TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
TAMKO
LA PAMOJA KUTOKA MTANDAO WAKUTOKOMEZA NDOA ZA UTOTONI TANZANIA KUIPONGEZA
MAHAKAMA YA RUFAA YA TANZANIA
Mtandao
wa Kutokomeza Ndoa za Utotoni Tanzania (TECMN), unaojumuisha mashirika na Asasi
zisizo za kiserikali zaidi ya 50 ukiratibiwa na Shirika la Jukwaa la Utu wa
Mtoto kwa Sauti Moja tunapongeza Mahakama
ya Rufaa ya Tanzania kwa uamuzi wake wa
kubatilisha kifungu namba 13 na 17 vilivyopo kwenye sheria ya ndoa No. 5 ya mwaka 1971 (Sura 29).
Mtandao
wa Kutokomeza Ndoa za Utotoni kwa muda mrefu tangu kuanzishwa kwake mwaka 2012
umekuwa ukifanya jitihada na mikakati mbalimbali ya uhamasishaji na uelimishaji
juu ya athari ya ndoa za utotoni na kwa vipindi tofauti wanachama wa mtandao
wamekuwa wakifanya tafiti mbalimbali kuonesha ukubwa wa tatizo la ndoa za
utotoni na visababishi vyake ambavyo ni pamoja na umasikini, mila na desturi
pamoja na sheria ya ndoa ya mwaka 1971 kifungu cha 13 and 17 ambayo inaruhusu
mtoto wa kike kuolewa kuanzia umri wa miaka 14.
Kwa
nyakati tofauti Mtandao umeweza kuhamasisha jamii, wanahabari, viongozi wa dini,
viongozi wa kimila na viongozi wa serikali katika ngazi tofauti ili wachukue hatua
au washirikiane na Mtandao katika jitihada za kutokomeza ndoa za utotoni pamoja
na kuunga mkono jitihada za mtandao za mabadiliko ya sheria ya ndoa ya mwaka
1971.
Katika
kuhakikisha tatizo la ndoa za utotoni na mabadiliko ya sheria ya ndoa
yanatekelezwa ili kulinda haki na ustawi wa mtoto wa kike; Mtandao uliweza
kufanya mazungumzo na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kupitia Kamati ya Katiba na Sheria, Kamati ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na
Maendeleo ya Jamii pamoja na Umoja wa Wabunge Wanawake Bungeni. Vilevile katika
vipindi tofauti, Mtandao uliweza kufanya mazungumzo na Spika wa Bunge, Naibu Spika na Mwanasheria
Mkuu wa Serikali zikiwa ni harakati za kutafuta kuungwa mkono jitihada za
Mtandao unaolenga kuleta mabadiliko chanya yatakayomnusuru mtoto wa kike dhidi
ya ndoa za utotoni.
HALI YA NDOA ZA UTOTONI TANZANIA IKOJE
KWA SASA?
1. Tanzania
ni moja ya nchi zenye kiwango cha juu cha ndoa za utotoni duniani. Kwa mujibu wa takwimu za UNICEF za kati ya mwaka 2010
na 2017, Tanzania ni ya tatu kwa kuwa na viwango vya juu vya ndoa za utotoni
baada ya Sudan Kusini na Uganda. Sudan Kusini kiwango cha watoto wa chini ya
miaka 18 wanaoozwa ni asilimia 52 na nchini Uganda ni asilimia 40. Tanzania ni
asilimia 31. Nchini Kenya, ni watoto asilimia 23 wanaoozwa kabla ya kutimiza
miaka 18.
2.
Kwa wastani, kati ya watoto watano (5) wakike
wawili (2) huolewa kabla ya umri wa miaka 18. Utafiti wa afya na watu (TDHS
2015) unaonesha kuwa asilimia 31% ya wanawake kati ya umri wa miaka 20 – 24
waliolewa wakiwa na umri wa chini ya miaka 18.
3.
Takwimu za ndoa za utotoni kimkoa; Shinyanga
(59%), Tabora (58%), Mara (55%), Dodoma (51%), Lindi (48%), Mbeya (45% -),
Morogoro (42%), Singida (42%), Rukwa (40%), Ruvuma (39%), Mwanza (37%), Kagera
(36%), Mtwara (35%), Manyara (34%), Pwani (33%), Tanga (29%), Arusha (27%),
Kilimanjaro (27%), Kigoma (26%), Dar es Salaam (19%) na Iringa (8%).
4.
Ndoa za utotoni kwa hapa Tanzania huathiri
zaidi watoto wa kike kwani kwa wastani wanawake wengi huolewa mapema zaidi kwa
tofauti ya umri wa miaka 5 wakilinganishwa na wanaume.
