Serikali inaendelea kufanya mapitio ya sheria ya utumishi ili kupata muarobaini wale wote wanaojitolea katika taasisi mbalimbali za umma.
Hayo yameelezwa leo Jumatatu Septemba 04, 2023 Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Utumishi na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete wakati akijibu swali la Mbunge wa Kiteto Edward Kisau na wabunge wengine waliotaka kujua mpango wa serikali kuwaangalia wanaojitolea na namna ya kuwapa kipaumbele katika ajira.
"Serikali kwasasa inafanya mapitio ya sheria ya utumishi wa umma Sura no. 298, sera ya Menejimenti ya ajira ya umma toleo la pili la 2008, kanuni ya utumishi wa umma ya 2022 na miongozo yake inayohusu masuala ya ajira. Katika kufanya mapitio haya ikibainika kigezo cha kujitolea kinatakiwa kuingizwa kwenye marekebisho ya sheria ya utumishi wa umma basi serikali italeta marekebisho ya muswada wa sheria hiyo bungeni."
Kikwete amesema kumekuwa na miongozo mbalimbali katika suala la kujitolea na ndiyo maana sasa serikali inafanya mapitio ya sheria na miongozo hiyo kuhusu suala la kujitolea, na pindi ikikamilika itafikishwa Bungeni ili wabunge watoe maoni yao kabla ya kuwa sheria.
No comments:
Post a Comment