BAADHI ya madiwani wa wilaya ya Kisarawe Mkoani Pwani ,wakionekana
kusikiliza jambo wakati wa baraza la madiwani lililofanyika mjini hapo .
Picha na Mwamvua Mwinyi
......................................
Na Mwamvua Mwinyi, Kisarawe
BARAZA la madiwani la halmashauri ya wilaya ya Kisarawe mkoa wa Pwani,
imeazimia kumfukuza kazi mganga mfawidhi wa zahanati ya Mtakayo wilayani humo
Dkt. Emmanuel Benedict.
Benedict amefukuzwa katika nafasi hiyo kutokana na kutowajibika
ipasavyo,utoro na kufunga zahanati kwa siku tisa hali iliyokwamisha utoaji
huduma ndani ya siku hizo .
Mwenyekiti wa halmashauri ya Kisarawe Hamisi Dikupatile akizungumza baada
ya kumalizika kwa baraza la madiwani alieleza wamechukua hatua hiyo kufuatia
mtumishi huyo kufanya uzembe.
Alisema maamuzi hayo yamefanyika kwa mujibu wa kanuni za utumishi ya
mwaka 2003 jedwali A ,kifungu namba 42 ambapo kuna mapendekezo ya adhabu
ikiwemo kushushwa cheo,kupunguziwa mshahara au kufukuzwa kazi .
Dikupatile alibainisha kwamba ,Benedict hajaitendea haki jamii ambayo
ilikuwa ikihitaji huduma za afya ,hali iliyosababisha mgogoro kati ya wananchi
na eneo analotolea huduma.
Alifafanua ,kutokana na hayo ndipo wakaadhimia kumfukuza kazi ili
kurudisha nidhamu kazini .
“Kama Rais Dkt. John Magufuli anavyotaka kuona uwajibikaji kazini na
kuhudumia wananchi na kama mtumishi awezi anatakiwa kupisha nafasi yake ama
kuwajibishwa nasi tumemua kumuachisha kazi mara moja kwa kitendo chake cha
kutokaa katika eneo la kazi”alieleza Dikupatile.
Hata hivyo alielezea kwasasa wanawachukulia hatua mbalimbali watumishi
wenye makosa ya kiutumishi ambao wapo waliowapunguzia mishahara .
Alisema hatua wanazozichukua zinarejesha heshima kazini na kuleta tija
kwa wananchi .
Dikupatile alisema baraza hilo pia limeadhimia kuwa kabla ya mwaka wa
fedha 2018/2019 wakazi wa Kibong’wa wanaodai fidia yao inayofikia mil.246 ,wawe
wamelipwa fidia hiyo .