UAMUZI
WA MAHAKAMA KUU YA TANZANIA KUHUSU MABADILIKO YA SHERIA YA NDOA YA MWAKA 1971
KIFUNGU NAMBA 13 NA 17
Baada
ya kusubiri kwa muda mrefu, hukumu ya
mahakama iliyokatwa na serikali Julai 8, 2016 kupinga kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na Rebeca Gyumi (Mwanachama wa Mtandao-Msichana
Initiative) ya kupinga sheria ya ndoa ya mwaka 1971 kifungu namba 13 na 17,
hatimaye, tarehe 23 ya mwezi Julai mwaka 2019 Mahakama ya Rufaa ya Tanzania ilikubaliana na maamuzi yaliyotolewa na Mahakama Kuu ya
Tanzania kubadilisha vifungu hivyo kwa kua ni
vya kibaguzi na vinakiuka haki ya kikatiba ya kujieleza kwakua mtoto
mwenye umri wa miaka 14 hawezi kuingia
katika mkataba wa ndoa kwa kuwa hana
ufahamu kiasi cha kuweza kujihusisha na mkataba wa ndoa na kuiamuru serikali
kuibadilisha sheria hiyo ndani ya mwaka mmoja kumruhusu mtoto wa kike kuolewa
akiwa na umri kuanzia miaka 18. .
Hukumu
hii ni ushindi kwa watoto wa kike wa Tanzania kwani imewapa ulinzi wa kisheria,
pia hii ni hatua muhimu sana kwetu sisi kama mashirika na wadau mbalimbali wa
maendeleo ya jamii tunayopigania haki za watoto wa kike kwa kuona hatua ya
kwanza inayopelekea watoto wa kike kupata haki zao za msingi kwa maendeleo yao
na taifa kwa ujumla.
Watoto
wa kike wa Tanzania wapo huru kisheria
kilichobaki ni kuunganisha nguvu zetu kwa pamoja katika kuhakikisha
tunatoa elimu kwa wadau, viongozi, Jamii na watoto kwa ujumla kwa lengo la kuwaelimisha
wahusika wote juu ya sheria hii na athari zinazotokana na ndoa za utotoni ili
kuwasaidia na kuwalinda watoto wa kike wafikie malengo na ndoto zao za kielimu.
Katiba
ya Tanzania inasema binadamu wote
huzaliwa huru, na wote ni sawa na kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na
kuthaminiwa utu wake (Ibara ya 12 (1)). Inaeleza zaidi kwamba watu wote ni sawa
mbele ya sheria, na wanayo haki, bila ya yeyote miongoni mwao kubaguliwa,
kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria. Sheria zinazoweka umri wa chini
tofauti wa kuoa au kuolewa baina ya mvulana na msichana ni za kibaguzi na
zinakiuka haki ya usawa mbele ya sheria.
ATHARI ZA NDOA ZA UTOTONI
Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 inaruhusu
ndoa za utotoni. Inakadiriwa kwamba asilimia 37 ya wasichana Tanzania wanaolewa
kabla ya kufikisha umri wa miaka 18. Umasikini, mila za kijamii na kiutamaduni,
unyanyasaji wa kijinsia, , vyote hivyo
vinachangia ndoa za utotoni.
ATHARI YA NDOA ZA UTOTONI
·
Kupoteza fursa za elimu na ujuzi wa kazi
·
Kupata maambukizo ya virusi vya ukimwi (VVU)
au magonjwa ya zinaa (STD)
·
Kunyanyasika kisaikolojia, kimwili, kijinsia
·
Kuyumba kiuchumi na kudumu katika umasikini,
·
Kukosa au kushindwa kujitawala
·
Unyanyasaji wa kimwili unyanyasaji wa maneno
·
Vifo vya watoto wachanga na watoto wa kike
pindi wanapojifungua kwa kuwa viungo vyao vya uzazi bado havijakomaa
·
Vifo vya wajawazito
·
Kuharibika kwa mimba
SHAURI LA REBECA GYUMI
Baada
ya kuona changamoto zote wanazokutana nazo watoto wa kikekatika suala zima la
kuolewa wakiwa na umri chini ya miaka 18, Rebeca Gyumi alifungua shauri
kwa niaba ya watoto wa kike walio katika
hatari ya kuingia kwenye ndoa za utotoni. Shauri la Rebeca Gyumi dhidi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Katika Shauri la Madai Na.5 ya 2016 (Shauri la
Rebeca Gyumi) lilipinga uhalali wa kikatiba wa ndoa za utotoni. Matokeo yake ni
kwamba mahakama kuu Tanzania ilitamka kwamba vifungu vya 13 na 17 vya sheria ya
ndoa ni vya kibaguzi na vinakwenda kinyume na katiba.
