Friday, September 22, 2023

TANZANIA KUFIKIA LENGO LA AFYA KWA WOTE MWAKA 2030.

 

Serikali yaTanzania imejidhatiti kutekeleza malengo ya kufikisha huduma za afya kwa wote hadi ifikapo mwaka 2030.


Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu jana akiwa kwenye kikao cha Huduma za Afya kwa wote kilichofanyika kwenye Mkutano Mkuu wa 78 wa Umoja wa Mataifa Jijini Newyork.


"Tanzania inaungana na wajumbe wengine wa kikao hiki katika kutekeleza azimio hili la kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa huduma bora za afya popote alipo". Amesema Waziri Ummy Mwalimu.


Waziri Ummy amesema kuwa upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi nchini Tanzania zimeendelea kuimarika kutoka asilimia 38 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 43 mwaka 2022 huku bajeti ya afya ikiendelea kuboreshwa maradufu kutoka Dola Milioni 529 mwaka 2019 hadi kufikia Dola Milioni 950 mwaka 2022.


Waziri Ummy amesema kuwa Tanzania imeendelea kutekeleza azimio la Afya kwa wote waliloweka Viongozi wakuu wa nchi kwenye Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa mwaka 2019 kwa kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wote, kuhamasisha wananchi kujiunga na skimu mbalimbali za Bima ya Afya. 


"Serikali ya Tanzania inaendelea kutenga fedha kuhakikisha inafikia lengo la afya kwa wote ikiwemo kuwasilisha muswada wa bima ya afya kwa wote katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania". Amesema Waziri Ummy.


Amesisitiza ili kufikia lengo la afya kwa wote ni lazima huduma za afya ngazi ya msingi ziboreshwe ili wananchi waweze kupata huduma bora za afya wakiwa karibu zaidi na maeneo yao, kuimarisha utoaji wa elimu ya afya pamoja na kuongeza nguvu za mapambano dhidi ya magonjwa na utoaji tiba.


"Tunahimiza ushirikiano wa pamoja kati ya Serikali na wadau wa sekta ya afya kuungana pamoja katika kufikia malengo tuliyoweka ya afya kwa wote hadi ifikapo mwaka 2030 kwa kuwekeza kwenye Ubunifu wa Teknolojia mpya, Rasilimali, mbinu bora za kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza pamoja na Huduma za chanjo na dawa". Amesisitiza Waziri Ummy. 





No comments:

Post a Comment