Friday, February 2, 2018

BAKHRESA AANZA KUPANDA MIWA BAGAMOYO KWAAJILI YA KIWANDA CHA SUKARI.


Baadhi ya miche ya miwa ikiwa katika kitalu tayari kwa kupandwa katika shamba la Bagamoyo Sugar mwishoni mwa wiki.
Mtaalam mzawa wa kufunga mabomba ya maji ya umwagiliaji miwa katika shamba la Bagamoyo Sugar Bi. Gloria Mmasi akiendelea na shughuli za ufungaji wa mabomba katika shamba hilo tayari kwa kuanza kuotesha miwa.
..............................................

Agizo la Rais John Pombe Magufuli la kuipatia Kampuni ya Said Salim Bakhresa (SSB) Group LTD ardhi yenye ukubwa wa ekari 10,000 kwa ajili ya kuwekeza katika kilimo cha miwa na ujenzi wa kiwanda cha sukari katika Wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani limetekelezwa.

Msemaji wa Makampuni ya Said Salim Bakhresa (SSB) Group LTD, Bw Hussein Sufian ameiambia Idara ya Habari (MAELEZO) leo katika mahojiano maalumu ilipokuwa ikifuatilia utekelezaji wa agizo la Rais Magufuli alilolitoa tarehe 6 Oktoba, 2017 baada ya kufungua kiwanda cha vinywaji baridi cha  Kampuni hiyo kilichopo Mkuranga Mkoani Pwani.

Bw. Sufian amesema, tayari Kampuni yake imetenga takriban Shilingi Milioni 75/- kwa ajili ya kuanza uwekezaji katika shamba hilo kwa shughuli za kilimo cha miwa na kufafanua kuwa, hatua ya awali ya upandaji wa miwa kwenye vitalu imeanza.

 Amesema, maandalizi ya upandaji wa miwa katika Kitalu A chenye ekari 48 umekamilika. Aidha, upandaji wa miwa katika eneo la jumla ya ekari 8 kati ya hizo utaanza tarehe 3 Februali na ekari nyingine 40 utafanyika mwezi Juni na Julai, 2018.

“Baada ya kukamilika kwa upandaji katika Kitalu “A” mwaka huu (2018), tunatarajia ifikapo Januari na Juni 2019 tutaendelea kupanda miwa kwenye kitalu “B” chenye ukubwa wa ekari 300. Mzunguko huo utaendelea hivyo hivyo mpaka kufikia hekari 2030 ambazo tumekusudia kuanza ujenzi wa kiwanda mapema 2019 na uzalishaji wa sukari kiwandani ifikapo Septemba 2020, “alisema Bw. Sufian.

Akielelezea zaidi juu ya mradi huo, Bw. Sufian amesema kwamba tayari watu 50 wameajiriwa, kati ya hao 20 ni wa kudumu na 30 vibarua. Watu 5 wanafanya kazi za kiufundi na 45 nguvu kazi. 

Aidha, Kampuni hiyo imeajiri Wataalamu 2 kutoka nje ambao ni Bw. Abraham Star Mtaalamu wa Umwagiliaji kutoka Israel na Mtaalamu wa Kilimo cha miwa kutoka India, Bw Narayan Krishna, kiwanda kinakusudia kuajiri watu 1000 ifikapo mwaka 2020.

Ili kilimo hicho cha miwa kiwe endelevu,  pamoja na mambo mengine uchimabji wa visima na utengeneaji wa mabwawa matatu umefanyika ambapo maji yanavutwa kutoka mto Wami kilometa 5 mpaka katika bwawa lililotengenezwa la Tambezi 1.

Maji yanapojaa yanavutwa kupelekwa bwawa dogo katika Kitalu A na sehemu ya mitambo ya  kuchuja maji, ambapo kila Kitalu kitakuwa na kituo cha kusukuma maji na kupeleka kwenye mabomba makubwa kisha madogo yanayopita katikati ya mimea iliyopandwa na kufanya umwagiliaji wa matone.

Agizo la Rais Magufuli lilikusudia kuondoa pengo la uzalishaji wa sukari kwa matumizi ya kawaida nchini ambapo katika kipindi cha mwaka 2016/ 2017 mahitaji yalikawa ni tani 590,000 kati ya hizo tani 135,000 ni mahitaji ya kiwandani na 455,000 ni mahitaji ya kawaida ya binadamu.

Uzalishaji wa sukari nchini ulikuwa tani 350,846 na kufanya kuwa na upungufu wa tani 259,156.  Hivyo uzalishaji wa tani elfu 30 mpaka 70 utaondoa pengo la uhaba wa sukari nchini Tanzania.
Eneo la shamba la Bagamoyo Sugar litakalo oteshwa miwa likiwa katika hatua za awali tayari kwa kuoteshwa miwa mwishoni mwa wiki.
Mtaalam mzawa wa upandaji miwa katika shamba la Bagamoyo Sugar akionesha waandishi wa habari (hawapo pichani) jinsi ya kuapanda miwa.
Baadhi ya wafanyakazi wa shamba la Bagamoyo Sugar wakiendelea na maandalizi ya shamba tayari kwa kuotesha miwa.
Mmoja wa wafanyakazi wa shamba la miwa akimwagilizia baadhi ya miche ya miwa tayari kwa kuoteshwa katika shamba la Bagamoyo sugar.

No comments:

Post a Comment