KUPINGA
SHERIA INAYOHUSIANA NA NDOA ZA UTOTONI
Sheria ya Ndoa imeweka vigezo
vinavyohitajika kwa watu wanaoingia katika ndoa. Kwa mujibu wa sheria, umri wa
chini kwa wasichana kuolewa ni miaka 15 na kwa wavulana ni miaka 18. Kwa mujibu
wa kifungu cha 13 cha sheria, wavulana na wasichana wanaweza kuoa au
kuolewa mapema zaidi, yaani wakiwa na umri wa miaka 14, kwa idhini ya mahakama
na miaka 15 kwa idhini ya wazazi.
Kifungu
cha 17 cha Sheria kinaelezea kwamba kwa ndoa ya msichana
mwenye umri wa chini ya miaka 18, baba yake ni lazima atoe idhini kuruhusu ndoa
hiyo, kama baba yake amefariki, basi mama yake. Kama wazazi wote wamefariki,
walezi wake ni lazima watoe idhini. Kama hakuna mlezi , hakuna idhini
inayohitajika.
Kwanini
Rebeca Gyumi alipinga vifungu vya 13 na 17 vya Sheria hii kwa misingi kwamba:
1. Vinakiuka
Ibara Ya 12(1) ya katiba ya Tanzania, katiba ambayo inatoa usawa kwa watu wote
mbele ya sheria;
2. Vinakiuka
Ibara ya 13(1) (2) ya katiba ya Muungano wa Tanzania ambayo inawalinda watu
dhidi ya ubaguzi kwa misingi ya kijinsia;
3. Watu
walio chini ya umri wa miaka 18 ni watoto na hawana uwezo wa kufanya mamuzi
sahihi juu ya kuoa au kuolewa;
4. Vinakiuka
Ibara ya 21(2) ya Katiba ya Tanzania kwa kutowapa wasichana fursa ya kushiriki
kikamilifu katika uamuzi wa kuamua mustakabali wa maisha yao
5. Vinamnyima
mtoto haki ya kupata elimu na uhuru wa mawazo.
Tarehe
8 julai, 2016, Mheshimiwa Jaji Lila J., Mheshimiwa Jaji Kihio J. na Mheshimiwa
Jaji Munisi J. walieleza kwamba vifungu vya 13 na 17 vya
sheria ya Ndoa vimepitwa na wakati na vinakwenda kinyume na katiba.
MASUALA
MUHIMU KWENYE UAMUZI WA MAHAKAMA KUU YA TANZANIA
1. Ndoa
za Utotoni Zinakwenda Kinyume na Maslahi
Muhimu ya Mtoto.
Kwa
sababu hiyo, mahakama ilieleza kwamba vifungu vya 13 na 17 vya sheria ya Ndoa
vinaruhusu watoto kuingia katika ndoa. Mahakama Kuu ya Tanzania ilieleza kwamba
haifai kuwaingiza watoto katika majukumu makubwa ya ndoa. Pia ilidokeza kuhusu
hatari kubwa ya kiafya inayowakabili wasichana pale wanapoolewa wakiwa na umri
mdogo.
2. Haki
ya Usawa Mbele ya Sheria na Kutobaguliwa kwa Namna Yoyote.
Mahakama
ilisema kwamba vifungu hivyo havitoi
usawa kwa wasichana na wavulana katika njia mbili. Kwanza umri wa ndoa ni
tofauti kati ya mvulana na msichana. Pili, wasichana chini ya miaka 18
wanahitaji ridhaa ya wazazi kuolewa wakati wavulana hawahitaji. Tofauti hii
inaleta maana kwamba, wasichana na wavulana hawatendewi sawa chini ya vifungu
vya 13 na 17 vya sheria ya Ndoa. Kwa hiyo, iliamuliwa kwamba vifungu hivyo
vinawabagua wasichana na vinakiuka Ibara za 12 na 13 za katiba ya Jamuhuri ya
Muungano wa Tanzania.
3. Sheria
ya Kimila na Kiislamu Hazitumiki Kwenye Masuala Yaliyoainishwa Kwenye Sheria
Ndoa.
