Naibu Waziri wa
Nishati, Subira Mgalu amekagua mitambo miwili ya umeme yenye uwezo wa kuzalisha
megawati 2 kila mmoja itakayofungwa katika kituo cha kuzalisha umeme kwa
kutumia gesi asilia cha Mtwara.
Amekagua mitambo
hiyo tarehe 21 Februari, 2018 katika eneo la Mkandarasi, jijini Dar es Salaam
ambapo kampuni ya Mantrac ndiyo iliyopewa kazi ya kufunga mitambo hiyo.
Baada ya kukagua
mitambo hiyo, Naibu Waziri alisisitiza kuwa, Serikali inafuatilia kwa karibu
utekelezaji wa kazi hiyo lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa
mitambo hiyo inafikishwa na kusimikwa mkoani Mtwara mapema iwezekanavyo
ili kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme katika mkoa wa Mtwara pamoja na
Lindi.
Kabla ya kukagua
mitambo hiyo, Naibu Waziri Mgalu alifanya kikao na watendaji wa kampuni hiyo ya
Mantrac pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) lengo likiwa ni kufahamu
maendeleo ya kazi hiyo.
Akizungumza
katika kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa Mantrac, Ahmed Saleh alimweleza
Naibu Waziri kuwa mpaka sasa mitambo hiyo tayari imewasili jijini Dar es Salaam
na kinachosubiriwa kwa sasa ni kuwasili kwa kontena maalum zitakazotumika
kuwekea mitambo hiyo kabla ya kusafirishwa kuelekea mkoani Mtwara.
Aliongeza kuwa,
kazi ya usafirishaji wa mitambo hiyo kwenda mkoani Mtwara itafanyika mwanzoni
mwa mwezi Aprili mwaka huu na kwamba kazi ya kufunga mitambo hiyo, majaribio na
makabidhiano itafanyika tarehe 9 hadi 30 mwezi Aprili mwaka huu.
Kituo cha
kuzalisha umeme kwa Gesi asilia mkoani Mtwara kina mitambo Tisa
yenye uwezo wa kuzalisha megawati 2 kila mmoja. Kituo kwa sasa kinazalisha
umeme wa kiasi cha megawati 16 kufuatia mtambo namba Tisa
kuwa nje kwa matengenezo.
Kuongezeka kwa
mashine hizo mbili mpya (4 MW) kutafanya uwezo wa kituo hicho kuongezeka na
kufikia megawati 22 na hivyo kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme
katika mikoa ya Lindi na Mtwara.
No comments:
Post a Comment