Waziri wa
Nishati, Dkt. Medard Kalemani amezindua rasmi huduma ya umeme katika Kata ya
Kigwe iliyopo wilayani Bahi, Mkoa wa Dodoma.
Uzinduzi huo
uliofanyika mwishoni mwa Juma, Jumamosi Februari 10 mwaka huu, ulienda sambamba
na ufunguzi wa Mtambo wa Maji ambao umeweza kufanya kazi kutokana na
upatikanaji wa huduma hiyo ya umeme.
Waziri Kalemani
alifanya uzinduzi huo akiwa katika ziara ya kazi wilayani Bahi kukagua miradi
ya umeme inayotekelezwa wilayani humo.
Awali, akiwa
katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge kumweleza nia ya
ziara yake, Waziri alisema kuwa wananchi zaidi ya 200 wataanza kupata umeme
kufuatia tukio la kurasimishwa kuwashwa kwa nishati hiyo Kigwe.
“Tunatoa
kipaumbele sana kwa Mkoa wa Dodoma kwa sasa kwani ni Makao Makuu.
Tunaweka juhudi za makusudi kuhakikisha kwamba wananchi wengi wanapata umeme na
huduma hiyo inakuwa ya uhakika,” alisema Dkt. Kalemani.
Akifafanua zaidi, alisema kuwa, Serikali imeanzisha harakati za kufanya ukaguzi kwenye utekelezaji wa Miradi yote ya umeme mkoani humo.
Alieleza kuwa
lengo la kufanya hivyo siyo tu kwa sababu Dodoma
ni Makao Makuu bali pia kama Mkoa, imebainika
kuwa miundombinu yake katika baadhi ya maeneo imepoteza ubora, hasa nguzo.
Hii
ni kwa sababu eneo hili ni tambarare na hivyo mvua ikinyesha maji yanatuama na
kuharibu nguzo mara kwa mara.
“Kwa hiyo tunaendelea
na ukaguzi wa miundombinu ili kuhakikisha Dodoma
inaendelea kupata umeme wa uhakika muda wote.”
Kwa upande wake,
Mkuu wa Mkoa pamoja na kupongeza jitihada ambazo Wizara ya nishati imekuwa
ikifanya nchi nzima katika kuhakikisha huduma ya umeme inapatikana katika
maeneo mbalimbali, pia alimwomba Waziri Kalemani kuupa upendeleo Mkoa huo kwa
kuwa ni kitovu cha nchi.
Akiwa katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Bahi katika ziara yake, Waziri Kalemani aliwasisitiza wananchi kufanya maandalizi ili umeme utakapounganishwa katika maeneo yao waweze pia kuunganisha katika makazi yao na katika maeneo yao mbalimbali ya kazi.
Aidha, alitumia
fursa hiyo kuwataka viongozi wa Halmashauri mbalimbali za vijiji kote nchini,
kuhakikisha wanajiandaa kwa ajili ya kuunganishiwa umeme katika taasisi zote za
umma zikiwemo Shule, Vituo vya Afya, Miradi ya Maji, Masoko na nyinginezo.
Vilevile, alikumbushia umuhimu wa kila mmoja kuhakikisha baada ya kuunganishiwa umeme katika eneo lake anakumbuka kulipa bili za huduma hiyo muhimu.
“Usipolipa, Serikali itakukatia umeme hivyo kurudisha nyuma maendeleo yako,” alisisitiza.
Jambo jingine
ambalo Waziri Kalemani alisisitiza ni kwa wakandarasi kuhakikisha wanawagawia
bure wateja 200 wa kwanza watakaojitokeza kuunganishiwa umeme wa REA, kifaa cha
Umeme Tayari (UMETA) kama ilivyoelekezwa na
Serikali na siyo vinginevyo.
“Kifaa hicho
hakiuzwi kwa sasa hadi wateja 200 wa mwanzo wakamilike na kugawiwa bure ikiwa
ni njia ya kuhamasisha wananchi wengi vijijini kujitokeza kuunganisha umeme.
Mkandarasi yeyote atakayebainika kuwauzia wananchi au kutowapatia kifaa hicho
wale wateja 200 wa kwanza kama tulivyoelekeza,
tutamchukulia hatua.”
Wakizungumza kwa
nyakati tofauti katika ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Bahi Elizabeth Kitundu na
Mbunge wa Jimbo hilo,
Omari Baduel walipongeza jitihada za Serikali kupitia Wizara ya Nishati katika
kuhakikisha wananchi, hususan wa vijijini wanafikiwa na huduma muhimu ya umeme.
Akiwasilisha
taarifa ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kwa Waziri Kalemani katika
ziara hiyo, Meneja wa Shirika hilo wa Wilaya ya Bahi, Kitila Bryceson alisema
kuwa, Wilaya hiyo ina jumla ya wateja 1498 wa umeme hadi kufikia mwezi Januari
mwaka huu na kwamba ina laini ya umeme yenye urefu wa jumla ya kilomita 78.8 na
jumla ya Mashine Poozo (Transfoma) 35 zinazohudumia wananchi, taasisi na
viwanda.
No comments:
Post a Comment