4. Serikali
ilijaribu kutetea sheria zinazoruhusu ndoa za utotoni kwa msingi kwamba
ilifanikiwa ili kuziweka kwa pamoja Sheria tofauti za Kimila, Kiutamaduni na
Kidini katika ndoa. Mahakama ilikataa hilo kwa maelezo kwamba kifungu cha 11(4)
cha Sheria ya Usimamiaji Haki na Matumizi ya Sheria Kinasema. “Kanuni za sheria za kimila na kanuni za Sheria za
Kiislamu hazitatumika katika suala lolote lililoanishwa katika Sheria ya Ndoa”.
5. Haki
ya Kushiriki Katika Maamuzi Yanayogusa Maisha Yako
Mahakama kuu ilibainisha kwamba itifaki ya Maputo
inazihamasisha nchi wanachama kutunga sheria ambazo zitahakikisha kwamba hakuna
ndoa inayofungwa bila kuwapo uamuzi wa uhuru na ridhaa kamili ya pande zote na
kwamba umri wa chini wa mwanamke kuolewa lazima uwe miaka 18.
“Kwakua
Tanzania imeridhia chombo hicho cha kikanda, umefika wakati sasa wa kuchukua
hatua stahiki za kisheria kuhakikisha kwamba haki iliyotolewa chini ya ibara
21(2) ya kikatiba inapatikana kwa wote”
6. Vifungu
vya Sheria Havistahili Kutumika Tena
Katika
uamuzi wake, Mahakama kuu ilitamka kwamba, vifungu katika Sheria ya Ndoa
ambavyo vinaruhusu ndoa za utotoni havistahili kutumika.
Mahakama
ilibaini kwamba kumekuwa na maendeleo kadhaa ya kisheria katika sheria ya Ndoa.
Maendeleo haya yamefanywa ili pengine kuhakikisha kwamba, “Ustawi na ulinzi wa
mtoto wa kike unaimarishwa, na utu na heshima ya mwanamke kwa ujumla
vinalindwa”
Kwa
mfano, Sheria Maalumu ya Makosa ya Kujamiiana (SOSPA) ya mwaka 1998
imebainishwa adhabu kwa watu wanaojihusisha kimapenzi na watoto. kwa hiyo,
kuruhusu ndoa za utotoni ni kama kutoa kibali cha kufanyika kwa uhalifu.
Mahakama
iliona kwamba katika sheria kama za SOSPA na Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009,
Serikali kupitia sheria kama hizo ni kama imekiri kimyakimya kwamba haki ya
watoto kulindwa inazidiwa nguvu na haja ya kuendeleza ndoa za utotoni.
Mahakama
katika shauri la Rebeca Gyumi iliamuru Serikali kufanya marekebisho ya sheria
ndani ya mwaka mmoja na kusahihisha vifungu vya kibaguzi vya 13 na 17 na kuweka
miaka 18 kama umri wa chini unaostahili kwa ndoa kwa wavulana na wasichana.
Shauri la Rebeca Gyumi ni ushindi wa kipekee kwa mtoto wa kike wa Tanzania.
Linaonesha kwamba wanawake wanapaswa kuwa na haki ya kuridhia kuolewa na
kwamba, umri wa chini wa kuoa/kuolewa lazima uwe miaka 18 kwa mwanamme na
mwanamke. Pia linasisitiza kwamba mila na desturi hazipaswi kutumika kuwabagua
wanawake au kuwanyima haki zao.
Tunaipongeza
serikali ya Jamuhuri wa Muungano wa Tanzania kwa kuendeleza jitihada za
kuwalinda watoto kwa sheria na sera zinazowalinda watoto wa kike ikiwa ni
pamoja na marekebisho yaliyofanywa kwenye sheria ya Elimu ya mwaka 1978 ambayo
imeweka vifungu vinavyo zuia watoto wa kike kupewa ujauzito wakiwa shuleni na
kutoa adhabu ya kifungo cha miaka 30 kwa yoyote atakeyepatikana na hatia. .
Mwisho tunaiomba serikali kutekeleza maamuzi ya hukumu
na kubadili vipengele husika.
Ni jukumu letu sote kuchukua hatua kuwalinda watoto na
kukemea vikali vitendo vya ndoa za utotoni.
KWA SAUTI MOJA TUNASEMA NDOA ZA UTOTONI SASA BASI !
Tamko hili limetolewa leo tarehe 19/11/2019 na Mtandao
wa Kutokomeza Ndoa za Utotoni na kusomwa na Mratibu wa Mtandao.
Kwa
Mawasiliano Zaidi:
Michael
J. Sungusia
Mratibu
wa Mtandao TECMN
Simu +255222775 010
au +255743 902858
Barua Pepe, michael@cdf.or.tz