Na Mwandishi wetu- Bagamoyo.
Baadhi ya wajumbe wanaoshiriki Mkutano wa kimataifa wa jukwaa la mifumo ya chakula barani Afrika (AGRF) wametembelea bwawa la ufagaji Samaki la TANLAPIA lililopo Bagamoyo mkoa wa Pwani, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mafunzo na kuangalia fursa mbalimbali zilizopo nchini kwenye sekta ya ufugaji na uvuvi.
Wakiongea mara baada ya kujionea ufugaji wa Samaki kwa njia za kisasa unaofanywa na Kampuni ya TANLAPIA wilayani Bagamoyo wajumbe hao wamesema Tanzania ni miongoni mataifa ulimwenguni ambayo yana Ardhi inayokubali uwekezaji wa aina mbalimbali ikiwemo kilimo na mifugo.
Wameongeza kwa kusema kuwa, kupitia ziara hiyo wameweza kufahamu fursa mbalimbali zilizopo Tanzania ikiwemo kilimo na ufugaji.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tanlapia, Baraka Kalangahe amesema wanaishukuru serikaki ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa ushirikiano mzuri kwa wawekezaji hali inayopelekea kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Kalangahe ameongeza kwa kusema kuwa, bado sekta ya ufugaji Samaki nchini inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa chakula cha samaki kwakuwa asilimia kubwa ya chakula hicho kinaagizwa nje ya nchi.
Aidha ameiomba Serikali kuendelea kuwashawishi wawekezaji waweze kuwekeza kwenye uzalishaji wa chakula cha samaki ili iwe rahisi kwa wafugaji wa samaki kuhudumia samaki wao na hatimae kuwavuna kwa wakati unaostahili ili kuepuka hasara za uendeshaji zinzosababishwa na usumbufu wa kupata chakula hicho cha Samaki.
Wajumbe hao waliotembelea Bwawa la Samaki la Kampuni ya TANLAPIA Bagamoyo ni miongoni mwa wajumbe zaidi ya 3,000 kutoka nchi 70 Duniani, wanaoshiriki katika Mkutano wa siku nne wa Mifumo ya chakula Afrika (AGRF) ambao unafanyika katika Ukumbi wa Kimatifa wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Sar es Salaam kuanzia Tarehe 05 hadi 08 Septemba 2023.
No comments:
Post a Comment