Mkuu
wa Wilaya ya Bagamoyo, Alhaj, majid Hemed Mwanga, amewaonya waendesha pikipiki
(Bodaboda) kuzingatia sheria za uslama barabarani ikiwa ni pamoja na kuvaa
kofia ngumu ili kuepuka ajali za mara kwa mara na zenye madhara.
Mkuu
huyo wa wilaya alitoa kauli hiyo alipofanya Mkutano wa hadhara katika kitongoji
cha Maji Coast kata ya Magomeni katika utaratibu
wake wa kuhutubia kila kata zilizopo ndani ya wilaya yake.
Alisema
mwendo kasi, upakiaji wa mishikaki pamoja na kutovaa kofia ngumu ni miongoni
mwa sababu zinazopelekea ajali zenye madhara kwa bodaboda.
Alisisitiza
kuwa boda anapaswa kovaa kofia ngumu kila aendeshapo bodaboda na kumuagiza Mkuu
wa polisi wilaya ya Bagamoyo kufuatilia waendesha bodaboda wote wilayani humo kama wanafuata sheria.
Aidha,
alisema wazazi na jamii kwa ujumla wanapaswa kuwaelimisha vijana wao
wanaoendesha boda boda juu ya kujifunza sheria za barabarani na kuzifuata
wakati wa kuendesha kwani madhara yatokanayo na ajali za bodaboda si ya familia
tu bali ni Taifa kwa ujumla kwa kupoteza nguvu kazi ya Taifa.
Katika
hatua nyingine Mkuu huyo wa wilaya ambae pia ni Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi
na usalama wilaya amewataka waendesha Bodaboda wote wilayani humo kuacha
kujihusisha na ubebaji mali
za magendo ikiwa ni pamoja ubebaji wahamiaji haramu,
Alisema
vijana wengi wa Bodaboda wanabeba bidhaa za magendo ikiwemo sukari, mafuta ya
kula na vinginevyo na kupelekea kuikosesha serikali mapato huku wahamiaji
haramu wakitumia bodaboda kupitishwa njia zisizo rasmi kufika wanapotaka.
Wakati
huo huo amepiga marufuku mgambo kukamata Bodaboda kwakuwa Mgambo hawajui sheria
za barabarani na ukamataji wao pia unakiuka sheria.
Alimtaka
Mkuu wa polisi kusimamia hilo
kuhakikisha kuwa bodaboda zote zinazokiuka sheria za usalama barabarani na zile
zinazojihusisha na biashara za magendo polisi wahusike kuzikamata na sio
mgambo.
Kwa
upande wake Mkuu wa Polisi Wilaya ya Bagamoyo, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi
(SSP) Adam Maro alisema kila mwananchi anapaswa kutii sheria bila ya shuruti.
Alisema
jeshi la polisi kazi yake kulinda usalama wa raia na mali zao na kuzuia uhalifu hivyo
kila mwananchi anapaswa kuisaidia polisi katika kuhakikisha kuwa uhalifu
hautokei kwenye mitaa mbalimbali.
Alisema
ameandaa utaratibu wa kutoa elimu kwa raia juu ya utii wa sheria hivyo kupitia
wenyeviti wa vitongoji mikutano ya hadhara itaandaliwa na jeshi la polisi
litafika kutoa elimu ya utii wa sheria bila ya shuruti na jinsi ya kukabiliana
na uhalifu kwenye maeneo wanayoishi.
Akizungumzia
swala la ulinzi shirikishi SSP. Adam Maro alisema ulinzi shirikishi unambulika
kisheria hivyo utekelezaji wake unapaswa ufanyike kwa makubaliano ya wananchi
wenye na njia zipi na wakati gani wafanye huo ulinzi shirikishi.
Wananchi
wa Kitongoji cha Maji
Coast kata ya Magomeni
wilayani Bagamoyo wakifuatilia Mkutano ulioitishwa na Mkuu wa wa Wilaya.
No comments:
Post a Comment