Saturday, September 16, 2023

MAKAMU WA RAIS AWAPONGEZA WATANZANIA WAISHIO NCHINI HUNGARY.

 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ameipongeza Jumuiya ya Watanzania waishio nchini Hungary pamoja na Ubalozi wa Tanzania unaowakilisha nchini humo kwa msaada waliotoa wakati wa kuwaondoa watanzania waliokuwa wakiishi na kusoma nchini Ukraine mara baada ya kuanza kwa vita.
 
Makamu wa Rais ametoa pongezi hizo wakati alipokutana na kuzungumza na Jumuiya ya Watanzania wanaoishi na wale wanaopata elimu ya ngazi mbalimbali nchini Hungary, mazungumzo yaliofanyika Jijini Budapest nchini Hungary. Amewataka kuendelea kushikamana na kushirikiana wakati wote na kuwa na moyo wa huruma na upendo kama baadhi yao walivyojitolea hali na mali kusaidia watanzania waliokuwa wakiondoka eneo la vita.
 
Makamu wa Rais amewasihi watanzania waishio nchini Hungary kuhakikisha wanaishi kwa kufuata sheria katika nchi hizo na kujiepusha na vitendo vya kihalifu vitakavyoharibu taswira ya Tanzania. Aidha amewaasa kuendelea kuitangaza vema Tanzania, kuvutia wawekezaji pamoja na wao kuchangamkia fursa za uwekezaji katika sekta mbalimbali nchini. Pia amewasihi kuendelea kusaidia kwa karibu ndugu na jamaa wenye uhitaji katika familia zao nchini Tanzania kwa kutumia mifumo rasmi ya utumaji fedha.
 
 
Halikadhalika Makamu wa Rais amesema kutokana na lugha ya Kiswahili kuanza kutumika katika Jumuiya mbalimbali kama lugha rasmi, Diaspora wanapaswa kuendeleza lugha hiyo kwa kuitangaza na kuanzisha vituo vya kujifunzia lugha ya Kiswahili katika maeneo waliopo. Aidha amewataka watanzania waishio nje ya Tanzania kutambua jukumu la kwanza la ujenzi wa Tanzania litafanywa na watanzania wenyewe hivyo wanapaswa kutoa mchango wa kila hali katika kuliletea taifa maendeleo.
 
Amewasisitiza wanafunzi kutumia fursa waliopata vema kwa kuvuna maarifa na kutengeneza mahusiano mazuri na mataifa mengine ili kuweza kuijenga Tanzania.
 
Makamu wa Rais amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuleta mabadiliko yenye tija kwa watanzania wote na kueleza kwamba serikali imefanya jitihada katika kuboresha sekta mbalimbali ikiwemo afya, sekta ya elimu, kuimarisha sekta ya nishati, ujenzi wa mindombinu kama vile barabara, reli viwanja vya ndege na barabara. Pia amesema serikali inaendelea na jitihada za kuimarisha demokrasia, sekta ya madini, maji na sekta ya kilimo kwa kuanzisha programu za kuvutia vijana katika kilimo cha biashara.
 
Pia Makamu wa Rais amesema Serikali kwa kutambua ongezeko la watu nchini imedhamiria kuwekeza katika kuimarisha rasilimali watu ili iweze kutumika vema katika kuleta maendeleo. Makamu wa Rais amesema kwa kuzingatia hali hiyo huduma za afya na elimu zimeboreshwa kwa kuongeza vifaa tiba na miundombinu ya afya, kutoa fursa kwa madkatari kupata elimu zaidi pamoja na ujenzi wa vyuo vya ufundi.
 
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mbarouk Mbarouk amesema pamoja na kazi ya kukuza na kudumisha mahusiano ya kirafiki na kidiplomasia kati ya Tanzania na mataifa mengine pia serikali imeendelea kutekeleza kikamilifu kazi ya uratibu wa masuala ya diaspora. Amesema kuanzishwa kwa mfumo wa kuwasajili diaspora kidijitali (Diaspora Digital Hub) umesaidia katika kurahisisha kutambua takwimu za watanzania waishio nje ya Tanzania.
 
Balozi Mbarouk amesema takwimu zitakazopatikiana katika mfumo huo zitawezesha serikali kupanga na kuandaa kwa usahihi mahitaji yanayohitajika ili kuwapa diaspora huduma wanazohitaji kama vile huduma za kibenki, hati za kusafiria, vitambulisho vya taifa na vitambulisho rasmi vya utambuzi wa diaspora wakati wa utekelezaji wa hadhi maalum. 
 
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanafunzi Watanzania wanaopata Elimu nchini Hungary Michael Matonya ameishukuru serikali kwa ufadhili wa wanafunzi wanaosoma nchini humo na kuomba kuongezwa kwa idadi ya wanafunzi wanaosoma nchini humo hasa katika fani za kimkakati za sayansi na teknolojia.
 
Pia ametoa wito kwa serikali kuwekeza zaidi katika kushirikiana na nchi ya Hungary katika sekta ambazo nchi hiyo imepiga hatua kama vile utaalamu katika sayansi ya kompyuta, tehama, uhandisi, urubani, afya, elimu ya mimea na wanyama
 
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
16 Septemba 2023
Budapest Hungary. 




Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza na Jumuiya ya Watanzania wanaoishi na wale wanaopata elimu ya ngazi mbalimbali nchini Hungary, mazungumzo yaliofanyika Jijini Budapest nchini Hungary.

No comments:

Post a Comment