Tuesday, September 26, 2023

THAMANI YA UWEKEZAJI NSSF YAONGEZEKA KWA ASILIMIA 111.


Na Mwandishi Wetu


THAMANI ya uwekezaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), imeongezeka kwa asilimia 111 kutoka Sh trilioni 3.4 Machi 2021 hadi kufikia Sh trilioni 7.15 Juni 30 mwaka 2023.


Kwa mujibu wa mfuko huo ongezeko la thamani hiyo ya uwekezaji imechangiwa na kukua kwa thamani ya vitegauchumi, michango ya wanachama na mapato ya uwekezaji.


Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa mfuko huo, Masha Mshomba, katika kikao cha wahariri wa vyombo vya habari na mfuko huo kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina Dar es salaam jana.


Alisema lengo la mfuko huo ni kuhakikisha thamani ya uwekezaji inaongezeka na kufikia Sh trilioni 11.6 ifikapo mwaka 2025/26.


Alisema pia thamani ya vitegauchumi vya mfuko imekua kwa asilimia 55 hadi kufikia Sh trilioni 7.15 Juni 30, 2023 kutoka Sh trilioni 4.62 zilizofikiwa Juni 30 mwaka 2021.


"Wastani wa mapato ya uwekezaji kwa mwezi katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, mwaka 2023, yalifika Sh bilioni 72.06 ikiwa ni ongezeko la asilimia 92 ukilinganisha na Sh bilioni 37.35 zilizokusanywa mwezi Machi 2021," alisema Mshomba.


Aidha, alisema mapato halisi ya Mfuko yameongezeka kutoka wastani wa asilimia 3.31 Machi 2021, hadi kufikia asilimia 5.32 kwa kipindi kilichoishia Juni 30, mwaka 2023.


Alisema mapato ya uwekezaji kwa mwaka yameongezeka kwa asilimia 93 na kufikia Sh bilioni 864.76 katika mwaka wa fedha ulioishia 30 Juni 2023 ukilinganisha na Sh bilioni 448.17 zilizokusanywa katika mwaka wa fedha Juni 30, mwaka 2021.


 


Pia, alisema katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, mwaka 2023,


Mfuko ulilipa Sh bilioni 61.93 kwa mwezi kama mafao kwa wanufaika mbalimbali ikiwa ni ongezeko la asilimia


22 ukilinganisha na Sh bilioni 50.58 zilizolipwa kwa mwezi kipindi kilichoishia Machi Mosi, mwaka 2021.


"Ongezeko hili lilichangiwa na kuongezeka kwa madai ya fao la upotevu wa ajira na mkupuo maalum," alisisitiza.


Aidha, Mshomba alisema malipo ya mwaka ya mafao kwa wanufaika mbalimbali wa Mfuko yaliongezeka kwa asilimia 25 na kufikia Sh bilioni 743.17 katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, mwaka 2023 ukilinganisha na Sh bilioni 594.33 zilizolipwa katika mwaka wa fedha ulioshia Juni 30, mwaka 2021.


Kuhusu idadi ya wanachama alisema kati ya Machi Mosi, mwaka 2021 na Juni 30 mwaka 2023, Mfuko uliandikisha wanachama 547,882 na idadi ya


wanachama wachangiaji iliongezeka kwa asilimia 36 kutoka 874,082 Machi Mosi 2021 hadi kufikia wanachama 1,189,222 Juni 30, mwaka 2023.


Alisema ongezeko hilo limechangiwa na mkakati wa serikali wa kuvutia wawekezaji, pamoja na utekelezaji wa mpango wa Mfuko katika uandikishaji wanachama.


Aidha, alisema wanachama wachangiaji katika Mfuko wameongezeka kwa asilimia 26 hadi kufikia wanachama wachangiaji 1,189,222 Juni 30, mwaka 2023 ikilinganishwa na wanachama wachangiaji 945,029 waliofikiwa Juni 30, mwaka 2021.


Alisema katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, mwaka 2023, makusanyo ya michango kwa mwezi uliongezeka kutoka Sh bilioni 97.67 iliyofikiwa Machi Mosi mwaka 2021 hadi kufikia Sh bilioni 143.05 kwa mwezi katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, mwaka 2023.


 


"Ongezeko hili limechangiwa na kuongezeka kwa waajiri wanaoleta michango kwa wakati na mazingira mazuri ya ufanyaji biashara kwa sekta binafsi," alisema.


Mkurugenzi huyo alieleza kuwa makusanyo ya michango kwa mwaka yameongezeka kwa asilimia 43 hadi kufikia Sh trilioni 1.7 katika mwaka ulioishia Juni 30, mwaka 2023 ukilinganisha na Sh trilioni 1.2 zilizokusanywa katika mwaka ulioishia Juni 30, mwaka 2021.


Mkurugenzi huyo alisema katika kipindi husika, Mfuko umeweza kupunguza siku za ulipaji wa mafao ya wanachama wake kutoka wastani wa siku 68 zilizokuwa Machi Mosi, mwaka 2021 hadi wastani wa siku Juni 30, mwaka huu 2023 kwa mwanachama aliyekamilisha taarifa zake kwa usahihi.


“Kupitia maboresho haya, asilimia 75 ya madai ya mafao yanalipwa ndani ya siku 30, moja kwa moja kupitia akaunti ya mwanachama, mstaafu ama mtegemezi,” alieleza.


Akizungumzia miradi ya uwekezaji ya Mfuko, Mshomba alisema NSSF inaatekeleza miradi mitano ambayo ni miradi ya nyumba za makazi za Dungu, Toangoma, Mtoni Kijichi, jengo la kibiashara na makazi la Mzizima Towers na Hoteli ya kitalii yenye hadhi ya nyota tano, Mwanza.


Alisema changamoto na kasoro za kizabuni na kimikataba zilizokuwepo zilisababisha miradi hiyo kusimama mwaka 2016.


"Miradi hii imepitia hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufanyiwa mapitio na kufanyiwa kaguzi maalum ikiwepo ile ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) iliyokamilika mwishoni mwa mwaka 2020.


Alisema katika kipindi kilichoanzia Machi Mosi, 2021, Mfuko ulitatua changamoto zilizokuwepo na kwa sasa utekelezaji wa miradi yote unaendelea na miradi hiyo inatarajia kukamilika kati ya Juni na Septemba mwakani.


Kuhusu mradi wa Dege Eco Village alisema katika mwaka wa fedha 2023/24, Mfuko unatarajia kuuza mradi huo wenye eneo la ekari 302, Kigamboni jijini Dar es Salaam kwa thamani yad ola za Marekani milioni 220 sawa na Sh bilioni 450 hadi 500. Mradi huo una nyumba 3,750 zilizokuwa katika hatua mbalimbali za ujenzi.


Alisema mradi huo umeuzwa kama ulivyo, ikiwa ni utekelezaji wa uamuzi wa Bodi ya Mfuko na serikali ili kurudisha fedha za wanachama zilizowekezwa awali katika mradi huo.


Akizungumzia mradi wa kiwanda cha sukari Mkulazi alisema unamilikiwa kwa ubia kati ya NSSF kwa asilimia 96 na Jeshi la Magereza asilimia nne na unatarajiwa kushirikisha wakulima 845. Kiwanda kinatarajiwa kuzalisha tani 50,000 za sukari kwa mwaka.



















No comments:

Post a Comment