Serikali imesema haita wavumilia watendaji watakaoshindwa kusimamia
ipasavyo mradi wa Malipo kwa Ufanisi katika kuboresha utoaji wa huduma za
Afya “Results Based Finance” (RBF) ambao hivi sasa unatekelezwa katika
mikoa minane hapa nchini.
Akifungua kikao kinacho wakutanisha Makatibu Tawala wa Mikoa,
Mameya na Wenyeviti wa Halmashauri, Wakurugenzi wa Halmashauri, Waganga Wakuu
wa Mikoa na Wilaya, Maafisa Mipango kutoka mikoa inayotekeleza mradi wa RBF,
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI) Mh. Seleman Jafo, amesema ni lazima kufanyike mabadiliko katika
utoaji wa huduma za afya kuleta matokeo tarajiwa.
Naibu Waziri Jafo ametawataka Mameya na Wenyeviti wa Halmashauri
kuhakikisha kuwa utekelezaji wa Mradi wa RBF unakuwa ni ajenda ya kudumu katika
vikao vinavyofanyika kila mwezi ili kuwezesha kujua kiasi cha fedha zilizoletwa
kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi huo ili kuweza kuboresha huduma za afya kwa
wananchi.
Katika hatua nyingine Waziri Jafo, ameiomba Benki ya Dunia ambayo ndiyo
mfadhili wa mradi wa RBF kuangalia uwezekano wa kuwezesha utekelezaji wa Mradi
wa huu kufanyika nchi nzima ili kuboresha utoaji wa huduma za afya nchini kote.
Naye Mwakilishi wa Benki ya Dunia Bibi Gayle Martine ameipongeza
Serikali ya Awamu ya Tano kwa hatua ambazo inazichukua katika kuhimiza suala
zima la uwajibikaji na kusema kuwa hali hiyo imeongeza shauku ya Wadau wa
Maendeleo kuendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na serikali katika
kuleta mabadiliko ya kiutendaji na utoaji wa huduma za jamii.
Akizungumza katika kikao hicho, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais- TAMISEMI
anayeshughulikia Afya Dkt. Zainab Chaula amesema ili kufikia malengo chanya
yanayotarajiwa katika uboreshaji wa utoaji wa huduma za Afya kila mmoja
katika eneo lake inabidi kutengeneza mpango kazi ambao ndio utakuwa dira ya
utendaji kazi ili kuleta matokeo chanya.
Mradi wa Malipo kwa Ufanisi katika Kuboresha Huduma za Afya nchini
Ulianza mwaka 2015 katika mkoa wa Shinyanga kama eneo la majaribio
ambapo hadi hivi sasa unatekelezwa katika mikoa nane ambazo ni Mwanza,
Shinyanga, Pwani, Simiyu, Geita, Kigoma, Tabora na Kagera
No comments:
Post a Comment