Saturday, February 24, 2018

DAWASA KUONDOA TATIZO LA MAJI BAGAMOYO.


Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga, (katikati) akiongoza Mkutano wa kujadili upatikanaji wa maji Bagamoyo pamoja na kuanzisha mfumo wa kusafirisha maji taka.
........................................................... 
Wadau wa maji wilayani Bagamoyo wamekutana kujadili namna ya kuboresha miundombinu ya maji safi pamoja na kuandaa mpango mkakati wa kuanzisha namna kusafirisha maji taka ili mji wa Bagamoyo ubaki safi na salama.

Mwenyekiti wa Mkutano huo, Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga alisema kufuatia kukua kwa mji wa Bagamoyo ipo haja ya kujadili namna bora ya kusafirisha maji taka badala ya kuwa na maeneo yasiyo rasmi kwa utupaji wa taka.

Alisema lengo la mkutano huo ni kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu mradi wa maji taka ambao DAWASA tayari wameshafanyia upembezi yakinifu juu ya utekelezaji wa mradi huo.

Akizungumza katika Mkutano huo, Mhandisi wa Miradi Chrisitian Gava alisema katika kipindi cha mwaka 2014 mpaka 2016 Mamlaka ya maji safi na maji taka Dar es Salaam (DAWASA) imeongeza uzalishaji kutoka mita za ujazo milioni 262 mpaka mita za ujazo milioni 466 kwa siku  ambazo zinazalishwa katika mitambo ya Ruvu juu na Ruvu chini iliyoko Bagamoyo.

Alisema uzalishaji huo umekuwa hadi kufikia kiwango hicho baada ya kuzinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli Mwezi Juni 2017.

Aliongeza kwa kusema kuwa,  kufuatia hali hiyo uzalishai wa maji kwa ujumla katika maeneo yanayohudumiwa na DAWASA ikiwemo wilaya ya Bagamoyo umeongezeka kutoka mita za ujazo milioni 300 mpaka mita za ujazo milioni 544,000 kwa siku.

Aidha,  alisema uzalishaji wa maji kutoka Ruvu juu, Ruvu chini, mtoni, na Visima vidogo umeongezeka kutoka lita milioni 300 mpaka lita milioni 502 kwa siku.

Alifafanua kuwa, katika kuhakikisha adha ya maji inaondoka katika wilaya ya  Bagamoyo DAWASA inaendelea na mradi wa ujenzi wa tenki la kuhifadhia na kusambaza maji katika maeneo ya mji wa Bagamoyo lenye ukubwa wa mita za ujazo 6000, ambalo lina uwezo wa kuhifadhi maji lita milioni sita.

Alisema Tenki hilo litakapokamilika litahudumia wananchi wa maeneo ya Mpii, Zinga, Kiromo, Kitopeni, Ukuni, Kerege, Buma, Mataya, Bagamoyo mjini na ukanda maalum wa ewekezaji EPZA.

Akizungumzia Mradi wa usanifu wa mpango wa muda mrefu na muda mfupi wa kujenga mfumo wa kutibu majitaka, Mhandisi Christian Gava alisema tayari muandaaji wa mpango mkakati ambae ni Mhandisi mshauri (Consultant) ameshaanza kazi  kwaajili ya kupembua na kuandaa mpango mkakati wa muda mrefu pamoja na kupendekeza  mfumo nafuu wa kutibu majitaka katika wilaya za Kibaha, Bagamoyo na eneo  maalum la uwekezaji wilayani Bagamoyo  (BSEZ).

Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Kawambwa amesema mji wa Bagamoyo unakuwa kwa kasi hivyo ni vyema mikakati ya kukabiliana na majitaka iwepo ili kwenda sambamba na ukuaji wa mji.

Alisema katika kkufanya mji kuwa wa kisasa usiokuwa na taka kila mahali, ni vyema maandalizi ya kitaalamu yakafanyika mapema ili kila mwananchi ajue namna ya kusafirisha majitaka badala ya kuacha kila mtu atupe taka kwa namna anayoitaka yeye.

Akizungumza wakati wa kufunga mkutano huo, Mwenyekiti wa mkutano huo ambae  ni Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Majid Mwanga alisema anamshukuru Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya maji safi na maji taka (DAWASA) kwa kushirikiana na serikali ya wilaya ya Bagamoyo katika kuboresha miundombinu ya maji safi na maji taka ndani ya Wilaya ya Bagamoyo. 
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamoyo, Fatuma Latu akiwatambulisha washiriki wa mkutano huo mbele ya Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo ambae ndiye Mwenyekiti wa Mkutano huo. 
Mhandisi wa Miradi kutoka mamlaka ya maji safi na maji taka (DAWASA) Christian Gava akiwasilisha Taarifa ya Miradi ya kusambaza maji safi pamoja na kutibu maji taka katika wilaya ya Bagamoyo.
Wahandisi kutoka DAWASA wakisikiliza kwa makini mapendekezo kutoka kwa washiriki wa mkutano huo uliofanyika ukumbi wa Halmashari ya Bagamoyo.
Madiwani wa Halmashauri ya Bagamoyo pamoa na watalamu wa Halmashauri hiyo wakisikiliza Taarifa ya wataalamu wa DAWASA. 
Mwenyekiti wa mkutano huo ambae ni Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga (katikati) kulia ni Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Kawambwa, Kushoto ni Makamo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bagamoyo,  Saidi Ngatipula.

No comments:

Post a Comment