Mtaalam wa Huduma ya Usikivu
katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Mathayo Majogoro Alfred (katikati)
akiunganisha kifaa cha usikivu cha nje na cha ndani ili mtoto Matilda Katobesi
aweze kusikia kwa mara ya kwanza. Kulia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Pua,
Koo na Masikio, Dkt. Edwin Liyombo akifuatilia na kushoto ni mama wa mtoto
huyo, Angelina Cosmas.
................................
Watoto sita ambao
wamewekewa vifaa vya usikivu Januari mwaka huu katika Hospitali ya Taifa
Muhimbili (MNH) leo wameanza kusikia kwa mara ya kwanza baada ya kuwashiwa
vifaa hivyo.
Kuwashwa kwa
vifaa hivyo kumeleta furaha kwa wazazi kwani wameshuhudia watoto wao wakisikia
sauti kwa mara ya kwanza na hivyo kuwajengea matumaini ya watoto hao kuanza
maisha mapya.
Zoezi la
kuwawashia vifaa hivyo (Switch On) limefanyika leo katika Hospitali ya Taifa
Muhimbili kwa kushirikiana na wataalaam kutoka Medel Austria ambao ndio
wasambazaji wa vifaa hivyo.
Akizungumza na
waandishi wa habari , Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Pua, Koo na Masikio
Dkt. Edwin Liyombo amesema watoto hao walifanyiwa upasuaji wa upandikizaji
kifaa cha usikivu Januari mwaka huu ambapo zaidi ya asilimia 80 ya upasuaji huo
ulifanywa na watalaam wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili .
‘’Watoto
hawa wataanza maisha mapya ya kusikia sauti mbalimbali katika mazingira
yanayowazunguka baada ya kuunganisha vifaa hivi na kuviwasha’’. Amesema Dkt.
Liyombo.
Akifafanua
amesema mbali na watoto hao sita lakini pia watoto wengine watano ambao
walifanyiwa upasuaji huo mwaka jana na wengine sita ambao
walifanyiwa upasuaji huo nchini India nao wamekuja kufuatiliwa maendeleo yao
ili kubaini changamoto zinazowakabili na kupewa ushauri wa
kitaalam.
Akielezea ukubwa
tatizo Dkt. Liyombo amesema takwimu za Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO)
zinaonesha kuwa katika watoto 1,000 wanaozaliwa, inakadiriwa kuwa watoto
watano wanazaliwa na tatizo kubwa la usikivu .
Pia amesema MNH
ipo kwenye mchakato wa kuanzisha utaratibu wa kuwachunguza watoto wachanga ili
kubaini mapema wenye matatizo yakutosikia.
Kwa upande wake
Muwakilishi kutoka Medel Fayaz Jafar amesema upasuji huo umekua na mafanikio
makubwa kwakua katika awamu hiyo kumekua na mabadiliko kwani
asilimia kubwa ya upasuaji umefanywa na watalaam wa MNH na kwamba
hatua hiyo ni ya kuridhisha.
Huduma ya
Upandikizaji wa kifaa cha usikivu (Cochlear Implant) ilizinduliwa Juni 7 , 2017
na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii , Jinsia , Wazee na Watoto
Mheshimiwa Ummy Mwalimu hivyo Tanzania imekuwa nchi ya pili kutoa huduma hiyo
katika nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki baada ya Kenya. Aidha Tanzania
imekuwa nchi ya kwanza kutoa huduma hiyo kupitia Hospitali ya Umma ambayo
ni Muhimbili yenye hadhi ya ubingwa wa hali ya juu.
Mtoto Matilda kwa mara ya kwanza tarehe 24, Januari, 2018 akianza kutamka baadhi ya maneno baada ya
kufundishwa na mtaalamu wa sauti kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Wazazi wa watoto wenye matatizo
ya kusikia wakiwa kweny mkutano huo.
No comments:
Post a Comment