Friday, February 9, 2018

NSSF YATOA MSAADA MASHUKA 600 HOSPITALI YA BAGAMOYO.



Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Majid Mwanga (wa tatu kutoka kulia) akipokea Mashuka 600 ikiwa ni msaada kutoka Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) anaemkabidhi ni Kaimu Meneja Masoko wa NSSF ( wa pili kulia) Salim Khalfani, kutoka  kushoto ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamoyo, Fatuma Latu, Mwenyekiti wa kamati ya huduma za jamii Dickson Makamba, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bagamoyo, Ally Ally Issa. 

Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga, Timu ya usimamizi wa Afya Halmashauri ya Bagamoyo (CHMT) Madiwani wa Halmashauri ya Bagamoyo, kwa pamoja wakipokea msaada wa mashuka 600 kutoka Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) anaekabidhi wakipeana mikono na Mkuuu wa wilaya ya Bagamoyo ni Kaimu Meneja wa Masoko NSSF, Salim Khalfani.
.........................................
Shirikia la Taifa la hifadhi ya jamii (NSSF) limetoa msaada wa mashuka mia sita (600) kwa Hospitali ya Bagamoyo.

Akizungumza wakati wa kukabidhi mashuka hayo Kaimu Meneja wa Masoko na uhusiano, Salim Khalfani, alisema shirika la NSSF ni shirika linalohudumia jamii hivyo kutoa misaada ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yao katika kujenga mahusiano mema na jamii.

Aidha, alimtaja Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo kuwa ni kiongozi anaejali watu wake anaowaongoza hali iliyompelekea kuomba msaada wa mashuka kwa shirika la NSSF.

Akizungumza wakati wa kupokea msaada huo Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Alhaj, Majid Mwanga aliwashukuru NSSF kwa msada huo ambao ni muhimu katika sekta ya Afya.

Alisema Hospitali ya Bagamoyo inakabiliwa na changamoto kadhaa na kwamba serikali ya wilaya kwa kushirikiana na ofisi ya Mkurugenzi wa Bagamoyo imejipanga kutatua changamoto hizo kupitia wadau mbalimbali waliopo ndani na nje ya Bagamoyo.

Mkuu huyo wa wilaya ya Bagamoyo, alimtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamoyo kuhakikisha anafanya utaratibu wa ununuzi wa mashine ya kufulia ili mashuka hayo yadumu katika hali ya usafi muda wote.

Aidha, alitumia nafasi hiyo kuwataka Madaktari na manesi katika Hospitali ya wilaya ya Bagamoyo kuacha kutoa lugha chafu kwa wagonjwa na kwamba watekeleze majukumu yao kwa mujibu wa maadili ya kazi yao.

Alisema uboreshaji wa vitanda vya wagonjwa kwa kuweka mashuka mapya uende sambamba na uwajibikaji ili kuleta faraja kwa Hospitali hiyo ambayo inahudumia watu kutoka ndani na nje ya Bagamoyo.

Nae Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Dkt. Salvio Wikesi alisema anamshukuru Mkuu wa wilaya kwa juhudi ya kutafuta wahisani ili kuweza kusaidia matatizo mbali mbali katika Hospitali ya Bagamoyo.

Dkt. Salvio alisema Hospitali ya wilaya ya Bagamoyo ina jumla ya vitanda 100 ambapo kwa mujibu wa muongozo wa wizara ya Afya kila kitanda kimoja kinahitaji mashuka nane na hivyo mashuka yanayohitajika ni 800 huku Hospitali ikiwa na mashuka 325 na hivyo kufanya Hospitali hiyo kuwa na upungufu wa mashuka 475 .

Alisema kufuatia msada huo wa mashuka 600 Hospitali hiyo ina ziada ya mashuka 125 kwa sasa na kwamba tatizo la mashuka litakuwa limekwisha kabisa katika Hospitali hiyo.

 Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Majid Mwanga, akizungumza mara baada ya kupokea mashuka 600 kutoka Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii, katika Ukumbi wa Halmashauri ya Bagamoyo, kulia ni Kaimu meneja masoko wa NSSF, Salim Khalfani na kushoto ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bagamoyo, Ally Ally Issa.

Kaimu meneja masoko wa NSSF, Salim Khalfani, akizungumza wakati wa makabidhiano ya mashuka 600 yaliyotolewa na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii, (NSSF).

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamoyo, Fatuma Latu, akizungumza wakat wa makabidhiano ya mashuka 600 kutoka Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Timu ya Usimamizi wa Afya Halmashauri ya Bagamoyo (CHMT) wakifuatilia kwa karibu hafla fupi ya kupokea mashuka 600 kutoka Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii, (NSSF) iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Bagamoyo.
 

No comments:

Post a Comment