Tuesday, September 5, 2023

DKT. BITEKO AIKABIDHI OFISI YA WIZARA YA MADINI KWA MAVUNDE

 

Mavunde aainishiwa Vipaumbele vya Wizara ya Madini 2023/24


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko amemkabidhi Ofisi ya Wizara ya Madini kwa Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde ili aanze rasmi kazi ya kuiongoza Wizara hiyo muhimu.


Makabidhiano hayo mafupi yamefanyika Septemba 4, 2023 katika ofisi za wizara jijini Dodoma ambapo Dkt. Biteko ametumia fursa hiyo kumkabidhi Waziri Mavunde vipaumbele vya Wizara ya Madini katika Mwaka wa Fedha 2023/2024.


Vipaumbele hivyo ni Kuimarisha ukusanyaji wa Maduhuli na kuongeza mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa, kuendeleza madini muhimu na madini Mkakati, kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani madini na kuhamasisha uwekezaji na biashara katika Sekta ya Madini.


Aidha, uanzishwaji wa minada na Maonesho ya madini ya vito, kuwaendeleza na kusogeza huduma za ugani kwa wachimbaji wadogo na kuzijengea taasisi uwezo zilizo chini ya Wizara ya Madini ili ziweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.


Dkt. Biteko ametumia fursa hiyo kuwashuru uongozi na Watumishi wa Wizara ya Madini na Taasisi zake kwa ushirikiano mkubwa waliomuonesha katika kipindi chote akiwa wizarani.


Kwa upande wake, Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde amesisitiza atatoa ushirikiano kwa watumishi wa Wizara ili kufikia malengo yaliyowekwa kwa Mwaka wa Fedha 2023/24.


Naye, Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amemshukuru Dkt. Biteko kwa ushirikiano aliompatia katika kipindi walichofanya kazi pamoja na kumtakia Kheri katika majukumu yake mapya.


Akizungumza kwa niaba ya watumishi wote Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula amemuhakikishia Waziri Biteko kuwa watumishi watampatia ushirikiano wa kutosha Waziri Mavunde katika kutekeleza majukumu yake.


Viongozi wengine walioshiriki katika Makabidhiano hayo ni Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali, Wakuu wa Taasisi za Wizara na Watumishi. 





No comments:

Post a Comment