Saturday, September 9, 2023

TANZANIA KUVUNA DOLA MILIONI 2.1 KUPITIA UVUVI WA BAHARI KUU

 

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uvuvi wa bahari kuu (DFSA) Dkt. Emmanuel Sweke (kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya COFA kutoka China Bw. Chen Xuejian wakisaini mkataba utakaoiwezesha kampuni hiyo kuvua katika ukanda wa bahari kuu tukio lililofanyika Septemba 08, 2023 jijini Dar-es-salaam. Wanaoshuhudia nyuma yao katikati ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (kulia), Waziri wa Uchumi wa bluu na Uvuvi kutoka Zanzibar Mhe. Suleiman Makame na makatibu wakuu wa wizara hizo.


Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uvuvi wa bahari kuu (DFSA) Dkt. Emmanuel Sweke (kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Albacora Bw. Imanol Loinaz wakibadilishana nyaraka za mikataba itakayoiwezesha kampuni hiyo kuendelea kuvua ukanda wa bahari kuu muda mfupi baada ya kuisaini Septemba 08, 2023 jijini Dar-es-salaam,  Anayeshuhudia tukio hilo katikati ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe Abdallah Ulega na Viongozi na watendaji kutoka Wizarani hapo na ile ya Uchumi wa bluu na Uvuvi kutoka Zanzibar.

...........................

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bahari Kuu (DSFA) zinatarajia kuvuna takribani Dola Milioni 2.1 kupitia mauzo ya leseni 45 za uvuvi wa bahari kuu zilizonunuliwa na wawekezaji kutoka nchi za China na Hispania.


Akizungumza katika hafla ya kusaini mikataba ya mauzo ya leseni hizo iliyofanyika septemba 08, 2023 jijini Dar-es-Salaam, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema kuwa eneo la bahari kuu kwa upande wa Tanzania bara na Zanzibar lina ukubwa wa takribani kilomita za mraba 220,000 ambazo kwa muda mrefu zimekuwa hazitumiki ipasavyo.


“Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ana imani kubwa sana kwetu hivyo ni lazima tuwe wabunifu katika utekelezaji wa maelekezo yake ambayo amekuwa akitutaka tuhakikishe rasilimali hii ya maji ya bahari inatumika kikamilifu kuwanufaisha Watanzania wote” Amesema Mhe. Ulega.


Aidha, Mhe. Ulega amebainisha kuwa eneo la bahari linalomilikiwa na Tanzania bara na Zanzibar lina uwezo wa kuhimili mpaka meli 100 hivyo ametoa rai kwa wawekezaji wengine wenye nia ya kuwekeza kwenye Uvuvi wa bahari kuu kufanya hivyo ambapo amewahakikishia hali ya usalama na mazingira rafiki ya kufanya shughuli zao wakati wote.


Kwa upande wake Waziri wa Uchumi wa Bluu na Uvuvi kutoka Zanzibar, Mhe. Suleiman Makame amewahakikishia wawekezaji hao kuwa Wizara yake kupitia mamlaka ya usimamizi wa Uvuvi wa bahari kuu (DSFA) itasimamia na kutekeleza vipengele vyote vilivyopo kwenye leseni hizo.


Hatua hiyo ni miongoni mwa jitihada zinazochukuliwa na Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha eneo la bahari kuu linatumika vizuri ili kuongeza upatikanaji wa fedha za kigeni hapa nchini.

No comments:

Post a Comment