Thursday, September 7, 2023

JAJI MKUU AZINDUA KITABU CHA MKUSANYIKO WA MASHAURI YA UNYANYASAJI WA KINGONO KWA MTOTO.

 

NA MWANDISHI YETU


Mhe. Prof. Ibrahim H. Juma, Jaji Mkuu wa Tanzania amezindua Kitabu cha Mkusanyiko wa Mashauri ya Ukatili wa Kingono kwa Mtoto wa Tanzania na Ireland na kutoa wito kwa wadau kufanyia kazi yale yote yaliyomo ndani ya kitabu hicho.



Uzinduzi huo umefanyika tarehe 05/09/2023 katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam, na umeratibiwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa kushirikiana na Irish Rule of Law International (IRLI) kupitia ufadhili wa ubalozi wa Ireland hapa nchini Tanzania.



“Kitabu hiki kitakuwa hakina maana kama hatutakwenda hatua nyingine kutekeleza mapendekezo yaliyomo kwenye kitabu hiki,” amesisitiza Mhe. Prof. Juma.



Mhe. Jaji Mkuu ameongeza kuwa kitabu hicho kimekuja wakati muafaka ambapo Tume ya Rais ya maboresho ya haki jinai imewasilisha ripoti yake ambayo ina baadhi ya masuala ambayo yanashabihiana na yaliyomo kwenye kitabu hicho.



“Kitabu hiki kimekuja wakati muafaka wakati ambapo Tume ya Rais ya maboresho ya Haki jinai ikiwa imetoa ripoti yake na imebainisha maeneo kadhaa muhimu ambayo yanafana na mapendekezo mengine yaliyomo kwenye kitabu hiki,” amesema Mhe. Jaji Mkuu.



Kitabu hiki kimeandaliwa kwa Ushirikiano kati ya IRLI na IJA na ni moja ya maeneo ya Makubaliano ya Mashirikiano (MoU) baina ya taasisi hizo mbili uliosainiwa Machi 2022, kwa lengo la kuendeleza uhusiano kwenye eneo la haki ya mtoto.



Naye Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), ambaye ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo amesema kuwa ili kuhakikisha kitabu hicho kinaleta tija, watatoa mafunzo kwa baadhi ya Majaji na Mahakimu ambao watakwenda kuwafundisha maafisa wengine wanaohusika na masuala ya usimamizi wa haki.



“Baada ya kutengeneza kitabu hiki, tutakwenda kwa hatua ya pili kwa kutoa mafunzo kama vile mafunzo kwa ajili ya wakufunzi ambayo yatafanyika kwa Majaji na Mahakimu 15, baada ya hapo tutakwenda kwenye kanda saba kutoa mafunzo kwa kuwatumia hao wakufunzi kutoa elimu kwa maafisa wa Mahakama,” amesema Mhe. Jaji Dkt. Kihwelo.









No comments:

Post a Comment