Katika siku za hivi karibuni, kumeibuka kikundi kidogo cha matapeli
wanaozunguka katika maeneo mbalimbali hususani vijijini na kuwalaghai vijana
kwamba wao ni watumishi ama waajiriwa wa Jeshi la Polisi na kujipatia fedha
kutoka kwa wananchi/vijana hao kwa udanganyifu kwamba watawapatia ajira ndani
ya Jeshi la Polisi jambo ambalo siyo la kweli.
Jeshi la Polisi nchini, linatoa tahadhari kwa wananchi kwamba ndani
ya Jeshi la Polisi hakuna ajira zilizotangazwa, na hivyo tunawataka wananchi
wote kuwa makini na mtandao huo wa matapeli. Mfumo wa ajira ndani ya Jeshi la
Polisi ni wa wazi na una utaratibu maalum ambao hutangazwa kwa wananchi kwa
mujibu wa taratibu za Jeshi la Polisi.
Kufuatia hali hiyo, Jeshi la Polisi linatoa onyo kali kwa wote
wenye tabia hiyo ya utapeli kuacha mara moja na endapo mtu yeyote atabainika
hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Jeshi la Polisi linatoa rai kwa wananchi wote wenye taarifa za matapeli
hao kuzifikisha haraka katika kituo chochote cha Polisi kilicho karibu ili
sheria iweze kuchukua mkondo wake.
Imetolewa na:
Advera John Bulimba – ACP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.
Makao Makuu ya Polisi.
No comments:
Post a Comment