi mahitaji ya miundombinu.
” Ili kufanikisha hili Serikali tutasaidia kutenga fedha pia kuwa na
jukumu la kutafuta wabia na Serikali tutatafuta udhamini wa ubia huo” Amesema.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Prof.Emanuel Mjema akizungumza wakati wa mahafali hayo ameeleza kuwa chuo anachokisimamia kimeweza kutoa wahitimu kwenye mafunzo ya biashara nyanja za Uhasibu, Usimamizi wa Biashara, Usimamizi wa Masoko, Ununuzi na Ugavi, Mizani na Vipimo ,TEHAMA pamoja na mafunzo ya Shahada ya Ualimu katika Biashara.
Amesema kuwa mafunzo hayo yamewanufaisha Watanzania kwa kuwawezesha ujiajiri na kuajiriwa na kuongeza kuwa chuo hicho hivi karibuni kimeanzisha Shahada mbili za Uzamili katika fani za Habari na Mawasiliano.
Prof.Mjema ameeleza kuwa chuo hicho kina wahadhiri waliobobea katika nyanja mbalimbali za mambo ya Elimu ya Biashara na wanao uwezo wa kufanya tafiti na kutoa ushauri katika nyanja ya biashara na kuiomba Serikali kuwatumia wataalam hao.
” CBE tunao wataalam waliobobea katika nyanja ya Biasahara na tuna
uwezo wa kufanya tafiti na kutoa ushauri katika shughuli mbalimbali, ni wakati muafaka Serikali itutumie hasa wakati huu tunapoelekea
kwenye ujenzi wa Tanzania ya viwanda ili tuwezesha kutoa taarifa
sahihi za Biashara na uwekezaji” Amesisitiza Prof.Mjema.
Amesisitiza kuwa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kimekuwa ni Taasisi ya kwanza ya Elimu ya juu kufanya Utafiti na kuendesha Kongamano juu ya Fursa za Kibiashara na Uwekezaji zilizopo mjini Dodoma, kongamano ambalo limesaidia kwa kiasi kikubwa kubaini fursa za Biashara na uwekezaji pamoja na namna bora na endelevu ya kuzitumia fursa hizo.
Kwa upande wao baadhi ya wahitimu wa chuo hicho waliohudhuria mahafali hayo wakizungumza kwa nyakati mbalimbali wamesema kuwa wako tayari kulitumikia taifa kwa kuwa wanao uwezo na ujuzi wa kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
Wameeleza kuwa licha ya changamoto ya uhaba wa nafasi za ajira
Serikali wako tayari kujiajiri wenyewe kwa kuanzisha makampuni yao
wenyewe yatakayowawezesha kujiajiri wenyewe na kuajiri vijana wengine kwa kuitumia elimu waliyoipata chuoni hapo.
Wahitimu wa Chuo cha Elimu ya Biashara CBE wakivaa kofia zao mara baada ya kutunukiwa Shahada zao katika fani mbalimbali wakati wa mahafali ya 51 ya Chuo cha Elimu ya Biashara jijini Dar es salaam.Baadhi ya Wahitimu wa CBE fani ya wakifurahia mara baada ya kutunukiwa Shahada zao mgeni Rasmi Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mijage.
Sunday, November 13, 2016
WAHITIMU CBE WATAKIWA KUWA WABUNIFU KWA KUANZISHA VIWANDA VIDOGO VIDOGO ILI KUJIPATIA AJIRA.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment