Wednesday, February 14, 2018

MADIWANI CHALINZE WAMUOMBA RAIS AINGILIE KATI KILIO CHA MAJI.



BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Chalinze ,limemuangukia rais Dkt. John Magufuli kwa kumuomba aende kujionea mradi wa maji awamu ya tatu WAMI-CHALINZE ambao umekwama huku wananchi wakiwa hawana maji kwa takriban miezi mitatu sasa.

Wamesema Rais ,ndio mwenye mamlaka za mwisho kwani waziri mkuu alishafika kujionea mradi huo ambapo mkandarasi aliongezewa muda lakini mkataba umekwisha na hakuna kilichofanyika.

Wakitoa kilio hicho ,wakati wa kikao cha bajeti ,baadhi ya madiwani akiwemo diwani wa Talawanda ambae pia ni mwenyekiti wa halmashauri hiyo,Saidi Zikatimu alisema kuna kila sababu serikali ikaingilia kati na kutoa tamko ili kurejesha imani kwa wananchi.

Alieleza tatizo hilo ni kubwa kwani zipo baadhi ya shule hazina maji safi na salama na wanahofiwa wanafunzi kupata magonjwa ya mlipuko.

“Maji ni tatizo mradi wa WAMI -CHALINZE, kamati ya fedha tulishaenda lakini majibu ya meneja wa CHALIWASA Christer Mchomba  hayakuturidhisha “

“Baraza hili linaimani na Mh.Rais jambo hilo lichukuliwe ufumbuzi wa haraka zaidi ya miezi miwili ama mitatu hakuna maji, serikali itoe tamko kuhusiana na mradi huo “; alisema Zikatimu .

Zikatimu alisema zipo shule za sekondari ya Kikalo ,Miono ,Chalinze hazina maji na wanafunzi wameshaanza kusumbuliwa na magonjwa ya matumbo kutokana na ukosefu wa maji.

Aliomba serikali kuu,CCM na halmashauri ishirikiane kwa hilo ili kupata ufumbuzi.

Zikatimu alieleza kwasasa, wamechukua hatua ya kuzungumza na watu wenye maboza ya kusambaza maji kwenye maeneo muhimu ya kijamii kama mashuleni kwani meneja wa CHALIWASA  aliwaambia kuna uwezekano wa kuchukua maji katika chanzo chao cha maji ambayo yatawasaidia wakati suluhu ikiendelea kutafutwa .

Nao diwani wa kata ya Miono Juma Mpwimbwi,Diwani wa Lugoba Rehema Mwene na diwani wa Kimange Hussein Hading’oka walisema hali ya mradi mkubwa wa aina hiyo iliyofikia ni mbaya na haileti taswira nzuri kwa jamii.

Diwani wa kata ya Miono ,Juma Mpwimbwi,alisikitika kutokuwa na maji ya uhakika kwa miaka mingi hali ambayo inakatisha tamaa wananchi.

“Rais aje kujionea labda kauli yake itasaidia kutatua changamoto ya mradi huu:;”Mradi huu sio rafiki tena na jamii shule hazipati maji na unasababisha usumbufu kwa wanafunzi ambao wakati mwingine inabidi waache masomo wakatafute maji ;” alifafanua Mpwimbwi.

Mpwimbwi alisema ,amehamasisha kila kaya katika kata ya Miono kutoa 2,000 itakayosaidia kulipia maboza yanayosambaza maji yatakayowezesha kusaidia wanafunzi .

“Kuna shule hizi za sekondari ya Miono na Kikalo zinapata shida,walimu wanaogopa kuchangisha wanafunzi kutokana na suala la elimu bure,kila trip moja ya boza kwa wiki ni sh.100,000 ,mkuu gani wa shule atamudu kulipia ama diwani ” alisema Mpwimbwi.

Mkazi wa Bwilingu,Chalinze Zulfa Hassan alieleza wanalazimika kununua madumu ya maji matano hadi kumi kwa siku kwa ajili ya matumizi ya familia.

Alisema uwezo wa kutoa sh.2,500 na 5,000 kila siku hawana hivyo wnaiomba serikali itatue changamoto ya maji Chalinze.

Kwa upande wake ,mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Bagamoyo alhaj Abdul Sharif ,alisema ukienda kwa meneja wa CHALIWASA hupati majibu ya kuridhisha hivyo viongozi kukosa majibu mazuri ya kuwaeleza wananchi.

Alisema ni vyema wizara ya maji ikaeleza kinaga ubaga kinachofuata kwenye mradi baada ya mkataba wa ujenzi wa mradi wa maji WAMI-Chalinze kuisha.

Alhaj Sharif alisema, serikali inafanya juhudi kubwa kuendeleza viwanda na Chalinze ni moja ya halmashauri yenye viwanda na wawekezaji lakini kukosekana kwa maji miezi mitatu anahofu ya kukatisha tamaa baadhi ya wawekezaji .

Meneja wa Chaliwasa alielezea serikali inaendelea kuchukua hatua na kufanya jitihada za kuondoa tatizo la maji tangu mwaka 2001 ,ilipoanza kutekeleza mradi wa maji Chalinze kwa awamu mbalimbali.

Mapema sept mwaka jana Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitembelea baadhi ya viwanda mkoani Pwani ,na kutoa agizo la wiki mbili kwa waziri wa maji kutathmini matokeo ya mwenendo wa mradi wa maji wa mradi wa WAMI CHALINZE ,;:      ili kutoa utaratibu na kama sheria ingeruhusu kuvunja mkataba ikiwa mkandarasi ameshafikia kiwango cha asilimia 50 ya utekelezaji.

No comments:

Post a Comment