Friday, September 15, 2023

TUMIENI MITANDAO YA KIJAMII KUELIMISHA KUHUSU MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA- MSIGWA

 


Na Athumani Shomari.

Msemaji Mkuu wa serikali, Gerson Msigwa, amewataka wadau mbalimbali wanaopambana na magonjwa yasiyoambukiza kutumia mitandao ya kijamii katika kutoa elimu kuhusu magonjwa hayo.


Msigwa ambae alikuwa mgeni rasmi katika Mkutano wa kuwajengea uelewa Wahariri wa vyombo vya habari kuhusu magonjwa yasiyoambukiza uliofanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es salaam, amesema kwa sasa watu wengi wanatumia mitandao ya kijamii kwaajili ya kupata habari, kujiburudisha na mawasiliano hivyo ni vyema elimu ya magonjwa yasiyoambukiza ikatolewa pia kupitia mitandao hiyo.


Alisema zamani mitandao ya kijamii haikupewa kipaumbele lakini kwa sasa ni sehemu ya vyombo vya habari na taarifa zinawafikia wengi zaidi kwakuwa mitandao hiyo hupatikana kupitia simu janja ambazo watu wengi wanazo.


Aliongeza kwa kusema kuwa watu wengi kwa sasa wamekuwa wavivu wa kununua na kusoma magazeti lakini simu wanazo na wanazitumia kupata taarifa mbalimbali.


Aliwakumbusha wadau hao kuwa, wanapofikiria kutumia Tv, Radio na Magazeti wasisahau pia kutumia mitandao ya kijamii kufikisha elimu hiyo kama vile Blogs, Facebook, twitter na instagram ambayo inawatumiaji wengi kwa sasa.


Akizungumzia hali ya magonjwa yasioambukiza hapa nchini kwa sasa, Msigwa alisema Mtanzania 1 kati ya 3 ameathiriwa na magonjwa hayo na kupelekea asilimia 40 ya fedha za mfuko wa taifa wa bima ya afya kutumika kuhudumia walioathirika na magonjwa yasiyoambukiza.


Mkutano huo wa kuwajengea uelewa wahariri wa vyombo vya habari umeandaliwa na wadau mbalimbali wakiwemo Serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania, PharmAccese, Norad, Shirikisho la vyama vya magonjwa yasiyoambukiza Tanzania (TANCDA), Shirika la kisukari Duniani (WDF) Chama cha ugonjwa wa kisukari Tanzania (TDA) lengo ni kuleta mtazamo mpya juu ya mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.











No comments:

Post a Comment