Friday, September 8, 2023

DOLA MILIONI 50 KUWANUFAISHA WAVUVI

 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (katikati) akielezea namna wavuvi watakavyonufaika kutokana na mikopo itakayotolewa na Benki ya CRDB muda mfupi kabla ya uzinduzi wa mpango wa kuwawezesha wavuvi unaoratibiwa na benki hiyo  uliofanyika Septemba 08,2023, jijini Dar-es-salaam. Kulia ni Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Zanzibar, Mhe. Suleiman Makame na kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CRDB, Bw. AbdulMajid Nsekela.

........................................

Mkutano wa Jukwaa la mifumo ya chakula barani Afrika (AGRF) umekuwa na matokeo chanya kwa upande wa program ya “Jenga kesho iliyo njema” (BBT) mara baada ya benki ya CRDB kwa kushirikiana na Mfuko wa kimataifa wa kuhifadhi mazingira (GCF) kutoa kiasi cha Dola milioni 50 zitakazotumika katika utekelezaji wa program hiyo.


Hayo yamebainika wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa mpango wa kuwezesha wavuvi nchini unayoratibiwa na benki ya CRDB.


Tukio lililofanyika Septemba 08, 2023 ambapo Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema kuwa hatua hiyo ni miongoni mwa jitihada kubwa zinazoendelea kufanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha vijana hao wanapata mtaji mara baada ya kumaliza mafunzo yao kwa vitendo.


“Hii inamaanisha kuwa hawa wajasiriamali tunaowatengeneza kwa upande wa sekta za Mifugo na Uvuvi sasa wamepata uhakika kabisa wa kupata mikopo yao na kwa kuwa tayari wana maandiko mazuri ya biashara wataingia moja kwa moja kwenye mnyororo wa thamani wa sekta hizo mbili” Amesema Mhe. Ulega.


Aidha Mhe. Ulega ametoa wito kwa benki hiyo kugeukia upande wa tasnia ya ufugaji wa samaki ambako ameweka wazi kuwa anaamini kuna faida kubwa sana endapo wafugaji hao watawezeshwa rasilimali fedha na zana mbalimbali za kisasa za kufanyia shughuli hiyo.


“Wavuvi ni jamii iliyoonekana kuwa masikini kuliko jamii yoyote na kwa muda mrefu wamekuwa na kipato cha chini sana lakini walichokuwa wanakosa ni namna ya kupata tija katika mnyororo wa thamani wa shughuli zao za uvuvi na mimi wakati wote nimekuwa nikiamini mnayo suluhu ya kuwaondoa wavuvi na wafugaji hawa kwenye hali hiyo kwa sababu ninaamini kabisa Mifugo na Uvuvi ni Utajiri” Ameongeza Mhe. Ulega.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CRDB Bw. AbdulMajid Nsekela amesema kuwa mikopo yenye masharti nafuu itawapa fursa vijana hao kujipanga kwani ina muda mrefu zaidi wa matazamio kuliko aina nyingine zote za mikopo inayotolewa na benki hiyo.


“Vijana watapata muda usiopungua miaka 3 ya matazamio mara baada ya kuchukua mikopo hii hivyo tunaamini kipindi hicho kinatosha kwa wao kufanya shughuli zao na kuanza kupata faida itakayowawezesha kuanza kuirejesha” Amebainisha Bw. Nsekela.


Mpango wa mikopo kwa wavuvi uliozinduliwa leo utawanufaisha wavuvi waliopo kwenye vyanzo vyote vya maji ya asili kwa upande wa Tanzania bara na Zanzibar ambapo vikundi vya vijana na wanawake watapatiwa mafunzo yatakayowawezesha kuainisha aina ya zana wanazotaka kukopeshwa.


Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CRDB Bw. AbdulMajid Nsekela (kushoto) akielezea namna benki hiyo itakavyotekeleza mpango wa kuwawezesha wavuvi nchini muda mfupi kabla ya uzinduzi wa mpango huo uliofanyika Septemba 08, 2023 jijini Dar-es-Salaam. Katikati ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega na kulia ni Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Zanzibar, Mhe. Suleiman Makame.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (katikati) akizindua mpango wa kuwawezesha wavuvi nchini tukio lililofanyika Septemba 08, 2023 jijini Dar-es-Salaam ikiwa ni moja ya matokeo ya Mkutano wa Jukwaa la mifumo ya Chakula (AGRF), Kushoto kwake ni Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Mhe. Suleiman Makame na kulia kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CRDB, Bw. AbdulMajid Nsekela.

No comments:

Post a Comment