Na Mwandishi wetu- RUVUMA
Wazazi na walezi wametakiwa kuhakikisha wanawalinda watoto dhidi ya vitendo vya kikatili kwa kuhakikisha wanatoa taarifa ili hatua za kisheria zichukuliwe badala ya kuwa sehemu ya kuwaficha watu wanaofanya vitendo hivyo vinavyosababisha madhara makubwa kwa watoto.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama wakati akizungumza na wakazi wa Kata ya Kilagano, Kijiji cha Muungano Zomba , Wilaya ya Songea Vijijini katika ziara yake Jimbo la Peramiho mkoani Ruvuma ambapo amesema wazazi na walezi wanapaswa kuwa mfano bora kwa watoto wao.
Mhe. Jenista amesema vitendo vya ukatili vimekuwa vikikithiri kila kukicha maeneo mbalimbali huku baadhi ya vitendo hvyo vikifanywa na wazazi wenyewe, walezi na hata watu wa karibu ambao wanategemewa na jamii kuwa sehemu ya kuwajenga watoto katika malezi bora.
“Dunia imeharibika na wala siyo siri na lazima tuelezane walindeni hao watoto tutadaiwa na Mwenyezi Mungu, lazima tuwe waangalifu jengeni tabia ya kuwafuatilia watoto kila wanapotoka shule mtoto anafananaje, anaonesha na tatizo? msikilize na kina mama wenzangu mjenge urafiki na watoto siyo mtoto anakusogelea unakuwa mkali hutaki kumsikiliza,”Amesisitiza Mhe. Jenista.
Sambamba na hayo amewahimiza Maafisa Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa Jamii, Dawati la Jinsia, Polisi, Walimu na Wadau wengine wote kuendelea kutoa huduma ya elimu ya malezi na makuzi ya watoto kwa wazazi na walezi ili waelewe wajibu wao wa kulea watoto katika msingi wa haki na usawa wa kijinsia.
“Ndugu zangu watoto wanapitia vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia, vipigo kutoka kwa wazazi, walezi na walimu, kubakwa, kulawitiwa, mimba na ndoa za utotoni pia wanatumikishwa katika kazi zisizoendana na umri wao na hata kukosa haki zao za elimu kwahiyo ni wajibu wa kila mmoja kupaza sauti ”, Alieleza.
Katika hatua nyingine Mhe. Jenista amewaahidi wakazi wa Kijiji cha Maduwalo, Kata ya Maposeni akisema Serikali itaendelea kutatua changamoto zinazowakabili zikiwemo maji na barabara akisema yote yatafanyiwa kazi pamoja na kushirikiana na Mawaziri wenye dhamana ili wananchi wapate huduma hizo muhimu kama lilivyo lengo la Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Aidha katika ziara hiyo Mhe. Jenista aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa bweni la wasichana katika shule ya Sekondari ya Daraja Mbili iliyopo Kata ya Maposeni, Kijiji cha Maposeni, kukagua maendeleo ya ujenzi wa shule ya Sekondari katika Kijiji cha Lugagara , Kata ya Kilagano, kukabidhi vifaa kwa watu wenye ulemavu, vifaa vya michezo pamoja na kuweka jiwe la msingi ujenzi wa nyumba ya Mganga wa Zahanati ya Mdunduwalo kijijini hapo iliyojengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Akitoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa bweni la wasichana katika shule ya Sekondari ya Daraja mbili Makamu Mkuu wa Shule Bw. Damson Wenela ameeleza kuwa ujenzi huo umefikia hatua ya lenta na mpaka sasa umegharimu zaidi ya shilingi milioni 48.
“Mradi wa ujenzi wa bweni unaendelea na mpaka sasa upo hatua ya lenta jumuiya ya shule ya sekondari Daraja mbili inatoa shukrani wa Serikali, Mbunge wetu wa Peramiho Mhe. Jenista Mhagama, viongozi wa Kata na Vijiji na kwa ushirikiano wanaotupa kufanikisha mradi huu muhimu kwa watoto wetu,”Ameeleza Bw. Wenela.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Mdunduwalo kilichopo katika Kata ya Maposeni Bw. Longnus Haule amesema kuwa kuletwa kwa miradi katika kijiji chake imekuwa faraja kwa wakazi wao akisema imekuja kwa wakati muafaka kwani imekuwa kiu yao ya muda mrefu.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Songea Ndg. Thomas Msolwa amebainisha Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mwenyekiti wa Chama hicho ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatekeleza miradi mingi katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea.
“Niwaombe ndugu zangu sisi ndiyo wa kuyasema haya kwa vitendo CCM inatekeleza ahadi zake kwa vitendo kwa sababu ndiyo kiu yake kubwa kuwaletea wananchi wake maendeleo. Mbunge wetu anatimiza kwa vitendo madarasa, barabara, umeme, maji yote hayo anafanya tunayomtuma,”Amebainisha Mwenyekiti Huyo.
No comments:
Post a Comment