Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye alipokuwa akitoa hoja kabla
Kamati ya Bunge zima kujadili Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa 2016
ambao umepitishwa leo mjini Dodoma.
...............................
Mkutano wa Tano wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
umepitisha rasmi Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa mwaka 2016 ambapo
hatua inayofuata ni kuridhiwa na kusainiwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli ili
uwe Sheria kamili ya nchi.
Muswada huo umepitishwa leo Bungeni mjini Dodoma ambapo mkutano huo
uliongozwa na Mwenyekiti wa Bunge hilo, Mhe. Andrew Chenge.
Wabunge walijadili Muswada huo kifungu kwa kifungu na kuunga mkono
upitishwaji wake baada ya Waziri mwenye dhamana na habari kutoa hoja ili
Muswada huo uweze kujadiliwa.
Akiongea na waandishi wa habari mara baada ya kupitishwa Muswada huo,
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye amewashukuru
wadau wote walioshiriki katika kutoa maoni juu ya Muswada huo kwani ndiyo yamepelekea
kukamilisha mchakato mzima wa Muswada huo.
“Kwa niaba ya Serikali napenda kuwashukuru wadau wote walioshiriki kwa
namna moja au nyingine katika kuhakikisha tunatimiza malengo ya takribani miaka
20 iliyopita ya kuifanya taaluma hii ya habari kuheshimika kama zilivyo taaluma
zingine”, alisema Waziri Nape.
Waziri Nape ameongeza kuwa kwa sasa Muswada huo umeshapitishwa hivyo
kilichobaki ni utungaji wa Kanuni ambapo ameomba wadau wa tasnia ya habari
kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kutoa maoni yatakayopelekea kuwa na kanuni
zenye tija kwa wanahabari na taifa kwa ujumla.
Aidha, Mhe. Nape amewaasa wadau wa habari kuunganisha nguvu kwa pamoja
hasa katika kipindi hiki ambacho Muswada huo umepitishwa pia amewataka wadau
hao wasiruhusu mgawanyiko utokee kati yao bali washirikiane na Serikali katika
kutekeleza wajibu wao wa kihabari kwa jamii.
Kwa upande wake Mwanasheria Mkuu wa Serikali George Masaju amesema kuwa
Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa mwaka 2016 ni mwanzo mpya wa tasnia ya
habari nchini ambapo amewaasa wadau wa habari wakiwemo waandishi wa habari
kutambua kuwa haki mara zote huendana na wajibu, hivyo hakuna haki isiyo na
wajibu.
Muswada huo uliopitishwa leo umejadiliwa na Bunge hilo kwa siku mbili
ambapo kwa mara ya pili ulisomwa mbele ya Kamati ya Bunge zima na hatimaye
kusomwa kwa mara ya tatu ili kukidhi hatua za utungwaji wa Sheria nchini.
No comments:
Post a Comment