Thursday, September 14, 2023

LUDEWA YAPOKEA ZAIDI YA BILIONI 1.5 KUKAMILISHA MIUNDOMBINU YA AFYA NA VIFAA TIBA.

 

Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe imepokea zaidi ya Shilingi Bilioni 1.5 kwa ajili ya ukamilishaji na uboreshaji wa miundombinu ya Afya na Vifaa tiba.


Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Victoria Mwanziva ameyasema hayo mara baada ya ufunguzi wa Zahanati ya Chimbo katika Kijiji cha Amani ambayo inatarajiwa kuhudumia wananchi zaidi ya 5,000 waliokuwa wakisafiri umbali wa zaidi ya kilomita Saba kufuata huduma katika makao makuu ya kijiji. Tunamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutubeba kwa Milioni 50 kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati hii ambayo itakuwa mkombozi kwa wananchi hawa. 


Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Dkt. Stanley Mlayi amesema kuanzia mwaka 2020 hadi mwaka huu zahanati 13 zimezinduliwa pamoja na vituo vya Afya vitano katika Wilaya hiyo.


Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, Sunday Deogratias amesema vifaa tiba vilivyokabidhiwa katika kituo cha afya cha Mundindi vimegharimu Shilingi Milioni 150, na Serikali imekwishatenga Milioni 150 nyingine kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba vya kuongezea kwa ajili ya Kituo cha Afya Cha Mundindi ambacho kinaenda kutoa huduma mtambuka kama Upasuaji, Afya ya Mama na Mtoto, Vipimo na huduma mbalimbali.


Kituo cha Afya Mundindi kimegharimu Milioni 500 mpaka kukamilika kwake na ni maendeleo makubwa kwa Kata ya Mundindi, Tarafa ya Liganga- Wilaya ya Ludewa. 

Diwani wa Kata ya Mundindi ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa; Wise Mgina ameshukuru kwa maendeleo haya thabiti kwa ajili ya utoaji wa huduma bora kwa wananchi. 

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi- Wilaya ya Ludewa Ndugu Gervas Ndaki naye ameshukuru utekelezaji wa Ilani unaoendelea Wilayani Ludewa; kwa maslahi ya kusogeza huduma bora kwa wananchi. 







No comments:

Post a Comment