Saturday, September 2, 2023

PROF. ASAD ATOA SOMO KWA WAJUMBE WA MENEJMENT YA IJA.

 

Wajumbe wa Menejimenti ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA) wamepatiwa mafunzo ya uongozi wa kimkakati na jinsi ya kukabiliana na changamoto za afya ya akili katika maeneo ya kazi.



Mafunzo hayo yamefanyika tarehe 01/09/2023 katika Ukumbi wa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo (LST) jijini Dar es Salaam na yamefunguliwa na Mkuu wa Chuo cha IJA ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo.



Wawezeshaji wa mafunzo hayo walikuwa ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro(MUM), Utawala na Fedha, Prof. Mussa Assad na Dkt. Garvin Kweka, Daktari wa binadamu na mtaalamu wa masuala ya afya ya akili kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.



Katika nasaha zake, Mhe. Kihwelo amesema kuwa anaamini mafunzo hayo yatawabadilisha wajumbe hao na hivyo kuwafanya waanze kufanya kazi kwa ufanisi mpya.



“Naamini baada ya hizi siku mbili za mafunzo, sote tutatoka tukiwa ni watu ambao tumebadilika," amesema Mhe. Kihwelo.



Katika hatua nyingine, Mhe. Dkt. Kihwelo ameongeza kuwa Chuo kimeandaa mada za Uongozi wa kimkakati na afya ya akili pamoja na kukabiliana na msongo wa mawazo kutokana na umuhimu wa mada hizo katika kuendesha taasisi na kukabiliana na changamoto za kazini ambazo zinaweza kuathiri afya ya akili ya mfanyakazi, hali ambayo inaweza kuyumbisha malengo na dira ya taasisi husika.



Akiwasilisha mada ya “Strategic Leadership in Achieving Organizational Goals,” yaani Uongozi wa Kimkakati katika kutimiza malengo ya taasisi, Prof. Assad amegusia nukta mbalimbali ambazo ni muhimu kwa taasisi yoyote ile ikiwemo ya Umma kuweza kufikia malengo yake na kuzidi kustawi.



Miongoni mwa nukta hizo ni pamoja na taasisi kuwa na malengo na iwe na utaratibu wa kupitia malengo hayo ili kujitathmini wapi ilipo na inaelekea wapi.

Pia amezungumzia suala la mchanganyiko wa watu wenye taaluma tofauti katika ngazi za juu za maamuzi za taasisi kama kwenye za Bodi za taasisi.



“Ni vema bodi za taasisi ziwe na watu wenye sifa tofauti ili kuleta tija kwa taasisi. Sio wajumbe wote wawe wamesoma taaluma moja, hapo sio rahisi kupata mawazo mchanganyiko, mathalani kwa dunia ya sasa huwezi ukawa na bodi halafu haina mtu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(TEHAMA), huyu ni mtu muhimu kwa dunia ya sasa,” amesema Prof. Assad.



Vilevile, Prof. Assad amesisitizia suala la taasisi kuwa na utamaduni mzuri wa kuwajali wateja wake, utamaduni ambao amesema kuwa ni vema ukajengeka kuanzia ngazi ya chini, ikiwemo ya mlinzi mpaka ngazi za juu.



Nukta nyingine, ni matumizi sahihi ya Rasilimali watu na vitu huku akibainisha kuwa taasisi nyingi zinashindwa kufikia malengo yake kutokana na viongozi wa taasisi hizo kuwa na matumizi mabaya ya rasilimali.



Kwa upande wake, Dkt. Kweka ambaye amewasilisha mada ya “Stress Management and Mental Health,” yaani kukabiliana na msongo wa mawazo na Afya ya akili, amesisitizia suala la kulinda afya ya ubongo akisema kuwa kiungo hicho kimebeba eneo muhimu la afya ya akili ya binadamu.



Amesema kuwa ubongo ukiathiriwa na changamoto mbalimbali, husababisha mtu kupata matatizo ya afya ya akili na hivyo mtu huyo kuchukua hatua hasi zikiwemo kujidhuru na kuwadhuru wengine.

Pia amebainisha kuwa ni muhimu watu wakawa na akili hisia (Emotional intelligence) ambayo itawasaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo, kwa kuwa akili hisia inamsaidia mtu kujijua yeye ni nani na kuweza kujidhibiti mwenyewe, ikiwemo pia kuwafahamu watu wengine na kujua jinsi ya kuishi nao.



Akifunga mafunzo hayo ya siku moja, Naibu Mkuu wa Chuo Taaluma, Tafiti na Ushauri Elekezi, Bw. Goodluck Chuwa amesema kuwa mafunzo hayo yatakuwa na tija kwa wajumbe kama wao wenyewe wataanza kuonesha mabadiliko katika utendaji wao wa kazi huku akisisitiza kuwa hiyo ndio mbinu bora zaidi ya kufundisha wengine.



“Njia pekee ya wewe kumfundisha mtu sio kuongea nae bali ni wewe kufanya kitu, wafanyakazi wenzetu, wakishatuona sisi tumebadilika hilo ni somo kubwa kwao kuwa tulipokuja hapa tulijifunza kitu,” amesema Bw. Chuwa.



Naye Kaimu Mkuu wa Idara ya Udahili na Usajili wa IJA, Bw. Nuhu Mtekele akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wajumbe wenzake amesema: “Wajumbe wenzangu tuna deni kwa viongozi waliyotuandalia mafunzo haya, viongozi wetu wengependa kuona matokeo baada ya mafunzo, nasi tunaahidi tutayafanyia kazi vema na yalete tija kwa taasisi yetu ya IJA.”











 

No comments:

Post a Comment