Thursday, September 7, 2023

SWALA LA MAFUTA, WAZIRI MKUU ATOA AGIZO KWA NAIBU WAZIRI MKUU

 

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amemuagiza Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Dotto Biteko aendelee kushughulikia suala la changamoto ya upatikanaji wa nishati ya mafuta katika maeneo mbalimbali nchini.


“...Watanzania wapate hii huduma, upatikanaji huu ni muhimu kuhusisha taasisi zote za mafuta na wanunuaji mafuta kwa pamoja ‘bulk’ wakae pamoja na Wizara zinazohusika ikiwemo Wizara ya Fedha na Idara ya Ofisi ya Uratibu Ofisi ya Waziri Mkuu waone namna ya upatikanaji wa mafuta.”


Ametoa maagizo hayo leo (Alhamisi, Septemba 7, 2023) wakati akijibu swali la Mbunge wa Mlalo, Rashid Shangazi katika kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu Bungeni Jijini Dodoma. Mbunge huyo alitaka kufahamu ni upi mkakati wa Serikali katika kuhakikisha Taifa linakuwa na mafuta ya kutosha.


“Lakini pia tupanue wigo wa waagizaji wa mafuta ili tuwe na mafuta mengi nchini kwa usalama wa Taifa letu. Na kama hili litafanyika ndani ya wiki moja tutakuwa tumeshapata majibu na kuwapa taarifa Watanzania.Tutahakikisha nishati hii ya mafuta inapatikana na Naibu Waziri Mkuu atashughulikia hilo.”


Wakati huo huo, Waziri Mkuu ameiagiza Ofisi ya Rais-TAMISEMI iendelee na utaratibu wa kubaini maboma yote kwenye sekta ya afya na elimu ambayo waliyajenga na hayakukamilika, wahakikishe wanaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuyakamilisha kwa sababu yametokana na bajeti zao.


Waziri Mkuu amesema suala la ujenzi wa miradi ya elimu au afya ambayo inahusisha majengo ni mkakati ulioelekezwa katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa kupitia fedha zinazopelekwa kutoka Serikali Kuu ambazo zinapelekwa kujenga majengo hayo kwa thamani ya jengo kutokana na makadirio waliyoyatoa, hivyo wanatakiwa wasimame ujenzi ukamilike kama ilivyokusudiwa.


Aidha, Waziri Mkuu amesema chanzo kingine ni fedha inayotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri zenyewe ambapo wao hupanga mipango ya maendeo yao kupitia bajeti yao na kwenda kujenga, maboma mengi yanatokana na mipango yao, hivyo wayakamilishe.


“Uzoefu tulioupata wakati wa ukaguzi wa miradi hii, majengo ambayo yametekelezwa kwa fedha kutoka Serikali Kuu yamekwenda kama yalivyo na pale ambapo hayakukamilika hatua kali zimechukuliwa. Sasa kwa kuwa maboma mengi yanatokana na mipango yao na kushindwa kuyaendeleza, mkakati wa Serikali ni kuhakikisha maboma yote yanakamilika.“


Ametumia fursa hiyo kuziagiza zifanye tathmini ya miradi yake ione maeneo gani ambayo walianza miradi na wameshindwa kukamilisha na yamebaki maboma ili wapange bajeti ya kila mwaka kuhakikisha maboma hayo yanakamilika. “Halmashauri haziwezi kushindwa kupata shilingi milioni 50 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa zahanati.“


Ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Hawa Mwaifunga aliyetaka kujua ni nini mpango wa Serikali katika kuhakikisha inakamilisha maboma ya kutolea huduma za elimu na afya nchini, miradi iliyoanzishwa na Serikali na nguvu za wananchi ili wananchi hao waweze kuona thamani ya nguvu yao na ya fedha za Serikali zinazopelekwa katika maeneo yao.

No comments:

Post a Comment