*Asisitiza
ni kinyume na maelekezo ya Serikali.
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema kitendo cha watoto kurudishwa nyumbani kwa
sababu ya mzazi au mlezi kuto changia michango shuleni ni kinyume na maelekezo
ya Serikali.
Amesema Serikali
kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ilitoa Waraka wa Elimu
Namba 3 wa mwaka 2016 ambao pamoja na mambo mengine, ulipiga marufuku
michango ya aina yoyote isiyo ya lazima katika Elimumsingi.
Waraka
huo ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 sambamba
na maelekezo ya Ibara ya 52(a) ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi
(CCM) ya mwaka 2015-2020 inayosisitiza utoaji wa Elimumsingi bila malipo.
Waziri
Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Februari 9, 2018) bungeni mjini Dodoma wakati akitoa hoja
ya kuahirisha mkutano wa 10 wa Bunge la 11. Bunge limeahirishwa hadi Aprili 3,
mwaka huu.
Amesema
katika siku za hivi karibuni kumejitokeza malalamiko kuhusu baadhi ya shule
kuchangisha michango mbalimbali kutoka kwa wazazi na walezi na kusababisha
watoto kurudishwa nyumbani kwa sababu ya mzazi au mlezi kuto changia michango
shuleni.
“Napenda kutumia
fursa hii kutoa wito kwa watendaji wa elimu kuanzia Wakurungezi wa Halmashauri
pamoja na wadau wote wa elimu kuzingatia maelekezo ya Waraka uliotolewa na
Serikali, ambapo majukumu ya kila mdau katika kutekeleza Mpango wa Elimumsingi
Bila Malipo yamefafanuliwa.”
Akizungumzia
fedha zilizotolewa katika utekelezaji wa mpango huo, Waziri Mkuu amesema katika
kipindi cha mwezi Julai hadi Desemba, 2017, Serikali imetuma moja kwa moja
shuleni jumla ya sh. bilioni 124.8.
“Fedha
zinazopelekwa moja kwa moja shuleni kwa mwezi ni shilingi bilioni 20.8 na
shilingi bilioni 3.06 hupelekwa Baraza la Mitihani kwa ajili ya fidia ya
gharama za mitihani kwa wanafunzi wa shule za Serikali. “
“Ruhusa
ya michango shuleni ipo, kutoka mtu mmoja mmoja, vikundi au Taasisi. Hata
hivyo, michango yote sasa itafikishwa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ili
ashirikishe Kamati ya Shule za Msingi na Bodi kwa Shule za Sekondari. Walimu
wasisumbuliwe na michango ili wajikite na taaluma.”
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kukusanya
taarifa kutoka shule mbalimbali za Sekondari za Serikali kwa lengo la kujua
hali ya umiliki wa ardhi katika shule hizo.
Hatua
hiyo imekuja kufuatia kuwepo kwa changamoto ya umiliki wa ardhi kutokana na
baadhi ya shule kutokuwa na hati miliki, ambapo inatarajia
kuhusisha shule za Sekondari Kongwe zipatazo 89.
Amesema
zoezi hilo
litakapokamilika litawezesha Serikali kuandaa hati miliki kwa shule zenye
umiliki wa Serikali na pia kufanya maamuzi kwa shule ambazo umiliki wake uko
chini ya taasisi za dini.
Waziri
Mkuu amesema kupitia zoezi hilo
maeneo ya mipaka ya shule ikiwemo viwanja vya michezo vitatambuliwa na
kujumuishwa kwenye ramani za shule. “Zoezi la ufuatiliaji wa umiliki wa ardhi
kwa shule za msingi na shule za Sekondari zilizobaki za Serikali litaendelea
kufanyika ili kuondoa changamoto za migogoro ya ardhi.”
IMETOLEWA
NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
1.
L. P.
980,
41193
– DODOMA.
IJUMAA,
FEBRUARI 9, 2018.
No comments:
Post a Comment