Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto, inautaarifu umma kuwa Tanzania inaungana na Nchi nyingine za Afrika
kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika, tarehe 16 Juni 2017.
Chimbuko la Maadhimisho haya ni Azimio
lililopitishwa na uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) mwaka 1990 kwa
lengo la kuwakumbuka watoto wa kitongoji cha Soweto nchini Afrika ya Kusini
waliouawa tarehe 16 Juni, 1976 kutokana na ubaguzi wa rangi.
Watoto hao walikuwa wakidai haki zao za kutobaguliwa
pamoja na haki nyingine za kibinadamu ikiwemo haki ya kupata elimu bora
na hivyo kupinga mifumo ya elimu ya kibaguzi. Kufuatia tukio hili, OAU
iliazimia kuwa tarehe 16 Juni ya kila mwaka iwe Siku ya Mtoto wa Afrika.
Kupitia Maadhimisho haya, Serikali na wadau wengine
tunakumbushwa kuandaa mipango thabiti ya kuwaendeleza watoto na kukuza
ufahamu wa wazazi, walezi na jamii kuhusu utatuzi wa changamoto zinazowakabili
watoto wa Afrika na kuzitafutia ufumbuzi.
Aidha, maadhimisho haya ni fursa ya kutathmini
utekelezaji wa Sera za Taifa zinazohusu maendeleo ya watoto kwa kuwapatia
huduma stahiki ikiwa ni pamoja na afya, elimu, ulinzi na malezi bora ili
kuwarithisha stadi mbalimbali na tunu za kitaifa kwa manufaa yao, familia na
taifa kwa ujumla.
Kwa mwaka huu Maadhimisho haya yatafanyika kimkoa
hivyo kila Mkoa utaadhimisha siku hii kwa kuzingatia mazingira ya
mkoa husika.
Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Maendeleo Endelevu 2030:
Imarisha Ulinzi na Fursa Sawa kwa Watoto” Kaulimbiu hii inawataka wazazi,
walezi, Serikali na wadau wengine kuzingatia wajibu wetu katika kuimarisha
mifumo ya ulinzi na maendeleo ya Mtoto ili iweze kudhibiti changamoto ya
ongezeko la vitendo vya ukatili nchini pamoja na kutoa haki sawa kwa watoto
wote bila ubaguzi
wa aina yoyote.
Wizara inatoa wito kwa wanahabari, Asasi za
Kiraia na wadau wengine kushirikiana na Serikali katika kuadhimisha Siku
hii na kuelimisha jamii kutekeleza kaulimbiu ya mwaka huu. Utekelezaji wa
Kaulimbiu hii utasaidia kuimarisha ulinzi, usalama wa Mtoto na kutoa haki
sawa kwa watoto wote kwa lengo la kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo
mwaka 2030.
Mwisho, tunapenda kuwakumbusha
Watanzania wote kutambua kuwa kila mmoja wetu ana wajibu wa kuhakikisha
kuwa watoto wanapata Haki zao za Msingi kuanzia katika ngazi ya familia
ambayo ni kitovu cha maendeleo ya Mtoto, jamii na taifa kwa ujumla.
1.
Nkinga
KATIBU MKUU
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA
WATOTO – 10/6/2017
No comments:
Post a Comment