Mkurugenzi
Msaidizi Masuala Mtambuka kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,
Venance Manori akiwa katika picha ya pamoja na waandaaji wa warsha ya
kuwawezesha Maafisa Waandamizi wa Serikali kutoka nchi sita za Afrika katika
kutengeneza mipango inayozingatia usawa wa kijinsia katika elimu kutoka shirika
la Plan International- Tanzania, Global Partnership for Education (GPE), Dubai
Cares pamoja na United Nations Girls’ Education Initiative (UNGEI) mara baada
ya ufunguzi wa warsha hiyo uliofanyika jana jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi
Mkuu wa shirika la Plan International- Tanzania, Jorgen Haldorsen akitoa neno
fupi kwa ajili ya kuwakaribisha Maafisa Waandamizi wa Serikali kutoka nchi sita
za Afrika katika ufunguzi wa warsha ya kuwawezesha kutengeneza mipango
inayozingatia usawa wa kijinsia katika elimu. Ufunguzi wa warsha hiyo
ulifanyika jana jijini Dar es Salaam.
Baadhi
ya Maafisa Waandamizi wa Serikali wanaohusika na elimu kutoka nchi sita za
Afrika wakisikiliza hotuba ya Mkurugenzi Msaidizi Masuala Mtambuka kutoka
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (hayupo pichani), Venance Manori wakati
wa ufunguzi wa warsha ya kuwawezesha maafisa hao katika kutengeneza mipango
inayozingatia usawa wa kijinsia katika elimu.Warsha hiyo ya siku tatu
imefunguliwa jana jijini Dar es Salaam.
.............................
Serikali imejipanga kutengeneza mwongozo wa kuwarudisha shuleni wanafunzi
waliopata mimba wakiwa masomoni ili kuhakikisha wanapata elimu hadi kufikia
ngazi za juu.
Hayo yamesemwa jana Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Msaidizi Masuala
Mtambuka kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Venance Manori
alipokuwa akifungua warsha ya kuwawezesha Maafisa Waandamizi wa Serikali kutoka
nchi sita za Afrika katika kutengeneza mipango inayozingatia jinsia katika
elimu kwa niaba ya Waziri wa Wizara hiyo Prof. Joyce Ndalichako.
Manori amesema Serikali ya Tanzania inajitahidi kuzingatia jinsia katika
utoaji wa elimu ambapo takwimu zinaonyesha kuwa elimu ya Msingi na Sekondari
uwiano wake ni moja kwa moja japo kuwa idadi ya wasichana hupungua kutokana na
changamoto mbalimbali zinazowakumba hivyo lengo la warsha hiyo ni kuwasaidia
wadau kuweka mipango ya elimu inayozingatia usawa wa kijinsia.
“Serikali yetu imejipanga kuhakikisha wasichana wanapata elimu hadi ngazi
za juu lakini mpango huo unakumbwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za mimba
na ndoa za utotoni hivyo ili kuhakikisha mtoto wa kike anafikia ngazi za juu za
elimu tuko kwenye mchakato wa kuandaa mwongozo kwa ajili ya wanafunzi waliopata
mimba wakiwa bado wanasoma kupata nafasi ya kuendelea na masomo,”alisema
Manori.
Mkurugenzi Msaidizi amezitaja changamoto zingine zinazowapelekea
wanafunzi wa kike kuacha shule zikiwemo za umaskini, mazingira rafiki ya
kusomea, mila na desturi zinazomkataza msichana kupata nafasi ya kusoma pamoja
na kukosa muda wa kujisomea kwa sababu ya kufanya kazi nyingi wanaporudi
majumbani.
Manori ametoa rai kwa Watanzania kuelewa kuwa kila mtoto ana haki na
wajibu wa kupata elimu bila kujali jinsia pia ameiasa jamii kuacha kuwaozesha
wasichana wenye umri chini ya miaka 18 ili waweze kufikia malengo yao
waliyojipangia.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Plan International-
Tanzania, Jorgen Haldorsen ameahidi kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika
kuhakikisha mipango ya elimu nchini inaangalia usawa wa kijinsia kwa kuwa ni
njia moja wapo itakayochochea maendeleo ya elimu kwa watoto wa kike.
“Warsha hii imeandaliwa kwa ajili ya wadau wote kutoa mawazo yao juu ya
changamoto za usawa wa kijinsia zinazoikumba sekta ya elimu pamoja na kuwapa
fursa wadau hao kushauriana kuhusu mikakati mbalimbali ya kutatua changamoto
hizo ili kuinua sekta ya elimu sio tu kwa Tanzania bali kwa Afrika
nzima,”alisema Haldorsen.
Haldorsen ameongeza kuwa mfumo wa elimu umetambua uhusiano uliopo kati ya
elimu na usawa wa kijinsia ndio maana wadau wa masuala ya elimu wa Serikali
kutoka katika baadhi ya nchi za Afrika wameamua kuungana kwa pamoja kujadili
juu ya tathmini, mpangilio na ufuatiliaji wa elimu unayozingatia jinsia.
Tanzania imekua nchi ya kwanza kuendesha warsha hiyo ya siku tatu
iliyoshirikisha maafisa waandamizi wa Serikali wanaoshughulikia mipango ya
elimu kutoka nchi za Mozambique, Zambia, Malawi, Uganda, Zanzibar na Tanzania
Bara.
Imeandaliwa kwa ushirikiano wa shirika la Plan International- Tanzania,
Global Partnership for Education (GPE), Dubai Cares pamoja na United Nations
Girls’ Education Initiative (UNGEI).